Featured Post

HUHITAJI DAKIKA TANO KUSOMA AKILI ZA WAPINZANI TANZANIA


 Daraja la Mto Kilombero 

Na Daniel Mbega
KWA ujumla, huhitaji hata dakika tano ili kuweza kusoma na kuzielewa akili za wapinzani - wa kisiasa na maendeleo - nchini Tanzania.
Huu ni ukweli ulio dhahiri kwamba, dakika moja tu inatosha kabisa kuwatambua akili zao zikoje, kwa sababu wanachokihubiri ni tofauti na wanachokiamini ama kukifanya.
Wapinzani wa maendeleo nchini Tanzania wako hivi, watapinga serikali kushindwa kuwawajibisha wazembe, lakini serikali hiyo hiyo inapobadilika na kuamua kuwashughulikia wazembe, wala rushwa na mafisadi, wapinzani hao hao wataanza tena kupiga kelele na kupinga.

Haitoshi tu, wapinzani hao hao kuna wakati waliwahi kuomba Tanzania ipate kiongozi ambaye hatawaonea aibu mafisadi na ambaye atakuwa na mtazamo wa kuinua uchumi wa nchi ikiwemo kuboresha huduma mbalimbali za jamii.
Lakini baada tu ya Dkt. John Magufuli kuingia madarakani na kuanza kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo kupambana na mafisadi, wala rushwa, wakwepa kodi na watumishi wazembe, wapinzani wakaanza kupiga kelele kwamba eti ni dikteta.
Wakati Rais Magufuli anapoendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo, bado wapinzani wanabeza na kutoa hoja ambazo hazina kichwa wala miguu.
Kwa muda mrefu Tanzania ilikuwa haina ndege, hata ya kukodi, na kwa bahati mbaya Shirika la Ndege (ATCL) lilikuwa linaingizia serikali hasara kubwa huku likiwa na wafanyakazi zaidi ya 300.
Wapinzani walipiga kelele, wakajitahidi kukosoa, jambo ambalo lilikuwa sahihi na liliungwa mkono na Watanzani wengi kwa kuwa kodi za wananchi zilikuwa zikitumbuliwa na watu ambao walikuwa hawaingizi chochote.
Rais Magufuli, baada ya kutekeleza hatua ya serikali kuhami Dodoma ambayo ilipigwa danadana kwa miaka 45 iliyopita, hatimaye aliamua kwa dhati kabisa kulifufua shirika hilo la ATCL na kuhakikisha serikali inanunua ndege mpya, siyo mtumba wala siyo za kukodi, tena kwa fedha taslimu.
Wengi walipongeza hatua hiyo, lakini upinzani ukaanza wakati alipoamua kununua ndege aina ya Bombardier na siyo aina nyingine.
Rais Magufuli hakujali, akanunua ndege mbili ambazo zimekuwa zikifanya safari nchini na kupunguza adha ya usafiri katika sekta ya anga.
Haikutosha, akaahidi kwamba ndege nyingine ingewasili wakati wowote kabla ya mwezi Mei na nyingine mbili zitawasili Juni mwaka huu wa 2018 zikiwa ni sehemu ya ndege sita ambazo Serikali ya Magufuli iliahidi kuzinunua kwa fedha taslimu.
Jumatatu, Aprili 2, 2018 hatimaye ndege ya tatu baada ya zile mbili za kwanza ya Bombardier Dash 8 Q400 iliwasili nchini na kuzinduliwa na Rais Magufuli, uzinduzi ambao ulishuhudiwa kila kona ya nchini na sehemu nyingine duniani kwa kuwa ulionyeshwa mubashara.
Kabla ya ujio wa ndege hiyo, wapinzani hao wakitumia mitandao ya kijamii walishinda na kukesha mitandao kupinga na kukejeli ujio wa ndege hiyo, huku wengine wakifikia hatua ya kusema kwamba, hata awali hazikununuliwa ndege mbili, bali yalikuwa ni 'mapanga boi mawili tu'!
Wapinzani wengi wa maendeleo walisema hakukuwa na haja ya kununua ndege hiyo kwa sababu haina maana yoyote kwa wananchi walio wengi, kwa kuwa hawatazitumia.
Wakadai kwamba, vipaumbele vya serikali vilitakiwa kulenga kwenye afya, elimu na kilimo, lakini wakasahau kwamba katika sekta hizo tayari serikali imekwishafanya mambo makubwa kwa kukamilisha miradi mingi ya maendeleo kuliko wapinzani wanavyosema.
Hizi ni akili za wapinzani wa kisiasa na maendeleo wa Tanzania, na ndiyo maana nikasema haihitaji utumie muda mwingi kuzijua akili zao.
Leo wapinzani wale wale waliokuwa wakikosoa Tanzania kukosa ndege zake, wanathubutu kusema hakuna haja kwa serikali kununua ndege! Hivi kweli hizi ni akili au nini?
Basi na tuseme hivi, ndege hazitufai, basi hata meli nazo hazitufai maana si wananchi wengi wanaotumia usafiri wa majini!
Na tuseme kwamba hata magari hayatufai kwa kuwa hatuna uwezo wa kuyanunua, badala yake pengine turudi kule kule kwenye ukoloni tuanze kutembea kwa miguu.
Na kama ndivyo, basi hata hatuna haja ya kujenga barabara, reli na madaraja, miundombinu ambayo inagharimu fedha nyingi za umma.
Kwa akili mbovu za wapinzani wa maendeleo, itafika mahali kwamba hata nguo spehseli hazitufai kwa kuwa hatuna fedha za kununulia, badala yake tuvae mitumba, enzi zile tukiziita 'Kafa Ulaya, mazishi Bongo'!
Tunaweza kusema kwamba hata mchele wa kutoka nje hatuna haja nao kwa sababu tunalima mpunga sisi wenyewe - hata kama mchele hautoshelezi mahitaji.
Si hivyo tu, tunaweza kufika mahali - kwa kutumia akili za wapinzani wa maendeleo - tukasema hata dawa hazitufai, kwa sababu tunao waganga wengi wa kienyeji!
Hizi jitihada za Serikali chini ya Rais Magufuli katika kujenga na kuboresha miundombinu zinapingwa sana na wapinzani, ambao dhahiri wanataka kukwamisha maendeleo.
Wapo ambao wanathubutu kusema kwamba, hata wakoloni walijenga reli na barabara, lakini bado wazee wetu waliwakataa na kutaka kujitawala!
Wanasema: "Hata wakoloni walijenga reli, mashule, mabarabara, na kadhalika, lakini bado tuliwakataa na tukadai uhuru."
Ni akili fupi na za kijinga kabisa, kwa sababu hawaelewi kwamba wakoloni walipojenga barabara na reli walilenga kusafirisha malighafi na rasilimali zetu ili kuzipeleka kwao Ulaya kushibisha viwanda vyao.
Barabara na reli tunazojenga zinatusaidia sisi wenyewe kujipatia maendeleo.
Watu wanapinga ununuzi wa ndege, treni ya kisasa, ujenzi wa barabara za juu (flyovers) na kadhalika na wanasema eti vitu hivyo haviwezi kuwa mbadala wa utu, haki na uhuru wa mwanadamu.
Wanaongeza kwamba eti hizi ndege ni mzigo tu kwa mlipa kodi maskini wa nchi hii maana hawajui hata hii ndege imekombolewa kwa gharama kiasi gani huku shirika lenyewe likiripotiwa kuendeshwa kwa hasara.
Wanapewa dhahabu wanatupa na kuokota mawe, siyo wapewe nini jamani!
Tazama kule Libya yaliyowakuta, walipewa kila kitu wakasema Gaddafi amewanyima uhuru. Sasa wanatamani hata unga wa njano hawaupati!
Niseme ukweli tu kwamba, kuna watu wanaumia sana maana kuona maendeleo haya, na hawafahamu kuwa katika mapinduzi ya viwanda (industrial revolution) kuna kitu kinachoitwa trinity boom, ambayo kimsingi imeegemea zaidi kwenye miundombinu, jambo ambalo ndilo linalofanywa na Rais Magufuli, ikiwa ni awamu ya pili katika mapinduzi hayo ya viwanda na awamu ya pili hufanywa na sekta binafsi hususan katika ujenzi wa viwanda.
Inawezekana hawa wapinzani wa maendeleo wana malengo yao ya siri, kwa sababu haya yasipofanyika, na kama tutawasikiliza na kufuata akili zao, basi wataanza tena kukosoa kwamba hiki na kile hakikufanyika.
Tuseme tu ukweli, kwamba Tanzania ya sasa haihitaji mawazo ya kupinga maendeleo kama ya watu wenye akili kama hizi, kwa sababu hao hawaitakii mema nchi yetu.
Tumechelewa sana kuboresha mambo mengi kwa sababu ya sias zisizokwisha, sasa tunahitaji kuchapa kazi na kuwapuuza wenye mawazo ya kuturudisha nyuma.
Anayepinga maendeleo huyo hayuko upande wetu, tumwepuke kama ukoma!
0656-331974

Comments