Featured Post

KWA UKUSANYAJI WA MAPATO, UGUNDUZI WA GESI HATUNA HAJA YA KUJIITA MASKINI



Na Daniel Mbega
“NIMEKUWA nasema nchi yetu si maskini. Hii nchi ni tajiri sana, lakini wapo watu wamekuwa wanajinufaisha wao. Wapo tayari wapokee virushwa ili waneemeke wao huku Watanzania wengi wakiumia na kuteseka. Ndio maana nasisitiza kwamba nitaendelea kutumbua majipu ya viongozi mafisadi na wala rushwa.''

Hii ni kauli ya Rais John Pombe Magufuli alipokuwa akisisitiza umuhimu wa uamuzi wake wa kutumbua majipu kwa kuwawajibisha watendaji wa umma ambao ama wametumia vyeo vyao kuhujumu mali na rasilimali za umma kwa faida yao au wamezembea kutimiza wajibu wao huku rasilimali hizo zikiishia kwa wajanja wachache.
Taarifa ya mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaeleza kwamba, katika kipindi cha miezi tisa tu cha Mwaka wa Fedha 2017/2018, kati ya Julai 2017 hadi Machi 2018, mamlaka hiyo imekusanya kiasi cha Shs. 11.78 trilioni likiwa ni ongezeko la wastani wa asilimia 8.46.
Mapato hayo ni makubwa ikilinganishwa na kiasi cha Shs. 10.86 trilioni kilichokusanywa katika kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha 2006/2017.
Mapato haya yanatokana na kodi ambapo kwa mwezi Machi 2018 pekee serikali imekusanya kiasi cha Shs. 1.54 trilioni ikilinganishwa na Shs. 1.34 trilioni zilizokusanywa kwa mwezi Machi 2017, ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 14.49.
Ukuaji wa mapato hayo ya kodi unadhihirisha wazi kwamba, kuna juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha mapato yanakusanywa na fedha za umma hazipotelei kwenye mifuko ya wajanja wachache kama ilivyokuwa zamani.
Tunaelezwa kwamba, kwa muda mrefu serikali ilikuwa inapoteza fedha nyingi kutokana na ukwepaji wa kodi uliokuwa ukifanywa na wafanyabiashara wakubwa pamoja na misamaha ya kodi ambayo haikuzingatia maslahi ya taifa.
Leo hii tunaposhuhudia kuongezeka kwa mapato haya hatuna budi kuamini kwamba kumbe tunao uwezo wa kujisimamia wenyewe na kwa hakika kama makusanyo haya yanapanda hivi, hatuna sababu ya kuendelea kujiita Tanzania ni taifa maskini kama tulivyokuwa tukiaminishwa.
Tunazo rasilimali nyingi ambazo zikisimamiwa vyema zinaweza kutuingizia mapato makubwa na kuondokana na utegemezi unaotufanya tuwe watumwa wa misaada na madeni yanayotokana na mikopo, mingi kati ya hiyo ikiwa imeingiwa bila kuzingatia vipaumbele na kusababisha Deni la taifa lizidi kupaa.
Suala la rasilimali nyingi za taifa – kuanzia kwenye maliasili kama wanyama hadi madini – kuchotwa na wachache limekuwa likipigiwa kelele kwa miaka mingi sasa, ambapo Watanzania wamekuwa wakishuhudia nchi ikibaki na mahandaki huku rasilimali zikichotwa na kuondoka.
Kwamba kuna baadhi ya wawekezaji wanahujumu rasilimali hizo kwa kuwapatia rushwa baadhi ya watendaji wa umma, huku wengine wakihodhi vitalu vingi vya madini bila kuviendeleza na baadaye kuvikodisha wenyewe bila serikali kupata kodi ni mambo ambayo yanadhihirisha namna Tanzania ilivyokuwa imegeuzwa ‘shamba la bibi’ lisilo na mwangalizi.
Kugunduliwa kwa gesi yenye ukubwa wa ujazo wa futi trilioni 2.17 katika Bonde la Mto Ruvu mwaka 2015 kunadhihirisha kuwa Tanzania inao utajiri mkubwa wa rasilimali ya gesi asilia.
Katika ugunduzi huo uliofanywa na Kampuni ya Dodsal Hydrocarbons and Power Tanzania Limited ambayo imekuwa inafanya shughuli za utafutaji wa gesi na mafuta katika Mkoa wa Pwani umezidi kuleta matumaini makubwa kwamba, miaka 10 kuanzia sasa, Tanzania haitakuwa kwenye kundi la nchi maskini, bali zenye uchumi wa kati kutokana na mapato ya gesi asilia yatakayoanza kuvunwa.
Ugunduzi huo unafanya hadi sasa Tanzania kuwa na amana ya gesi yenye ukubwa wa futi za ujazo trilioni 57.27.
Licha ya ugunduzi huo tayari gesi imegundulika katika maeneo ya kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi na eneo la Mnazi Bay huko Mtwara na katika Wilaya ya Mkuranga, Pwani pia kumegundulika kiasi kikubwa cha gesi.
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Dodsal Hydrocarbons and Power Tanzania Limited, Pilavullathil Surendran alisema mwaka 2016 katika mkutano wa wawekezaji wa gesi na mafuta ulioandaliwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa, thamani ya gesi iliyoko katika eneo hilo inafikia Dola za Marekani bilioni sita sawa na Shs. 12 trilioni.
Gesi hiyo iligunduliwa tangu Julai 2015, lakini akaeleza kuwa Serikali imechelewa kutangaza ugunduzi huo kama inavyoagizwa na Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 kutokana na shughuli za uchaguzi.
Sheria mpya inasema kabla ya waziri mwenye dhamana ya gesi kutangaza ugunduzi mpya wa gesi na mafuta ni lazima athibitishiwe na Mamlaka ya Udhibiti wa bidhaa za Petroli na Gesi (PURA).
Kwa gesi iliyogunduliwa tu Bonde la Mto Ruvu inaweza kuzalisha kiasi cha Shs. 30 trilioni baada ya kutoa gharama za uendeshaji ikiwa tutachukulia bei ya gesi asilia kwa viwango vya Desemba 2015, ambapo serikali yenyewe inaweza kupata mpaka Shs. 7 trilioni kwa mgawanyo wa asilimia 30.
Kwa mujibu wa bei za mwaka 2015, nchini Marekani gesi asilia ilikuwa inauzwa takriban Dola za Marekani 10 kwa kila futi za ujazo 1,000 ambao ni wastani wa Dola 0.01 kwa kila futi moja ya ujazo.
Rasilimali hizo ni muhimu kwa kukuza uchumi kwa sababu siyo mapato pekee ya mauzo ya gesi yanayoangaliwa, bali hata fursa zinazotokana na uchimbwaji wa gesi hiyo kwa wakazi wa maeneo inakochimbwa na hata Watanzania kwa ujumla.
Maeneo inakochimbwa gesi yatabadilika kimaendeleo kwa kutoa fursa ya kuanzishwa viwanda baada ya kujengwa kwa miundombinu, lakini pia wananchi wanaweza kutumia fursa hiyo kwa kuwekeza biashara mbalimbali.
Mbali ya kutoa ajira kwa wazawa, bado wananchi wanaweza kuongeza uzalishaji wa tija kwa mazao ya chakula kwa sababu wafanyakazi kwenye maeneo hayo watahitaji chakula na mambo mengine kadha wa kadha.
Shughuli mbalimbali za ujasiriamali zikiwemo ufugaji pamoja na ufundi, zitapata msukumo mkubwa, hivyo kuonyesha ni kwa namna gani rasilimali hizo zinapotumiwa kwa usawa zinaweza kuleta tija kwa Watanzania wote.
Uchimbaji wa gesi katika maeneo ya Mnazi Bay mkoani Mtwara na Songo Songo mkoani Lindi tayari umekwishaleta matunda chanya kwa sababu mbali ya gesi hiyo kutumika katika viwanda na hata majumbani, lakini wananchi wananufaika kwa kupata nishati ya umeme unaozalishwa katikia mtambo wa Mdimba mkoani Mtwara ambao unatumika kwenye mikoa hiyo miwili.
Zaidi ya hayo, halmashauri ya Kilwa imekuwa ikipatiwa gawiwo la faida ya mauzo ya gesi hiyo ambayo ni 0.03%, ambapo inapokea wastani wa Shs. 100 milioni kila baada ya miezi mitatu.
Haya ni mapato makubwa kwa halmashauri ambayo yanasaidia kuhudumia miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii, licha ya kwamba wawekezaji nao wanatakiwa kuchangia kwa hiari, kwa mujibu wa sharia ya uwekezaji, miradi ya maendeleo.
Ikiwa usimamizi kwenye sekta hiyo utaimarishwa, hakika Tanzania itanufaika kwa mapato mengi ya kiuchumi huku Watanzania nao wakifaidika kwa fursa mbalimbali za maendeleo.

0656-331974

Comments