Featured Post

MAGARI HAYA YA WASHAWASHA SASA YATUMIKE KUZIMA MOTO



Na Daniel Mbega
MENGI kati ya magari 50 ya kutema maji ya kuwasha (washawasha) yaliyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 yametelekezwa baada ya kukosa shughuli ya kufanya.
Taarifa za ndani zinaeleza kwamba, ingawa ilipendekezwa kuwa magari hayo yatumike katika Kikosi cha Zimamoto ili kupunguza uhaba wa magari katika kitengo hicho kilicho chini ya Jeshi la Polisi, lakini uamuzi huo bado haujapitishwa.

Mnamo Mei 18, 2016, Serikali, kupitia kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yusufu Hamad Masauni, ilisema ilikuwa katika mchakato wa kuangalia uwezekano wa kubadili matumizi ya magari ya polisi ya washawasha ili yaweze kutumika kuzima moto.
Naibu waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga, aliyeuliza ni kwanini Serikali inanunua magari ya washawasha yasiyo na tija ambayo hutumika nyakati za uchaguzi tu badala ya kununua magari ya zimamoto.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, magari hayo 50 ya washawasha yalikuwa sehemu ya magari 777 yaliyoingizwa nchini kwa ajili ya kupatiwa Jeshi la Polisi, ambapo siku tano kabla ya Uchaguzi Mkuu, yaani Jumanne, Oktoba 20, 2015, Rais (mstaafu) Dkt. Jakaya Kikwete, alikabidhi kwa jeshi hilo magari 399, tukio lililofanyika katika Chuo cha Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Magari 20 kati ya 399 yaliyokabidhiwa siku hiyo yalikuwa ya washawasha na mengine ya kawaida ambayo lengo lake lilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kufanya doria na shughuli zingine za kipolisi.

Magari kununuliwa kwa mkopo
Uchunguzi unaonyesha kwamba, magari yote 777 yaligharimu jumla ya Dola 29,606,100 (takriban Shs. 60 bilioni), ambazo ni fedha za walipa kodi. Taarifa za ndani zinasema, hata kampuni iliyouza magari hayo, Ashok Leyland ya India, haijalipwa fedha zake zote zaidi ya kupokea kiasi cha Dola 10,362,135 (takriban Shs. 21 bilioni) sawa na asilimia 35 ya gharama licha ya mkataba wa malipo kusainiwa Juni 19, 2015 na magari ya kwanza kukabidhiwa Oktoba 20, 2015 kwa Polisi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, ukiacha magari madogo aina ya Toyota Land Cruiser na Leyland Vans, magari ya washawasha ‘yametelekezwa’ kutokana na kukosa shughuli za kufanya kwa sasa.
Wataalam wa masuala ya vyombo vya moto wanaeleza kwamba, yakiachwa kwa muda mrefu bila kutumika yanaweza kuharibika baadhi ya vipuri, hali ambayo itaitia hasara kubwa serikali.
Hata hivyo, wanashauri kwamba, kwa kuwa kazi kubwa ya magari ya washa washa ni kutuliza ghasia na kwa vile ghasia hazipo, ingalikuwa jambo la busara kama Wizara ya Mambo ya Ndani ikayapeleka kwa muda magari hayo kwenye Jeshi la Zimamoto, ambapo kwa kuyafanyia marekebisho kidogo, yangeweza kusaidia kuokoa amali pale ajali za moto zinapotokea.
Aidha, wengine wanashauri kwamba, wizara hiyo pia inaweza kuyapaleka magari hayo kwenye Jeshi la Magereza kwa ajili ya kusaidia kumwagilia mbolea za maji maji kwenye mashamba ya jeshi hilo nchini.
“Kwa kuwa yana uwezo wa kumwaga maji kwa kunyunyiza, nashauri serikali ingeweza kuyapaleka hata Magereza ambako yanaweza kutumika kumwagilia mbolea za majimaji na yatakapohitajika yanaweza kurudishwa polisi kuliko kuyaacha yameegeshwa,” anashauri Mohammed Mtandika, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Mohammed anasema, katika baadhi ya nchi zilizoendelea, magari ya aina hiyo hutumika kumwagilia hata mbolea za asili hasa zinazotokana na kinyesi cha nguruwe baada ya kuzichakata katika hali ya majimaji.
Ujio wa magari hayo katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi ulijenga taswira kwamba Chama Tawala kilikuwa kinaliimarisha Jeshi la Polisi ili kiweze kulitumia kujiokoa na wimbi la mageuzi lililokuwa linaendelea nchini, ambapo kila Mtanzania alitaka kuona ‘mabadiliko’ ya uongozi.
Ingawa Rais Mstaafu JK alikanusha vikali kwamba magari hayo hayakuletwa kwa ajili ya ‘kuwadhibiti wakorofi’ wakati wa uchaguzi, lakini ukweli ni kwamba ulikuwa ni mkakati wa serikali kupitia Jeshi la Polisi kujidhatiti ili kukabiliana na fujo zozote ambazo zingaliweza kutokea.
“Siyo kweli kwamba magari haya yamekuja kwa ajili ya uchaguzi, lakini ninakuomba IGP (Ernest) Mangu usiogope maneno ya watu kwani kusema ni kawaida yao. Jambo la kushukuru ni kwamba, kampeni za mwaka huu kila mgombea amekuwa akipanda jukwaani na kutoa ahadi zao kwa amani na usalama, hii yote ni kutokana na kazi nzuri ya Jeshi la Polisi,” alisema Rais Mstaafu Kikwete. 
Akaongeza: "Endeleeni kufanya kazi kwa weledi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, nafurahi kumaliza muda wangu madarakani huku nikiwa nimetimiza ahadi ya kuwapatia magari Jeshi la Polisi ili kuongeza ufanisi wenu.”
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki, akimshukuru Rais Kikwete kwa kuungana nao, alisema: "Vifaa hivi tulivovipata tutahakikisha tunatumia kwa uangalifu na utaratibu uliopo ili vilete tija kwa sababu tunatambua kwamba ni kodi za watanzania zimetumika kupata magari haya na vifaa vingine.”
Naye IGP Mangu aliongeza wakati huo kwamba, magari mengine 378 yaliyokuwa yamesalia yalitarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwaka 2015 huku akimshukuru JK kwa kutimiza ahadi  ya kuwapatia magari ambayo yatawawezesha katika kufanya kazi kisasa.
Wachunguzi wa masuala ya siasa na uchumi wanaeleza kwamba, uamuzi wa serikali kuliwezesha Jeshi la Polisi kiutendaji ni mzuri hasa kutokana na kukabiliwa na uhaba wa vitendea kazi, lakini wanahoji ni kwa vipi magari hayo yaliletwa wakati wa uchaguzi.
“Hizi ni fedha za walipa kodi maskini wa Tanzania, ingekuwa na kipindi kingine tungesema sawa wanaliwezesha jeshi, lakini kitendo cha kununua magari mengi kiasi hicho kilikuwa ni kama kuwatisha wananchi hasa katika kipindi ambacho kila Mtanzania alitaka kuona mabadiliko ya kweli ya uongozi kutokana na wimbi la kashfa za ufisadi, rushwa pamoja na matumizi mabaya ya madaraka,” anasema Jovin Mwakyambiki, mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Kilichotokea
Baada ya Ashok Leyland kushinda zabuni hiyo mwaka 2013, mkataba ulisainiwa Septemba 5, 2013 kati ya Ashok Leyland Limited na Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuleta magari hayo kwa Jeshi la Polisi.
Magari hayo ya aina tofauti yalinunuliwa kwa kati ya Shs. 150 milioni na Shs. 400 milioni.
Nyaraka mbalimbali ambazo gazeti hili limeziona zinaonyesha kwamba, hadi Oktoba 20, 2015 wakati Rais (mstaafu) Kikwete anakabidhi magari hayo – Toyota Land Cruiser, Leyland Vans na magari ya washawasha – kwa Jeshi la Polisi yalikuwa hayajalipiwa hata senti moja, ambapo malipo ya asilimia 35 (Dola za Marekani 10,362,135) yalilipwa Machi 2016 baada ya Katibu Mkuu wa Hazina kumwagiza Meneja Mkuu wa Benki ya Exim India.
Sehemu ya nakala ya barua ya idhini kumruhusu Meneja Mkuu wa Exim India kuilipa kampuni ya Ashok Leyland inasomeka hivi:
“Buyer Credit of USD 29,606,100 Under Buyer Credit Agreement dated 19th June 2015 Signed between Ministry of Finance and Exim Bank of India for Contract Valued at USD 29,606,100 Between Ashok Leyland India (SELLER) and Ministry of Home Affairs (BUYER).
We wish to inform you that Seller has presented us its claim for Advance Payment duly authorized by the Buyer for an amount of US$ 10,362,135 (US Dollars Ten Million Three Hundred Sixty Two and One Hundred Thirty Five Only), in respect of 35% advance payment under the contract.
We hereby irrevocably authorize Exim Bank of India to make payment of the said amount of US$ 10,362,135 (US Dollars Ten Million Three Hundred Sixty Two and One Hundred Thirty Five Only) being 35% of the contract value to the designated account of the Seller to Exim Bank. We agree that the amount so paid by Exim Bank to the Seller shall deem as an Advance Payment made by Exim Bank to us out of the Credit and date on which Exim bank shall remit the amount from Mumbai shall be deemed date of such advance,
We request Exim Bank to advice us the date and the amount of the advance payment soon after the Exim Bank makes the payment aforesaid.”
Idhini ya malipo hayo ilifanywa kufuatia barua kadhaa za ufuatiliaji kutoka Ashok Leyland India iliyoshinda zabuni hiyo Namba ME/014/PF/2012/2013/G/40, ambapo barua ya kwanza ilisainiwa Februari 3, 2016 na Nivedh Shetty, Meneja wa Operesheni za Kimataifa ikimtaka Katibu Mkuu Hazina kuwatumia taarifa mara malipo ya awali yatakapokuwa yamefanyika.
Baada ya ukimya wa barua ya kwanza, kampuni hiyo iliandika tena barua nyingine Machi 7, 2016 iliyosainiwa na Nivedh Shetty pia kukumbushia malipo hayo hayo na ndipo baadaye Hazina wakaamua kuidhinisha.
0656-331974

Comments