Featured Post

WAZIRI JAFO AWASIMAMISHA KAZI WAKURUGENZI WA HALMASHAURI ZA UJIJI NA PANGANI



Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
DAR ES SALAAM
27.3.2018
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amewasimamisha kazi Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Kigoma Ujiji na Pangani Tanga kutokana na Ofisi zao kupata hati chafu katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne (Machi 27, 2018), Waziri Jafo alisema Ofisi yake imetekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais Dkt. John Pombe kuhusiana na ripoti ya CAG kuwataja Watendaji hao kuzembea na kusababisha taasisi zao kupata hati chafu.
Aliwataja Wakurugenzi waliosimamishwa kazi na kupisha uchunguzi kuwa ni Bi. Hanji Godigodi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Bw. Sabas Damian Chambasi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.
“Namwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI aunde timu ya Wataalamu kuchunguza utendaji kazi wa Wakurugenzi hao na kunipatia taarifa ndani ya wiki tatu kuanzia leo” alisema Waziri Jafo.
Kuhusu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, Bw. Judethadeus Mboya ambaye kustaafu utumishi, Waziri Jafo alisema uchunguzi dhidi yake utaendelea kufanyika ili kubainisha kuhusika kwake katika kuisababishia halmashauri hiyo kupata hati chafu.
Akifafanua zaidi Waziri Jafo alisema katika taarifa hiyo ya CAG ya mwaka 2016/17, ripoti hiyo ilibainisha kuwa katika ngazi za Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuliwepo na jumla ya vitabu 379 vya makusanyo ya mapato ambavyo havikuwasilishwa kwa CAG kwa ajili ya kufanyika ukaguzi wa mahesabu yake.
Aliongeza kuwa kutokana na taarifa hiyo, Ofisi yake itawasiliana na Wakurugenzi wote kuhakikisha kuwa inawasilisha vitabu hivyo vyenye taarifa na nyaraka za ukaguzi katika ofisi ya CAG haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa Jafo alisema kwa sasa Serikali imepata mafanikio makubwa sana katika suala zima la udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali katika mamlaka za Serikali za Mitaa ikilinganisha na miaka ya nyuma ambao hali ya matumizi haikuwa nzuri.
Waziri Jafo alizipongeza Halmashauri 166 zilizopata hati safi na kuendelea kufanya vizuri katika kusimamia taratibu za matumizi ya fedha za umma pamoja na kuzitaka halmashauri 16 zilizopata hati isiyoridhisha kufanya maboresho katika utendaji kazi ili kupata hati safi.
“Kwa upande wa Halmashauri zilizopata hati chafu naziagiza zibadilishe mienendo ya utendaji kazi katika halmashauri zao sambamba na kuyaagiza Mabaraza ya Madiwani kusimamia vyema Halmashauri hizi katika mipango ya matumizi ya fedha za Serikali” alisema Jafo.

Comments