Featured Post

NCHI ILIJAA UVUNDO, RAIS MAGUFULI ANAENDELEA KUISAFISHA!



Na Daniel Mbega
VITENDO vya rushwa na ufisadi uliotamalaki, utendaji wa mazoea wa viongozi wa Serikali na watumishi wa umma, kutowajibika kikamilifu kwa viongozi, urasimu katika utekelezaji  wa huduma za wananchi, mishahara hewa, mikataba mibovu pamoja na deni kubwa la Taifa ni uvundo uliokuwa umetanda nchini Tanzania kwa miaka kadhaa.

Watendaji wa umma kufanya kazi kwa mazowea huku wakilindana hata pale wanapoharibu kazi au mali ya umma ni mambo ambayo yalikuwa kero kubwa kwa wananchi.
Katika kipindi cha nyuma haikuwa ajabu kuona ofisa mmoja akivurunda kazi au hata kutuhumiwa kwa ufisadi, lakini badala ya kuwajibishwa alikuwa akihamishiwa idara nyingine au kituo cha kazi.
Lakini miaka miwili na miezi takriban minne tangu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli achukue madaraka, hali imebadilika na sasa wananchi wanashuhudia namna watendaji wa umma wanavyowajibika licha ya kwamba baadhi ya huduma bado hazijatengemaa kutokana na ufinyu wa bajeti.
Zile kashfa za udungunaizesheni zilizokuwa zikipigiwa kelele huko nyuma, kwamba ukiingia kwenye taasisi moja unaweza kukuta watoto wa vigogo wamejaa, hivi sasa zimepungua au hazipo kabisa, bali wanaopewa nafasi ni wale wenye sifa sitahiki na wanawajibika.
Tumeshuhudia namna Rais Dkt. Magufuli anavyowatumbua viongozi wazembe na kunyoosha mambo ambayo yamekuwa hayaendi sawa kwa muda mrefu.
Tuliona namna wafanyakazi wa umma walivyoanza kubanwa katika suala la kuwahi kazini na kuwajibika wakati hata mawaziri walipoonyesha mfano wa kuwahi ofisini wakiwa wameshika madaftari ya mahudhurio na wale waliochelewa walikiona cha moto.
Hivi sasa ile tabia ya ‘kuzowea kazi’ haipo na watu wanawajibika na huduma zinatolewa bila upendeleo na kwa wakati.
Zamani haikuwa ajabu kuona mama mjamzito anafika hospitali halafu nesi badala ya kumhudumia anazungumza na mtu kwenye simu: “Shoga, mwenzio jana si nilikuwa na yule bwege pale Kijungu Baa… basi akajilengesha nikamnywea halafu nikatimua kwa kupita mlango wa uani…!”
Katika maeneo mengi ya umma, hivi sasa unapofika unaweza kuulizwa hata mara tano na watu tofauti, kila mmoja akitaka kukuhudumia. Nidhamu ya kazi imerejea.
Katika masuala ya kuendeleza uchumi, tumeshuhudia namna serikali inavyojitahidi kuboresha miundombinu mbalimbali pamoja na kuweka mazingira mazuri ya usimamizi wa rasilimali.
Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa kama shamba la bibi ambapo watu walikuwa wakijichotea mabilioni ya fedha watakavyo kwa kushirikiana na wafanyabiashara wasio wazalendo kukwepa kodi na ushuru.
Makontena mengi yalikuwa yamepitishwa bandarini bila kulipiwa ushuru, lakini alipokabidhiwa ofisi tu, Rais Magufuli alianza kuwashughulikia wote waliokwepa ushuru huo wakalipa.
Maofisa waliokuwa wamehusika kwa namna moja ama nyingine nao walishughulikiwa na wengine mpaka sasa kesi zao bado zinaendelea mahakamani.
Mikataba mingi ilionekana kuwa na upungufu mkubwa huku wawekezaji wakizoa rasilimali zetu huku sisi tukipiga miayo, lakini hili nano Rais Magufuli amelishughulikia kwa kiasi kikubwa bila hata kumtazama mtu usoni.
Tuliona namna alivyoshughulikia suala la makinikia, ambapo licha ya wahusika kupiga kelele, bado serikali ilishikilia msimamo wake mpaka wawekezaji hao walipolazimika kukaa mezani.
Tumeona maendeleo mengine kufuatia ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga, ujenzi ambao siyo tu utaimarisha uchumi wa Watanzania, bali utatoa fursa kubwa ya ajira kwa wananchi linakopitia.
Hivi sasa ujenzi wa Reli ya Kati unaendelea kwa kasi, na endapo reli hiyo itakamilika yote na safari za treni ya mwendokasi kuanza, sidhani kama kutakuwa na mtu atakayepanda basi kwenda Mwanza au Kigoma, kwani safari hizo zinazotumia saa 14 sasa zitatumia saa nane tu.
Yapo mengi ambayo Rais Magufuli ameyafanya na anaendelea kuyafanya katika kusafisha uvundo mwingi uliotamalaki nchini ambayo kwa hakika yanaleta taswira njema ya Tanzania yenye neema na nidhamu.
Lakini pamoja na jitihada hizo, bado kuna watu wanaompinga na wengine wanafikia hata hatua ya ‘kuwahurumia’ wezi na mafisadi wakati huko nyuma wao ndio waliokuwa mstari wa mbele kusema serikali ilikuwa inalea uozo.
Viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi walipotumbuliwa, wapinzani wenye kawaida ya kupinga kila jambo wakajitokeza na kusema hatua hiyo ni kinyume na haki za binadamu na wakafikia mahali wakataka kuwatafutia na wanasheria ili kuwatetea mahakamani.
Unaweza kusema Rais Magufuli hajafanya kitu kwa kuisafisha Bandari na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambako ndiko mapato mengi ya serikali yalikuwa yakipotelea? Au wanaobeza waseme wazi kwamba nao ni miongoni mwa wanufaika wa ufisadi huo!
Wapinzani hawa hawana tofauti na ndugu wa mume ambao daima huwa hawaishi visa kila kukicha.
Tunafahamu katika jamii zetu kwamba gubu la mawifi na kejeli ni mambo ya kawaida yanayompata mwanamke kutoka kwa ndugu wa mumewe.
Tumeshuhudia mara nyingi ndani ya jamii pindi ndugu wa kiume anapoamua kuoa, hasa mwanamke anapokuwa siyo chaguo la wanandugu – wazazi ama dada zake – kwamba mkamwana huyo hupata shida sana kuelewana na ndugu wa mumewe.
Kama hakuambiwa mvivu, basi ataambiwa mchoyo; na kama hakuambiwa ana maringo, ndugu wa mume watamtoa kasoro yoyote kwamba ama ni mbaya, havutii na kadhalika, ilimradi tu hawakosi cha kuongea.
Wanawake wengi wanapoolewa hujiandaa kwa mazingira hayo, wakati mwingine hata waume zao huwatahadharisha kuhusu tabia za ndugu zao.
Hata hivyo, maandalizi hayo huwa hayasaidii kwa sababu kila siku ndugu wanaibuka na mazengwe mapya, hawakosi cha kuongea na ukarimu wa mke huwa si kitu kwao.
Kama walivyo ndugu wa mume wasiokosa sababu, wapinzani hao walianza kwa kubeza, kukejeli na kupinga uamuzi mbalimbali wa serikali tena katika mambo ambayo ni ya msingi kabisa ambayo hata wenyewe walikuwa wakiyanadi kwa wananchi kwamba wangeyatekeleza wakiingia madarakani.
Tunafahamu kwamba, baadhi ya wanaopinga jitihada za serikali wanafanya hivyo kwa sababu Dkt. Magufuli hakuwa chaguo lao, lakini maadam ndiye Rais, hawana budi kumkubali.
Dkt. Magufuli anayafahamu hayo yote na alijiandaa kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania walio wengi na kamwe hana muda wa kumfurahi mtu fulani ama kikundi cha watu.
Kama alivyopata kusema kada wa siku nyingi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Steven Mashishanga, kwamba Rais Dkt. Magufuli ni binidamu kama binidamu wengine na asichukuliwe kama malaika licha ya kwamba ana madaraka makubwa ya urais.
Kwa maana nyingine, Rais Magufuli anaweza kukosea mahali na jambo hilo ni la kawaida kwa binadamu yeyote, lakini makosa hayo yasichukuliwe kama kigezo cha kwamba kiongozi huyo anawakandamiza wengine.
Ni wazi kwamba katika utendaji wake wapo watakaoumia na wapo watakaonufaika – kamwe watu hawawezi kuwa sawa.
“Hakuna kiongozi mkuu wa nchi duniani kote ambaye anaweza kufanya kazi kama malaika pasipo kulaumiwa na wananchi anaowaongoza, hata kama anatenda mazuri kiasi gani.
“Magufuli ni kiongozi mzuri sana, lakini sio malaika. Anayo mapungufu madogo madogo ukilingalinisha na mazuri yake mengi, hata hivyo njia nzuri ya kupima utendeji wake ni mwaka 2020, huo ndio utakuwa wakati muafaka wa kupima nini amefanya na nini hajafanya katika kutekeleza ilani ya CCM aliyonadi kweye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” Mashishanga alipata kukaririwa.
Kwa ujumla, Dkt. Magufuli amekwishaonyesha njia ya wapi anataka Tanzania ifike lakini bado anakabiliwa na masuala mengi kwa wakati mmoja na kwa kuwa ameonyesha dhamira ya kutatua kero sugu ambazo zimekwaza maendeleo kwa muda mrefu, ni lazima atalaumiwa na wananchi hususan wale waliozoea kuishi kwa mazoea.
“Huyu si malaika kusema kwamba atafanya mazuri tu ambayo yatampendeza kila mmoja. Wanaomlaumu sasa Rais Magufuli hawakosei, kama wasingemlaumu leo, ni lazima wangelijitokeza tu.
“Kwa kuwa Rais Magufuli ameonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na madudu, wale waliozowea kuvuna vipato vyao kupitia rushwa, kughushi nyaraka na wavivu kazini lazima watamlaumu na kumuona kuwa hafai, lakini mimi nasema utendaji  wa   Magufuli zaidi ya asilimia 90 ni mzuri,’’ alisema.
Inaonekana kabisa kwamba, kilichokuwa kinachangia utendaji mbovu wa serikali ni mfumo uliokuwepo, ambao hauwezi kufumuliwa kwa ghafla kama wengine wanavyotamani.
Rais Magufuli amejitahidi kupambana na mfumo huo kwa staili yake ya ‘kutumbua majipu’ na hata kuwawajibisha watendaji wazembe na wabadhirifu ni sehemu tu ya kupambana na mfumo huo.
Kitendo cha serikali kukusanya mapato mengi kila mwezi tangu serikali ilipoingia madarakani kinadhihirisha kwamba ni hatua kubwa kabisa iliyofikiwa na serikali hiyo katika kuhakikisha kodi zinakusanywa kukuza uchumi wa taifa.
Wapo hata wanasiasa wanaobeza uamuzi wa kufukuzwa ama kusimamishwa kwa watendaji wa serikali wanaotajwa kwa ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ambao ndio wamekuwa kwenye mfumo huo mbovu, lakini wanaobeza wanasahau kwamba ni vitendo hivyo hivyo vya watumishi hao vilivyoifanya serikali yote ionekane haifai.
Ndani ya serikali kumekuwepo na vikundi vilivyounda mfumo wa kifisadi, na hivi ndivyo vinavyovunjwa na serikali bila kuoneana haya. Hili linastahili kupongezwa kwa bidi.
Wanasiasa wanasema Rais Magufuli hajafanya lolote bali anaboresha yaliyokuwepo. Nashindwa kuelewa, hivi hawaoni kuboresha tu yaliyokuwepo ni hatua moja muhimu zaidi kuliko kushughulikia mapya wakati yale ya zamani yanasuasua?
Ni vizuri basi wanaomsifu ama kumkosoa Rais Magufuli wakatumia hekima na busara na wawe na kiasi kwa kuona kwamba yako mambo mengi mema yaliyofanyika na pia kuna mahali anaweza akawa amekosea kibinadamu.
Kumbeza Rais kwamba hajafanya chochote ni kutomtendea haki kwa sababu utendaji wake unaonekana hadharani, labda kama wanaombeza watakuwa na hoja nyingine.
0656-331974

Comments