Featured Post

DHANA YA SHERIA YA NDOA NA MAHUSIANO YA FAMILIA


NDOA na mahusiano ya familia ni mambo yanayowahusu watu wengi katika jamii; ndoa ni kiungo kikubwa katika mahusiano ya familia.
Msingi mkubwa wa familia ni ndoa, ambao unatokana na mahusiano ya kimapenzi kati ya mwanaume na mwanamke.

Katika makala haya tunaangalia mahusiano ya kimapenzi kati ya mwanamke na mwanaume yanapoweza kubeba dhana ya ndoa kisheria; jambo la kujiuliza ni je kila mahusiano ya mwanaume na mwanamke ni ndoa?
Katika Tanzania ipo sheria moja ya ndoa ya mwaka 1971 Sheria hii inatambua ndoa zote zilizofungwa kwa kuzingatia taratibu zinazoainishwa kwa sheria mbalimbali kama vile, sheria za kimila, sheria za kidini na sheria za  kiserikali.
Katika jicho la sheria ndoa zote katika makundi yanayotajwa zina hadhi sawa, ufungaji wa ndoa ni tofauti lakini sheria ya ndoa inawatambua wanandoa kuwa wako sawa.
Ndoa ni mahusiano huria kati ya mwanamke na mwanaume pia ni mkataba ama makubaliano huria yanayopelekea wahusika kupata hadhi ya ndoa ambayo inatambulika kisheria.
Sheria ya wanandoa ya mwaka 1971 inayatambua makundi mawili ya ndoa kutokana na makubaliano ya wanandoa. Kundi la kwanza ni ndoa za mke mmoja au zenye makusudio ya kuwa mke mmoja, kama zilivyo ndoa za Kiserikali na za Kikristo.
Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inasisitiza kuwa ndoa kati ya Wakristo iliyofungwa kanisani, haiwezi kugeuzwa kuwa ndoa ya mitala. 
Mwanamke au mwanaume aliyeoa ndoa ya mke mmoja au mume mmoja hataruhusiwa kufungua ndoa nyingine ila tu kama atakuwa mjane au mgane au amepata amri ya mahakama ya kuibatilisha ndoa yake ya awali ama baada ya amri ya Mahakama. Chombo pekee kinachoweza na chenye mamlaka ya kutoa talaka ni mahakama pekee.
Kundi la pili la ndoa ni ndoa za mitala au zinazoweza kuwa za mitala, kama zilivyo ndoa zilizofungwa kiislamu au kimila, ndoa yenye madhumuni ya kuwa na zaidi ya mke mmoja au ya mitala haitaweza kugeuzwa kuwa ya mke mmoja, kwa mfano mwanaume aliyefunga ndoa ya mitala hawezi tena kufunga ndoa ya Kikristo kama hajabatilisha ndoa ya awali.
Nikiwa mwanafunzi wa chuo kikuu wakati huo, niliona mambo kadhaa katika maisha ya chuo; Jambo majawapo ilikuwa ni wanachuo wa jinsia mbili kuishi katika nyumba moja kama mume na mke.
Nilijiuliza ambapo hata wewe unaweza kujiuliza je walikuwa mke na mume? Pia wakati mwingine niliwakuta watu wakisema “…huyu mwanaume kaishi na huyu mwanamke miezi mitatu (3) hawa ni mume na mke  tayari, lazima wagawane mali zao…” Mpendwa msomaji ukweli ni upi? Bila shaka utajua baada ya maelezo yangu mafupi hapa chini.Moja ya ndoa zinazoweza kutambuliwa ni ndoa dhania (presumption of marriage), Kulingana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971,endapo itathibitishwa kwamba mwanaume na mwanamke wenye sifa ya kufunga ndoa, wameishi pamoja mfululizo kwa miaka miwili au zaidi, katika hali ya kupata heshima ya mke na mume, basi watachukuliwa kuwa mume na mke, hata kama hawakujaliwa mtoto.
Jambo la msingi hapa ni kwamba jamii inayozunguka ndoa dhania hiyo iweze kushuhudia. Ikumbukwe kwamba kama ndoa dhania  itavunjika, mahakama inaweza kutoa amri ya kugawana mali kama ilivyoamriwa na mahakama ya Rufaa Tanzania katika Shauri la Hemed S.Tamim dhidi ya Renatha Mashayo, {1994}.
Sheria inayosimamia ndoa Tanzania ni moja tu ambayo ni sheria ya ndoa ya mwaka 1971, hakuna ndoa inayofungwa kinyume cha sheria hii, iwe ya kimila ,kikristo ,kiislamu au Kiserikali. Kiongozi wa dini au kiongozi wa Serikali aliye na kibali cha kufungisha ndoa wote katika sheria wanayo hadhi sawa aidha ndoa zote katika jicho la Sheria ni sawa.

Comments