Featured Post

WANAFUNZI LUGALO WALIA NA MIUNDOMBINU KWA WALEMAVU


Na Mwandishi Wetu, IRINGA
WAHITIMU wa kidato cha sita wa Sekondari ya Lugalo mkoani hapa wameiomba Serikali kuisadia kuboresha miundombinu kwa ajili ya wanafunzi walemavu.

Katika Risala yao kwa mgeni Rasmi wamesema pamoja na mafanikio mengi waliyoyapata kupitia shule hiyo bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa uzio, mfumo mbovu wa maji taka kukosekana kwa karatasi maalum za walemavu wasioona pamoja na kutokuwa na miundombinu rafiki kuwezesha kuwa salama katika mazingira ya shule kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum pamoja na uhaba wa waalimu wa Sayansi.
Akijibu Risala ya wanafunzi hao, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma shuleni hapo, Nayman Chavalla, kupitia kampuni inayoitwa Lugalo Associate Company Limited wameanza kukarabati nyumba ya Mkuu wa shule pamoja na ya Makamu wa shule na kuahidi kuwa umoja huo utaendelea kusaidia shule hiyo endapo matokeo ya taaluma yataboreshwa.
Chavalla ameongeza kuwa Umoja huo unayo nia ya dhati katika kusaidia kutatua changamoto za elimu shuleni hapo na kuwataka walimu kufuta daraja sifuri na daraja la nne katika matokeo ya kitaifa ili kuleta motisha kwa wadau wanaochangia maendeleo ya shule.
Pia amesema pamoja na kuwa Serikali inahamasisha Elimu Bure lakini bado jukumu la kujibidiisha katika masomo na kuinua viwango vya ufaulu ni la Mwanafunzi na waalimu wenyewe katika kukuza taaluma yenye viwango.
Mmoja wa wahitimu mwenye ulemavu wa macho, Elizabeth Mwaisoba mwenye umri wa miaka 18 amesema kuna haja kwa Serikali kuendelea kusaidia wazazi wenye watoto wenye uhitaji maalum katika kupata elimu kwani inahitaji kipato kikubwa katika kuwahudia wanafunzi wenye uhitaji wa ziada na kuiomba Wizara husika kutillia mkazo suala la komputa zenye sauti ili nao waweze kwenda sambamba na teknolojia ya sasa.
Felista Mkesela, mwenye ualbino, amesema ipo haja ya waalimu kuona umuhimu wa kuweka vifaa vya kukuza maandishi ya ubaoni na kuongeza muda wa ziada kwa wanafunzi walio na ulemavu wawapo darasani, kwani kuwapa muda sawa na wanafunzi wa kawaida kunaathiri kufanya vizuri katika masomo yao.
Mkuu wa Shule hiyo,  Benjamin Kabungo, amesema kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 63 wenye ulemavu wakiwemo wasioona, albino, wenye uoni hafifu, na walemavu wa viungo na kwamba walimu 4 wa Elimu Dumishi, awali Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1945 na kujulikana kama The H.H Aga Khani, pia imeanzisha ufugaji wa viumbe wakiwemo panya weupe kwa ajili ya kufanya utafiti wa Kisayansi.

Comments