Featured Post

RAIS MAGUFULI ATAKA MATOKEO YA UTAFITI WA UVUVI YATUMIKE

Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Ms. Hanne-Marie Kaarstad,akimpatia Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Mhandisi John Wiliam Kijazi zawadi ya kitabu kinachoelezea meli ya utafiti ya Dr Fridtjof Nansen kutoka nchini Norway iliyofanya utafiti wa uwingi wa samaki katika bahari ya Tanzania. Kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ambaye pia alipewa kitabu hicho. Picha na John Mapepele

Mhe. Balozi Mhandisi John Wiliam Kijazi aliyekaa akionyeshwa namna meli ya utafiti ya Dr Fridtjof Nansen kutoka nchini Norway inavyofanya kazi na Kapteni wa Meli hiyo, kushoto kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina na kushoto kwake ni Waziri anayesimamia Sekta ya Uvuvi kwa upande wa Zanzibar. Picha na John Mapepele
Mmoja wa waongozaji meli ya utafiti ya Dr Fridtjof Nansen kutoka nchini Norway (aliyenyoosha mikono ) akitoa maelezo wanavyoiongoza meli hiyo kuanzia kulia Mhe. Balozi Mhandisi John Wiliam Kijazi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Kudumu ya Kilimo Mifugo na Maji, Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina na Katibu Mkuu wa Uvuvi Dkt. Yohana Budeba. Picha na John Mapepele
Viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Mhandisi John Wiliam Kijazi wakiingia katika meli ya utafiti ya Dr Fridtjof Nansen kutoka nchini Norway katika Bandari ya Dar es Salaam wakati watafiti hao walipokuja kutoa utafiti wa awali hivi karibuni. Picha na John Mapepele.

Na John Mapepele, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutumia matokeo ya utafiti wa uwingi wa raslimali za uvuvi za bahari kuu uliofanywa na meli ya utafiti ya Dr Fridtjof Nansen kutoka nchini Norway ili kuleta mapinduzi katika Sekta ya Uvuvi nchini. Meli hiyo imefanya utafiti kwa ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Akizungumza katika Bandari ya Dar es Salam kwenye hafla ya kuikaribisha meli hiyo baada ya kumaliza kufanya utafiti wa siku 12 kwenye bahari ya Tanzania na kuiaga kuendelea na safari ya utafiti, Mwakilishi wa Mheshimiwa Rais katika hafla hiyo Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Mhandisi John Wiliam Kijazi alizielekeza Wizara na taasisi zote za Serikali kutumia tafiti zinazofanywa ili kuleta maendeleo katika sekta husika. “Kufanya utafiti ni jambo moja na kutumia taarifa za utafiti uliofanyika ni jambo jingine, kwa hiyo hakikisheni mnatumia taarifa za tafiti hizi kikamilifu” alisisitiza Mhe. Balozi Kijazi.

Aidha alitoa siku 30 kwa watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) walioshiriki utafiti katika meli ya Dr Fridtjof Nansen washirikiane na watafiti wenzao kuleta matokeo ya utafiti huo Serikalini ili uanze kufanyiwa kazi na hatimaye kuleta tija kwenye Sekta ya Uvuvi.

Wakati huo huo Balozi Kijazi aliishukuru Serikali ya Norway, Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa ufadhili, utaalamu pamoja na kuisaidia Tanzania katika nyanja za sayansi za kwenye maji. “Hii ni furaha kubwa kwa Tanzania hasa kwa kufaidika na meli yenye teknolojia ya hali ya juu kwa upande wa utafiti wa uvuvi kutoka Serikali ya Norway na FAO na tutafaidika zaidi tutakapopata matokeo ya utafiti kwa kujua uwingi wa samaki, mtawanyiko wao na mazingira yake katika maji yetu”.



Alisema utafiti huo ni matokeo ya mazungumzo yaliyofanyika Mwezi Septemba mwaka 2017, baina ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa FAO Bw. Jose Graziano da Silva, Ikulu Dar es Salaam. Alisema miongoni mwa mazungumzo yao yalikuwa ni utafiti wa masuala ya uvuvi ili kujua kiasi na aina ya samaki waliopo katika maji ya Tanzania. Aidha alisema ana tumaini kuwa takwimu na taarifa za uvuvi zitakazopatikana katika matokeo ya utafiti huu zitasaidia katika kuwavutia wawekezaji katika nyanja za uvuvi na biashara zake kwa ujumla.



Akimkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alimshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kumtuma Katibu Mkuu Kiongozi kumwakilisha katika hafla hii na kumuomba kusaidia ununuzi wa meli ya utafiti ili kufanya utafiti na kufuatilia uwingi wa rasilimali za uvuvi bahari kuu kuwa endelevu badala ya kutegemea meli za misaada kutoka nje ya nchi katika kufanya utafiti hapa nchini.

Waziri Mpina alisema utafiti huo uliohusisha maji ya ndani na Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone – EEZ), na ni wa kwanza kufanyika katika nchi yetu kwa Ukanda wa Uchumi wa Bahari, Wizara yake itahakikisha kuwa inatumia kikamilifu taarifa za utafiti huo ili kuongeza tija katika sekta ya uvuvi nchini. Aliiomba Serikali kusaidia ununuzi wa meli ya doria kwenye ukanda wa bahari kuu ili kufanya doria za mara kwa mara katika maji yetu na kulinda rasilimali za nchi.

Aidha Waziri Mpina aliomba Serikali iwekeze zaidi katika kupambana na uvuvi haramu na kuutangaza kuwa janga la kitaifa kwa kuwa hivi sasa taifa linapoteza zaidi ya 75% ya thamani halisi ya pato la sekta ya uvuvi kutokana na uvuvi haramu.

Pia Mpina alimwomba Rais kusaidia kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambayo itaongeza ajira kwa vijana, viwanda kwa ajili ya kuhifadhi na kuchakata samaki, mauzo ya bidhaa mbalimbali kwa ajili ya meli za uvuvi na kubwa zaidi kuinua pato la Taifa kwa ujumla. Alisisitiza kwamba, samaki watakaovuliwa katika maji ya Tanzania watashushwa hapa nchini na kupata takwimu halisi zitakazo ainisha samaki wanaovuliwa hapa nchini. Aidha kwa upande wa wahisani Mpina aliwaomba waendelee kuisaidia Serikali katika kujenga uwezo wa kufanya tafiti na watafiti wa hapa nchini pia waendelee kushirikiana na Wizara kwenye operesheni mbalimbali za kudhibiti uvuvi haramu.

“Tutapambana na wavuvi haramu bila suluhu hadi kuutokomeza uvuvi haramu hapa Tanzania, hatutoshindwa na tumedhamiria kwa dhati kufanikisha hili. Penye nia pana njia, tumepania. Kwa heshima na taadhima ninaamini kuwa Mhe. Rais atafanya kila awezalo kwa uwezo wake ili kuhakikisha kuwa sekta ya uvuvi inakuwa na rasilimali za uvuvi zinasimamiwa kwa njia endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo” aliongeza Waziri Mpina.

Kwa upande wake Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Ms. Hanne-Marie Kaarstad, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanya utafiti huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika Nyanja mbalimbali. Alimuahidi Balozi Kijazi kuwa matokeo ya utafiti huo yatawasilishwa ndani ya kipindi cha siku 30 alizoelekeza Mhe. Balozi Kijazi.

Naye mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani(FAO) hapa nchini, Fred Kafeero alisisitiza kuwa hirika la FAO litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwenye Sekta ya Uvuvi.

Comments