Featured Post

DKT. MWAKYEMBE ASIKITISHWA NA KAULI YA DIAMOND



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb) amesikitishwa na kauli zilizotolewa na mwanamuziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul (Diamond) wakati akihojiwa na mtangazaji wa kipindi cha PlayList Bw. Omary Tambwe (Lily Ommy) wa kituo cha redio cha Times Fm ya Jijini Dar es Salaam. Mwanamuziki Diamond alitoa maelezo yaliyoshutumu hatua mbalimbali ambazo Serikali imezichukua katika kutunza na kulinda maadili ya Kitanzania kwenye tasnia ya Sanaa za muziki.

Waziri Mwakyembe amesema  maamuzi ya kuzifungia baadhi ya nyimbo na wasanii wawili kwa kukiuka maadili yalifanywa kwa mujibu wa sheria, na siyo kwa utashi wa Mheshimiwa Naibu Waziri Shonza ambaye  anamshutumu. Diamond atambue kuwa Serikali ina taratibu zake na maamuzi ya Naibu Waziri ni maamuzi ya Wizara.

Aidha, amesema kuwa vikao na wasanii vimefanywa mara nyingi sana lakini Diamond hakuwahi kuhudhuria vikao hivyo, na si wajibu wa Serikali kumfanyia kikao cha peke yake.

“Sheria ni ya watu wote bila kujali umaarufu au nafasi ya mtu katika jamii, hivyo msanii Diamond anapaswa kutii Sheria na mamlaka zilizowekwa” amesisitiza Dkt. Mwakyembe.

Dkt. Mwakyembe ameeleza kuwa si busara kwa Diamond kushindana na Serikali, endapo anaushauri wowote ni vyema akawasilisha kwa njia sahihi lakini si kwa kumshambulia Naibu Waziri kwa dharau na kejeli kama alivyofanya. Aidha, Dkt. Mwakyembe amesema kwamba Diamond kwa mafanikio aliyoyapata kwenye muziki, anatarajiwa kuwa mfano bora kwa wanamuziki wenzake.

“Napenda kuwakumbusha wasanii wote kwamba Sanaa ni kazi kama zilivyo kazi zingine, hivyo pamoja na kuwa na kipaji hicho, wasanii wanatakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayoisimamia tasnia ya Sanaa kama ilivyo kwa tasnia nyingine”, amesisitiza Dkt. Mwakyembe.
Lorietha Laurence,
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
21/03/2018

Comments