Featured Post

VIWANDA 3,306 VYAANZISHWA KUFIKIA FEBRUARI MWAKA HUU



Na Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia kaulimbiu yake ya kujenga uchumi wa viwanda imeanzisha jumla ya viwanda 3,306 kufikia Februari mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alipokuwa akitoa hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/2019.

“Serikali inahamasisha uwekezaji katika viwanda kwa kutoa vivutio vya kodi na visivyo  vya kodi kwa wawekezaji mahiri, kuendeleza na kuboreshsa miundombinu wezeshi kama vile barabara, reli, bandari, umeme na maji,” alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha amesema, sera, sheria na kanuni pamoja na kufuatilia utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa na kuchukua hatua stahiki kwa wamiliki walioenda kinyume na mikataba ya mauzo.
Aidha, Mikoa na Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga maeneo ya uwekezaji wa viwanda.
Vilevile amesema Serikali imechukua hatua thabiti kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa kutoshsa na wa uhakika kwa ajili ya uchumi wa viwanda. Hatua zilizochukuliwa zinalenga kuongeza uzalishaji wa umeme na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme vijijini na mijini.
“Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya Kinyerezi I (MW 185), Kinyerezi II (MW 240) na mradi wa umeme wa Mto Rufiji (Rufiji Hydro Power Project – RHPP – at Stiegler’s Gorge) utakaozalisha MW 2,100,” alisema Mhe. Majaliwa.
Amesema, Serikali inatekeleza Awamu ya Tatu ya Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) ambao umepangwa kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji 7,873 ambavyo havijapata umeme nchini.
 Ameendelea kueleza kuwa Serikali imeamua kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao matano ya biashara ambayo ni chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku.
Lengo ni kuongeza mapato ya wakulima, kuwa chanzo cha kuaminika cha malighafi katika uchumi wa viwanda na kuendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na fedha za kigeni.
Katika hotuba hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake imeliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi 124,954,230,698 kwa mwaka 2018/2019. Kati ya fedha hizo shilingi 66,162,789,698 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 58,791,441,000 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Pia Bunge liidhinishe jumla ya shilingi 125,521,100,000 kwa ajili ya mfuko wa Bunge.
Kati ya fedha hizo, shilingi 117,205,487,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 8,315,613,000 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.


Comments