Featured Post

MITAALA YA ELIMU IBADILISHWE KUWAWEZESHA VIJANA KUJIAJIRI


Rais (mstaafu) Dkt. Jakaya Kikwete akizungumza na wanafunzi wa ufundi.


Na Daniel Mbega
“VIJANA wetu lazima wapate elimu inayoendana na Afrika. Hii ina maana kwamba, elimu ambayo siyo tu inatolewa Afrika lakini pia inayolenga kukidhi matakwa ya sasa ya Afrika.” Hayo ni maneno aliyoyatoa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Oktoba 25, 1961 akizungumzia kuhusu elimu na sheria.

Elimu ndio msingi wa maendeleo duniani na haijalishi kama elimu hiyo ni rasmi au siyo rasmi.
Ndiyo sababu mara baada ya Uhuru, Mwalimu Nyerere alitangaza vita dhidi ya maadui watatu: Ujinga, Maradhi na Umaskini.
Wananchi – hata katika kipindi kile cha mwanzo wa Vijiji vya Ujamaa – siyo tu walihamasishwa kuwapeleka watoto wao shule, bali serikali ikaanzisha Elimu ya Watu Wazima ili kuwafanya Watanzania wengi wajue kusoma, kuandika na kuhesabu.
Hii ilisaidia sana, Tanzania ikawa miongoni mwa mataifa ya Afika yaliyofanikiwa kuufuta ujinga.
Mwalimu Nyerere alisukumwa na taaluma yake ya ualimu, lakini pia ilikuwa nia yake ya dhati ya kuhakikisha kwamba elimu bora inatolewa kwa kila mtu, kwani aliamini elimu pekee ndiyo ingeleta maendeleo ya Tanzania, na hata Afrika kwa ujumla, na ndiyo maana hata katika hotuba zake nyingi alisisitiza umuhimu wa watoto kufundishwa namna ya kujitegemea na siyo kufaulu mitihani tu.
Leo hii mwamko wa elimu umekuwa mkubwa, lakini gharama za elimu zimeongezeka huku ubora wake ukipungua tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma. Wanaoweza kumudu gharama hizo ndio angalau wanawapeleka watoto wao katika shule za binafsi, ambako taaluma iko juu kulinganisha na shule za umma.
Kutokana na ukubwa wa gharama, ndiyo maana mwaka 2016 serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli, ilitangaza kutoa elimu bure katika shule za umma kuwanzia msingi hadi kidato cha nne.
Lakini elimu bure ya sasa haiwezi kuwasaidia watoto wetu kutokana na kuvurugwa kwa mitaala ambayo wakati ule iliwawezesha hata wanaomaliza elimu ya msingi kujitegemea.
Vipindi vya Elimu ya Kujitegemea (EK) katika shule za msingi na sekondari viliwapa fursa watoto kujifunza stadi za kazi, kuanzia kilimo, useremala na mafunzo mengine ya ufundi.
Mwalimu Nyerere aliamini elimu ni ule ujuzi ambao unamwezesha mtu kujitegemea katika mazingira yanayomzunguka, na siyo fikra zile za kale za kuona eti mtu mwenye elimu mahali pake pa kazi ni ofisini tu.
Suala hili mwalimu alilikemea kwa kutumia busara, akifafanua kwa hekima katika hotuba zake mbili alizowahi kuzitoa mjini Tabora (Mei 4, 1967) na mjini Mbeya (Mei 14, 1967) akisema shabaha ya elimu ya msingi lazima ibadilike.
Mwalimu alisikitika baada ya kubaini kwamba miaka ya nyuma wakati nafasi za elimu zilipokuwa chache watu waliona kuwa elimu ya msingi ilikuwa maandalizi siyo ya maisha, bali ya kuendelea zaidi kielimu na kupata kazi za ofisini.
Lakini akasema, kwa kuupanua mfumo wa elimu kwa wote (Universal Primary Education – UPE), elimu ya msingi inaweza kuwa maandalizi ya maisha kijijini na siyo kazi za ofisini tu.
“.. Elimu ya primary kama mnavyojua walimu wenzangu, mimi sikuwahi kufundisha katika primary kwa hiyo sijui matatizo yake ya kufundisha. Nimefundisha katika sekondari tu na nimeanzia hapa hapa Tabora. Kwa hiyo najua matatizo ya sekondari skuli lakini siyo haya ninataka kuzungumza; wala si matatizo ya walimu ninataka kuzungumza; ni matatizo ya nchi,” alisema wakati akiwa Tabora Mei 4, 1967.
“Primary, kama mnavyojua kwanza mpaka sasa ni nusu tu ya watoto wetu ambao wanapata nafasi ya kusoma. Kabla ya uhuru tulikuwa tuna ngazi mbili za shule za primary. Tunayo ile miaka minne ya kwanza, halafu wachache hupenya wakaingia katika miaka minne mingine inayofuata ambayo tunaita middle school. Halafu wachache hupenya wakaingia katika miaka miwili inayofuata iliyokuwa ya standard nine na standard ten ya sekondari skuli. Halafu tena tunachuja chuja.
“Tulikuwa na ngazi nyingi sana za kuchuja chuja. Sisi tukaahidi katika Tanu. Tukaahidi kwamba tutafanya mambo mawili. La kwanza, tutajitahidi kuondoa ngazi hii hapa ya baada ya miaka minne. Pili, kwamba primary nzima tutaifanya miaka minane. Miaka minane ile tukaijaribu ikatushinda. Tukaona mirefu. Tukaipunguza tukafanya kwamba elimu ya primary tutaifanya iwe miaka saba tu basi.”
Mwalimu alisema walikuwa wanaogopa kutokana na wingi wa watoto wanaomaliza shule halafu hawana mahali pa kwenda, yaani wanakosa nafasi za kwenda sekondari wakati huo, kutokana na uhaba wa shule za sekondari uliokuwepo.
“Wazee wanauliza; “Mwanangu nitamfanyaje? Sasa mtoto wangu ameshindwa kwenda darasa la nane, form one. Mimi nitamfanyaje mwanangu?” miezi ya nyuma nilipopita katika mzunguko ule nilioutaja hapa nilikuwa Musoma, wazee wangu kule wakataka kunikabidhi watoto wao. Wanasema:- “Nenda nao huko huko Dar es Salaam. Mimi nitawafanyaje watoto hawa. Wameshindwa! Nenda nao huko wewe utajua la kufanya.” Nenda nao watoto wenu? Mimi watoto wote hawa wa standard seven nitawabeba! Wa Tanzania nzima nitakwenda nao wapi? Mzee anauliza: Sasa mtoto huyu ana miaka 13 tu, 14 tu, mnasema eti alime? Atalimaje mtoto wa miaka 13 tu, 14 tu, atawezaje kulima?
“Swali hilo anayejiuliza si swali la kweli. Upande mmoja si swali la kweli hata kidogo. Ni swali la mazowea tu. Anasahau mzee huyu huyu, ama mwalimu, wakati mwingine mtu mwenye akili nzuri kabisa anakuuliza swali hili… anasema umri wake mdogo mno hawezi kulima. Upande mmoja ni kweli, watoto hawa wana umri mdogo lakini si umri unaoleta problem. Tatizo ni kwamba wamesoma watoto hawa. Maana swali hili haliulizwi kwa mtoto mwenye umri kama huo ambaye hakusoma. Haliulizwi. Wanasaga watoto wale nyumbani, wanaleta kuni… wanalima… wanachunga ng’ombe… wanavuna. Haliulizwi swali hili juu ya watoto ambao hawakupata nafasi ya kwenda shule. Wao wanasema atalimaje na mwanangu kasoma? Kusoma huko kwa kulima ni kusoma gani? Maana nia ya kusoma, madhumuni ya kusoma ni kuepuka jembe. Anasoma mtu aepukane na maisha haya ya vijijini ya majembe majembe haya.
“Elimu ilikuwa ni utaratibu wa kuhama vijijini… ukianza kumsomesha mtoto unajua safari yake ya kuhama imeanza. Ilikuwa inaanza hivi unaiona. Na hasa kwa sababu shule tulikuwa hatuna nyingi, watu waliweza kujua kwamba anakwenda huyu sasa. Halafu baada ya hapo tena nimefanya safari na kumaliza standard four. Kwangu standard five nimekuja Tabora. Kutoka Musoma unakwenda kuifuata standard five Tabora. Ndio unakwenda hivyo! Sasa ikawa ndio mazowea kwamba mtoto akishapata nafasi ya kusoma, kusoma ni kutokana na kilimo. Anakuwa kalani na kalamu anaiweka hapa kichwani. Lazima awe ana kalamu msomaji huyu na shughuli zake hazitokani na kilimo kilimo. Hata unaporudi nyumbani… wanakufanyia kazi wale wa nyumbani. Binti aliyesoma debe kichwani si mahala pake.
“Haya ndio mawazo yetu. Na hii ni kwa sababu siku zile elimu ndivyo ilivyokuwa. Ilikuwa ni kitu cha bahati bahati. Anakipata mtu mmoja kwa bahati, na makusudi yake ni hayo, unampata mtu akawatumikie wakoloni wanaomtaka kwa shughuli fulani fulani… Elimu haikuwa ni haki ya kila mtu.
“Elimu ikishakuwa ni haki ya kila mtu, lazima iwe si elimu ya kuhamisha mtu. Lazima iwe elimu ya kumwezesha mtu yule mahali pake alipo, maisha yake yanakuwa mazuri zaidi.”
Ingawa maneno haya aliyasema Mwalimu Nyerere miaka 57 iliyopita, lakini bado yangali vichwani mwa watu wengi, kwa sababu tunashuhudia kiwango cha elimu kinachotolewa sasa shuleni hakikidhi haja kwa mtoto kujitegemea hapo baadaye.
Maadamu tumekusudia kuwafundisha na kuwaelimisha watoto wetu, ni lazima tuondokane na mawazo kwamba elimu ni ya kuwahamisha wasomi kutoka vijijini.
Lazima tufike mahali tuone kwamba shule zetu zinatoa elimu bora ya kumwandaa mtoto kujitegemea, hata kama hakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya juu.
Ikibidi, lazima tuzibadili – kama inawezekana – shule zetu za Sekondari za Kata ziwe za ufundi stadi ili hata watoto hao watakapomaliza na kushindwa kuendelea na kidato cha tano, basi waweze kujitegemea.
Tukiweka mazingira mazuri ya elimu, tukajenga shule nzuri, madawati ya kutosha, walimu bora wa kutosha, nyumba bora za walimu, tutapeleka na huduma muhimu za kijamii huko vijijini, na kubadilisha mitaala yetu ya elimu kuwa ya kumfanya mtoto ajifunze elimu bora ya kujitegemea, hakika tutakuwa tumetimiza malengo ya Azimio la Musoma – Elimu ni Kazi!
Kila kitu kinawezekana tukiwa na malengo, na tukisimama imara kwa pamoja kushirikiana na wadau kuhakikisha tunayatimiza kwa vitendo malengo tuliyojiwekea, na kisha kutathmini kama tumefanikiwa au la.
0656-331974

Comments