Featured Post

GLOBAL FUND YAKUNWA NA UTENDAJI WA RAIS MAGUFULI


Rais Dkt. John Magufuli

Yatoa msaada wa magari 181 kwa Tanzania bila masharti
·         Yaahidi kuendeleza ushirkiano na Tanzania

Na Jonas Kamaleki
Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kitaifa na kimataifa kwa uwajibikaji uliotukuka na vita dhidi ya rushwa na ufisadi wa kila namna.
Kutokana na utendaji huu unaozingatia sheria,kanuni na taratibu, mashirika ya kimataifa zikiwemo nchi zilizoendelea na zinzoendelea zimeonyesha dhahiri kupendezwa na kazi nzuri zinzofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Hii imedhihirika hivi karibuni pale ambapo Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund), Linden Marrison  Global Fund kutoa msaada wa magari 181 kwa ajili ya kusambaza dawa za binadamu katika vituo vya afya na hospitali zilizopo nchini.
Hii ni mara ya kwanza tangu Tanganyika (Tanzania) ipate uhuru kupata msaada wa magari mengi kwa pamoja kwa ajili ya  Bohari ya Dawa (MSD). Jambo hili limefanyika kutokana na umakini wa Serikali ya Rais Magufuli ambao umejenga imani kubwa ndani na nje ya nchi.
Magari haya 181 pamoja na mengine yaliyokuwepo yatatumika kusafirisha dawa katika mikoa yote ya Tanzaniaili kurahisisha upatikanaji wa dawa hadi vituo vya afya vya vijijini ambavyo awali ilikuwa ni shida kuvikia kwa wakati.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria (Global Fund), Linden Marrison anaisifia Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inazofanya na kuahidi kushirikiana nayo.
Marrison anasema uwazi katika kuendesha serikali na vita dhidi ya rushwa vinaifanya Global Fund kuiamini Tanzania na kuendelea kushirikiana nayo na ndiyo maana wamekubali kuipa msaada wa magari 181 bila masharti.
Upatikanaji wa dawa kwa sasa nchini unaridhisha, na hii ni kwa sababu ya juhudi za makusudi zilizofanya na Serikali ya Rais Magufuli kuongeza bajeti ya dawa toka shilingi bilioni 31 hadi bilioni 269. Haya ni mabadiliko makubwa ambayo yameondoa dhana iliyokuwa imejengeka kuwa hospitali za serikali zinatoa tu Panadol na Asprin.
Rais Magufuli anadhihirisha hili anaposema kuwa bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikiongezeka na kwa mwaka wa fedha 2017/18 imefikia  shilingi trilioni 2.2.
Jitihada hizi za kuboresha sekta ya afya nchini zinashuhudiwa na Waziri mwenye dhamna ya Afya, Ummy Mwalimu ambaye anampongeza Rais Magufuli kwa kulipa kipaumbele suala la afya.
Ummy Mwalimu anamshukuru Rais Magufuli kwa kuongeza bajeti ya Wizara yake hadi kufikia trilioni 2.2 kwa mwaka wa Fedha 2017/18, jambo ambalo Waziri anasema halijawahi kutokea tangu nchi hii inapata uhuru takriban miaka 57 iliyopita.
Suala la kununua dawa kwa wingi toka nje, ni jambo ambalo linamkera Rais Magufuli. Hivyo wito wake kwa wawekezaji wa ndani ni kujenga viwanda vya dawa hapa nchni ili kupunguza uagizaji wa dawa hizo.
" Tanzania tuna wasomi wengi, tuna waandisi wengi , pamba za hospitali tunaagiza China wakati sisi ndio wakulima wa pamba, maji ya dripu tunaagiza Uganda, hivi Profesa Janabi wanafunzi wako hakuna ambao wanaweza kutengeneza maji hayo", anashangaa Rais Magufuli.
Rais Magufuli anasema Serikali iko tayari kuwawezesha watanzania kuwekeza katika viwanda vya dawa hapa nchini. Amasema kuwa asilimia 94 ya dawa zinazotumika hapa nchini zinatoka nje na ni asilimia 6 tu zinanunuliwa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Rugambwa Bwanakunu anasema kuwa mchakato wa kununua dawa nje ya nchi pamoja na kupunguza kutoka miezi 9 hadi wastani wa kati ya miezi 6 na 4 kulingana na aina ya dawa na kifaa tiba kinachonunuliwa, muda huu bado anaona ni mrefu  na unaligharimu taifa fedha nyingi.
" Kwa mwezi tunaagiza na kuleta makontena karibu 50 ya maji na makontena 20 ya pamba, Tanzania ina viwanda 13 tu vya dawa, vyenye mkataba na MSD ni vitano tu, hii haikubaliki kabisa", anasema Bwanakunu.
Rais Magufuli amewahikikishia watanzania kuwa soko la dawa hapa nchini ni la kutosha kwani Tanzania imepewa jukumu la kuuza dawa katika nchi zote za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Ametoa wito kwa wawekezaji hasa sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa ili fedha nyingi za kununulia dawa zibaki humu humu nchini na kutoa ajira kwa watanzania.
MSD inahudumia vituo vya afya zaidi ya 7,309 nchini, hili ni soko tosha kwa yeyote anayetaka kuwekeza katika viwanda vya dawa.
Watanzania ni wakati mwafaka kuweza kutembea na maono ya Rais magufuli ya kupunguza kuagiza dawa toka nje na badala yake kutenegeza dawa wenyewe kwa kuanzisha viwanda hapa nchini.
Ujenzi wa viwanda vya dawa utawezesha watanzania kuokoa fedha za kigeni ambazo zinaweza kutumika kwa masuala mengine ya maendeleo nchini Tanzania.
Kupitia viwanda hivyo, ajira hasa kwa vijana zitaongezeka, jambo ambalo litaongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwani kodi ya Serikali itakusanywa kutoka kwenye viwanda hivyo.
Mazingira ya uwekezaji nchini yameboreshwa kwa kupunguza ama kuondoa vikwazo katika vibali vya uwekezaji.
Kwa mujibu wa Mkurugezi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Geofrey Mwambe, Tanzania imebadilika kwa kuweka pamoja watoa vibali vinavyohusika na uwekezaji. Kimetengenezwa kituo cha pamoja kilichopo TIC.
Katika kituo hicho, taasisi zinazohusika na kutoa vibali vya uwekezaji zina wawakilishi katika kituo hicho. Ofisi za Uhamiaji, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Idara ya Kazi, zina maafisa kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa vibali kwa wawekezaji akiwemo afisa toka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
"Mwekezaji akiwasilisha maombi yake ya kibali, yanashughulikiwa ndani ya siku tatu na jibu linapatikana kwa sababu taarifa nyingi kuhusu matakwa ya vibali vya uwekezaji yako kwenye tovuti ya TIC", anasema Mwambe.
Ikumbukwe kuwa kabla ya kuwa na kituo kinachojulikana kama One Stop Centre usumbufu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba baadhi ya wawekezaji walikatatamaa ya kuwekeza nchini.
Juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuondoa ukiritimba zimezaa matunda hasa katika eneo la uwekezaji. Hivyo wenye nia ya kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza dawa wafanye hivyo kwani mazingira wezeshi yako tayari.


Comments