Featured Post

RAIS MAGUFULI AZINDUA JENGO JIPYA LA TAWI LA CRDB WILAYANI CHATO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi mbalimbalia Chato waliohudhuria kwenye uzinduzi wa jengo jipya la Benki ya CRDB tawi la Chato, Leo Machi 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akikata utepe ishara ya uzinduzi wa jengo jipya la Benki ya CRDB tawi la Chato, Leo Machi 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi mbalimbalia Chato waliohudhuria kwenye uzinduzi wa jengo jipya la Benki ya CRDB tawi la Chato, Leo Machi 2018

Na Mathias Canal, Chato-Geita

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Maguguli Leo 9 Machi 2018 amezindua jengo jipya la Benki ya CRDB Tawi la Chato Mkoani Geita.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe Dkt. Magufuli amesema kuwa uwepo wa Benki hiyo utarahisisha huduma za uhifadhi fedha kwa wafanyabiashara wa samaki Wilayani Chato sambamba na wananchi ambao kwa kiasi kikubwa katika msimu wa Kilimo wamenilima Pamba kwa wingi.

Ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuzifungia baadhi ya Benki nchini na kuzipa onyo zingine ambazo zilikuwa zinafanya kazi kwa mazoea na kwenda kinyume na utaratibu wa sheria za uendeshaji.

Alisema ni bora kuwa na Benki chache nchini ambazo zinaweza kuwahudumia wananchi wengi hususani masikini kama ilivyo CRDB ambayo imewafikia kwa kiasi kikubwa wananchi vijijini hivyo kuendelea kuzifungia Benki zote ambazo zimeshindwa kuendesha vyema shughuli zake na kusalia kufanya huduma Jijini Dar es salaam pekee.

Rais Magufuli ameiomba benki ya CRDB kupunguza riba ya mikopo kwani ni asilimia 16 pekee ya watanzania ndio wanaohudumiwa kwenye Benki nchini hivyo ili wananchi wote waweze kukopa na kuweka mitaji yao midogo kwa ajili ya faida yao ya Sasa na badae ni lazima kuwa na riba rafiki kwa wananchi.

JPM ameipongeza Benki hiyo kwa kuajiri wafanyakazi wapatao 3200 tangu ilipoanza rasmi nchini mwaka 1972 wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya kwanza chini ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeielewa dhana halisi ya kuwasaidia wananchi vijijini kutokana na usumbufu mkubwa wanaoupata katika huduma za kifedha.

Alisema kuwa anayo imani kubwa na Benki ya CRDB kwani naye ni mteja wa benki hiyo hivyo ili kuendeleza mahusiano mema tayari seikali imelipa Deni lote la shilingi Bilioni 16 ambalo ilikuwa inadaiwa na benki hiyo kutokana na mikopo katika miaka ya nyuma.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewahamasisha wananchi kutunza fedha zao benki na kuachana na dhana ya kuhifadhi fedha majumbani jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa fedha hizo na maisha yao wenyewe.

Mhe Magufuli amesisitiza watanzania kuwa wazalendo huku akisema kuwa anatambua kuwa wapo baadhi ya wananchi ambao wamesalia na jukumu la kuandika katika mitandao na vyombo vya habari mambo ambayo ni kinyume na utendaji wa serikali jambo ambalo ni uchonganishi dhidi ya wananchi na serikali yao.

Aidha, Mhe Rais Magufuli alikataa ombi la Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Tanzania Dkt Charles Kimei aliyetaka Benki hiyo kuitwa CRDB JOHN POMBE MAGUFULI-CHATO huku akisema kuwa isalie kuitwa CRDB tawi ka CHATO.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Tanzania, Dkt Charles Kimei ametoa pongezi kwa Rais Magufuli kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Benki hiyo huku akielezea namna ambavyo amekuwa na dhamira ya dhati ya kuwainua watanzania kupitia rasilimali zao jambo ambalo litawanufaisha na kuwainua kiuchumi.

Alisema kuwa Benki hiyo itaendelea kubuni njia nzuri za mikopo huku akisisitiza kuwa Benki hiyo kuendelea kuwasaidia wananchi kupitia SACCOS zao kupata mikopo nafuu ili kujinufaisha kwa kuwa na uchumi imara utakaowawezesha kukuza biashara zao.

Sambamba na hayo pia amekubali ombi la Mbunge wa Jimbo la Chato Mhe Medard Kalemani ambaye ni Waziri wa Nishati la kujenga uwanja wa kisasa wa Mpira wa miguu ambapo kwa niaba ya Benki hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini Benki ya CRDB Tanzania Ndg Martin Mmari amekabidhi Hundi la Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya hatua za mwanzo za kuanza ujenzi wa uwanja huo huku akiahidi Benki hiyo kuwa wadhamini wa timu ya mpira wa miguu ya wilaya ya Chato.

Dhifa ya uzinduzi wa Benki hiyo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Wa Nishati Mhe Medard M.Kalemani (Mb), Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko (Mb), Mkuu Wa Mkoa Wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, Naibu Waziri Wa fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijazi (Mb), Naibu Gavana Wa Benki Kuu Tanzania Dkt Bernard Yohana Kibese, Balozi Wa Denmark nchini Tanzania Mhe Einar Hebogard Jensen, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi CRDB Tanzania Ndg Martin Mmari, Mkurugenzi Mtendaji CRDB Tanzania Dkt Charles Kimei, na Wabunge wa majimbo mbalimbali ikiwemo jimbo la Busanda na Mbogwe.

Comments