Featured Post

HAKI ZA WATOTO NA UTEKELEZAJI WAKE


Na Blandina Manyanda (Wakili)
Watoto wanahaki nyingi katika jamii wakili, Blandina  Manyanda anatueleza baadhi ya haki za kisheria za watoto.
Kabla hatujaendea mbele, msomaji nakuomba uzingatie mambo mawili muhimu ambayo ni falsafa itakayokuongoza maishani:
 
(i)                Hakuna mtu yeyote awe tajiri ama masikini, wa kike ama wa kiume, mwenye ajira asiye na ajira na mwenye akili timamu ama punguani, ambaye wakati fulani hakuwahi kuwa mtoto kwa hiyo utoto ni sehemu ya maisha ya mwanadamu awaye yoyote yule, na yale yanayofanywa na watoto leo yakatuchukiza ama yakatufurahisha ni muendelezo tu wa yale tuliyoyafanya sisi tukayaacha mahali fulani. Hakuna kinachofanywa na watoto ambacho hakina chimbuko katika jamii na hasa katika familia zetu.
(ii)             Hakuna mtoto hata mmoja ambaye anakuja ulimwenguni humu kwa ridhaa yake mwenyewe, kwa kila mtoto anayezaliwa ulimwenguni, wenye maamuzi mazito ya kwamba azaliwe ama la ni wazazi wake wawili.

Msisitizo wangu hapa ni kwamba wote tunapozaliwa, hatuwaombi wazazi kwamba tunaomba tuzaliwe.
Ni mipango tu ya wazazi, ama hata wakati mwingine ni utaratibu wa kukidhi tamaa za miili yao ambao mwishowe unamleta kila mmoja wetu duniani kama mtoto.
Kwa msingi huo hao waliomleta mtoto ulimwenguni iwe ni kwa mipango yao ama kutokana na kukidhi tamaa zao za mwili, basi wana wajibu mkubwa sana wa kuhakisha watoto wanapata haki yao ya msingi ya malezi na matunzo mema.

Mtoto ni nani
Kuna sheria nyingi ambazo kwa kiasi fulani zinajaribu kuelezea mtoto  ni nani. Sheria hizi ni kama Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, Sheria ya Mikataba, Sheria ya Ushahidi, Kanuni ya Adhabu n.k.
Sheria hizi kila moja inajaribu kuainisha mtoto ni nani na akitambuliwa hivyo asifanye nini, lakini mimi kwa ajili ya makala haya, nitamchukulia mtoto kama anavyofafanuliwa na sheria ya mtoto hapa nchini yaani ‘’The Law of the Child No. 21 of 2009. sheria hii katika kifungu cha 4(i) inatamka bayana kwamba, mtoto ni mtu yeyote ambaye yu na miaka 18 kwenda chini, inasema “A person below the age of 18 years shall be known as a child’’.
Ikumbukwe hapa hii sheria haikuainisha huyo mtu awe yuko wapi na anafanya nini kwa hiyo mtu yeyote ambaye ni mwanafunzi, ama mfungwa, ama ni mgonjwa kitandani, ama ni mtaalamu wa jambo flani ama hata ni mke wa mtu, kama hajafikisha umri wa miaka 18 basi huyo ni mtoto.
Sheria ya Umri wa Utu Uzima (yaani the Age of Majority Act) inatamka bayana kwamba mtu akifikisha miaka 18 basi atahesabika kwamba ameingia utu uzima, vilevile sheria inatamka bayana kwamba utu uzima unaanza siku ambayo mtu anaadhimisha siku ya 18 ya kuzaliwa kwake, yaani siku hiyo ndiyo anaachana na utoto.
Siku ya pili yake yaani akiwa na umri wa miaka 18 na siku moja, huyo ni mtu mzima.
Hata hivyo, sheria hii imeaacha baadhi ya mashimo pasipo kuyafukia, kwa mfano haikuelezea kalenda itakayotumika katika kuhesabu miaka ni kalenda ipi, ama hata iwapo siku mtu anapotimiza miaka 18 je kama mtu kama huyo alizaliwa saa 4 asubuhi je inapofika saa 5 asubuhi anakuwa mtu mzima tayari ama bado?
Katika Tanzania kwa mujibu wa utafiti uliyofanywa mtoto ni nguzo muhimu ya taifa kwa sababu zaidi ya asilimia 46 ya wananchi wote wa Tanzania ni watoto. Mtu mwingine anaweza kusema sasa mbona asilimia inayosalia ndio nyingi  yaani karibu 54%.
Ni sawa vilevile kuna asilimia (tena kubwa tu) ya watu ambao akili yao imeisharudia kuwa ya kitoto.
Hawa ndio wenye umri mkubwa sana na labda hawana tena uwezo wa kujitegemea kiakili. Mnamo mwaka 1996 wastani wa watoto katika familia walikuwa ni watoto 6. (Takwimu hii ni ya 1996 kwa hiyo sasa hivi kunaweza kukawepo mabadiliko kidogo hasa ukizingatia kwamba kwa sasa wanajamii wanakazania kupunguza uzao)
Taifa kama taifa limefanya mambo kadhaa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata matunzo na malezi bora, sera na mipango ya taifa iliyochukuliwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya mtoto ni pamoja na ‘huduma za mama na mtoto, huduma za chanjo mbalimbali miladi kadhaa ya maji safi vijijini, kampuni za usafi wa mazingira, uanzishwaji wa vituo vya kulelea watoto wachanga (Yaani feeding and day care centre) uanzishwaji wa shule za awali yaani pre-shools, uanzishwaji wa viwanja vya michezo kwa ajili ya watoto na uanzishwaji wa sera ua elimu ya msingi kwa wote.
Ni bahati mbaya kwamba mipango na mikakati hii haitekelezeki kama inavyopasika si kwa sababu taifa halina uwezo bali kwa sababu ya uzembe na kutokuwajibika kwa wanapokadhiwa madaraka.
Tuchukulie kwa mfano suala la viwanja vya michezo kwa watoto kila mtaa unapaswa kuwa na kiwanja cha michezo kwa watoto wa mtaa huo.
Kila kijiji na kitongoji kinapaswa kuwa na viwanja vya michezo kwa ajili ya watoto wa maeneo hayo.
Lakini kusema ukweli viwanja hivyo havipo na hata viongozi hawajui kwa nini havipo.
Jibu la haraka utakalopewa iwapo utauliza juu ya uwepo wa viwanja, ni mara hakuna fedha, mara mtiskisiko wa uchumi duniani n.k.
Lakini ukweli mbona hii mitikisiko haitikisi misafara mikubwa ya magari wanayoambatana nayo viongozi wetu wanapokuwa katika ziara za mikoa? Kutokuwa na fedha pamoja na mtikisiko wa uchumi duniani, kwangu mimi naona ni kama visingizio ama, ‘scapegoat’’ upande wa viongozi.

Haki za watoto kwa mjibu wa sheria za Tanzania ni zipi?
Sheria ya mpya ya mtoto iliyoanzishwa hivi karibuni yaani The Law of the Child No. 21 of 2009, ambayo imefuta sheria zote zilizokuwa na upungufu kuhusu haki za watoto inaainisha haki mbalimbali ambazo watoto wamepewa kwa mjibu wa sheria.
Kwa mjibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 haki za mtoto zimeainishwa sehemu ya pili(II) ya sheria hiyo na haki hizo  ni pamoja na:
(a)  Haki ya kuishi kwa uhuru bila kubaguliwa.Haki hii imeanishwa katika kifungu namba 5(1) na(2) cha seria ya mtoto ambacho kiafafanua zaidi kuwa mtoto ana haki ya kuishi bila kubaguliwa kwa sababu ya jinsia, tabaka/rangi, umri, dini,lugha, ulemavu,hali ya kiuchumi, mahali anapoishi(mjini au kijijini),kuzaliwa hali ya ukimbizi nk.
(b)  Haki ya kuwa na jina, utaifa na kuwajua wazazi wake na ndugu wengine. Haki hii imeanishwa katika kifungu namba 6 cha sheria ya mtoto na kinasema kuwa mtoto yoyote  ana haki ya kuwa na jina, utaifa na kuwajua wazazi wake na ndugu zake,pia kinazidi kuelezea kuwa niwajibu wa mzazi au mlezi kuhakikisha anasajili kuzaliwa kwa mtoto huyo.  
(c)   Haki ya kuishi na wazazi au walezi wake na .Hii imeainishwa katika kifungu namba 7 cha sheria ya mtoto.Kifunu kinaelezea zaidi kuwa mtu yoyote hapaswi kumnyima mtoto haki ya kukua na kulelewa na wazazi  wake katika mazingira salama ispokuwa kama imeamuliwa na mahakama.
(d)                        Haki ya kupata matunzo na mahitaji ya lazima kutoka kwa wazazi, walezi au mtu yoyote mwenye mamlaka juu ya mtoto huyo. Kifungu cha 8 cha sheria ya mtoto kinatamka bayana kwamba ni jukumu la mzazi, mlezi ama mtu mwingine yeyote mwenye mamlaka juu ya mtoto huyo, kumpa matunzo yanayostahiki hasa: chakula, malazi, mavazi, huduma ya afya na kinga, elimu na malezi, Uhuru (yaani liberty) na haki ya kucheza na kustarehe.
(e)  Haki ya kuishi, utu, kuheshimiwa. Hizi zimeanishwa kaitka kifungu namaba 9 cha sheria ya mtoto na kinampa wajibu mzazi au mlezi wa kumlinda mtoto dhidi ya unyanyasaji,udhalilishaji kwa namna yoyote ile.
(f)    Haki ya kutumia na kufurahia mali za wazazi wake, hii imeainishwa katika kifungu namba 10 cha sheria ya mtoto.
(g)  Haki ya kutoa mawazo na maoni yake, kusikilizwa na kushiriki katika maamuzi mbalimbali.
(h) Haki ya kupewa adhabu inayositahili pale anapokosea. Adhabu hiyo isiwe yenye kuhatarisha afya, kumnyanyasa kisaikolojia,kumdhalilisha utu mtoto na kumnyanyasa.
Pamoja na haki zote alizopewa mtoto kwa mjibu wa sheria, mtoto pia ana wajibu wa kuheshimu wazazi wake na wakubwa zake, kusaidia kazi za nyumbani zisizo na madhara kwake, kutumikia jamii na taifa kulingana na uwezo wake na umri wake, kulinda na kuhifadhi mila chanya na utamduni nk.



Comments