Featured Post

MALEZI YA WATOTO WASIACHIWE 'MA-HOUSE GIRL' PEKEE - MEYA ILALA

 
Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko akichangia mada katika mkutano wa wadau washiriki kwenye mradi wa kuboresha elimu kwa makazi yenye msongamano wa watu mkoani Dar es Salaam.

Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea akichangia mada kwenye mkutano wa wadau washiriki kwenye mradi wa kuboresha elimu kwa makazi yenye msongamano wa watu mkoani Dar es Salaam.
Meya wa Manispaa ya Kigamboni, Maabad S. Hoja akichangia mada katika mkutano wa wadau washiriki kwenye mradi wa kuboresha elimu kwa makazi yenye msongamano wa watu mkoani Dar es Salaam.
Mtafiti Mwandamizi na Kiongozi wa Kitengo cha Elimu na Uwezeshaji Vijana wa African Population and Health Research Center (APHRC) Moses Ngware akizungumza katika mkutano kwa wadau wa elimu ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kusaidia maboresho ya elimu kwa makazi yenye msongamano wa watu mkoani Dar es Salaam.
Mmoja wa washiriki katika mkutano wa wadau washiriki kwenye mradi huo akichangia mada.
Sehemu ya washiriki katika mkutano wa wadau wa elimu ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kusaidia maboresho ya elimu kwa makazi yenye msongamano wa watu mkoani Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 
WAZAZI pamoja na walezi wa watoto ambao huwategemea kuacha uangalizi wote wa watoto wao kwa wadada wasaidizi nyumbani maarufu kwa jina la ma-house girl wametakiwa kubadilika kwani utaratibu huo ndio unaochangia kuharibu tabia na malezi kwa watoto. 
Ushauri huo umetolewa na Meya wa Manispaa ya Ilala mjini Dodoma alipokuwa katika mkutano wa wadau wa elimu kuangalia namna ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu kwa makazi yenye msongamano wa watu mkoani Dar es Salaam, ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) na taasisi ya African Population and Health Research Center (APHRC). 
Akizungumza katika majadiliano, Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko alisema licha ya uwepo wa changamoto nyingine na hatarishi kwa watoto bado suala la maadili na malezi limezi kuwa janga kwa kile wazazi wengi kwa sasa kuacha malezi ya watoto kwa wadada wa kazi (ma-house girl) peke yao. 
Alisema wadada hao wa kazi wengine wanatoka katika jamii mbalimbali na zingine zisizo na maadili jambo ambalo linazidi kuchangia kuporomoka kwa maadili na tabia njema kwa familia nyingi. 
"...Wazazi wengi sasa hivi tupo 'busy' suala la malezi ya watoto wetu tunawaachia wafanyakazi wa ndani (ma-haouse girl) hili nalo linachangia kuwaharibu watoto kitabia, tushirikiane kuwalea watoto wetu kimaadili, na kama umebanwa basi tuwapeleke kwenye vituo maalum vya kulelea watoto (Day Care Centre) hawa wamesomea kulea watoto," alisema Meya wa Ilala, Kuyeko. 
Kwa upande wake Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Rose Ileta alisema ongezeko kubwa la watu mijini haswa Dar es Salaam linatokana na fursa zinazopatikana katika jiji hilo na huduma mbalimbali za jamii, hivyo kushauri viongozi wengine kuendelea kuboresha huduma za kijamii maeneo yao na kuchochea vivutio vya fursa. 
Alisema suala hilo linaweza kufanywa na viongozi popote walipo iwe vijijini na hata mijini ikiwemo hata kuwashirikisha wadau wa maendeleo ya jamii (wafadhili), kwani viongozi wengine wameweza kufanya mjini na kubadili maeneo yao. 
Alisema kuboresha huduma za kijamii na utafutaji wa fursa za maendeleo mikoani kunaweza kupunguza kimbilio la watu mijini na kupunguza msongamano. 
Naye Mtafiti Mwandamizi na Kiongozi wa Kitengo cha Elimu na Uwezeshaji Vijana wa taasisi ya African Population and Health Research Center (APHRC), Moses Ngware ambao ni wafadhili wa mradi huo aliwataka wadau hao kujadiliana kwa mafanikio na kuhakikisha wanaibua takwimu halisi zitakazosaidia kumaliza changamoto katika utekelezaji wa mradi huo. 
"...Mkutano huu kwenu ni muhimu sana, taasisi kama Serikali na watunga sera wanahitaji takwimu halisi zinazoweza kuwashawishi kufanya mabadiliko pale kunakoonekana kuna dosari...hii ni kazi yenu kuibuka na tafiti zenye uhalisia na ushawishi," alisisitiza Bw. Ngware akizungumza na washiriki kwenye mkutano huo.

Comments