Featured Post

WARANGI – 2: KABILA LILILOJIVUNIA MNO ASILI YAO

Warangi ni warembo hasa.

Na Innocent Nganyagwa
NAWAKARIBISHENI tena kwenye safu yetu ya mambo ya Asili na Fasili, kama ilivyo ada yetu kila leo ambapo huwa tunapata fursa ya kutembelea makabila yetu mbalimbali na kujifunza asili na fasili yao. Tunajifunza mengi juu ya Uafrika na Utanzania wetu halisi kwa ujumla wake.
Basi kama nilivyowataarifu jana, bado tuko kwenye eneo lile lile la kaskazini magharibi mwa nchi yetu, tunawatembelea ndugu zetu Warangi, ambao tumewapigia hodi baada ya awali kuyatembelea makabila mengine.

Basi kwa faida ya wale ambao hawakubahatika kusoma sehemu ya kwanza ya simulizi hii ya Warangi juma lililopita, nifanye muhtasari mfupi juu ya mambo tuliyoyaona halafu tutaendelea na mengine kwa leo.
Tulisema kuwa ndugu zetu hawa wanapatikana kati ya Babati na Kondoa, lakini kiini chao hasa kikiwa huko Kondoa.
Tumezowea kuwaita Warangi sanjari na lugha yao ya Kirangi, lakini kwa uhakika wao kimatamshi halisi ya lugha yao ni ‘Valaangi’ na wanaongea ‘Kilaangi’.
Ndugu zetu hawa katika safari iliyowafikisha mahali walipo, wamepata kutangamana na makundi kadhaa ya makabila mengine yakiwemo yale ambayo kwa asili yanazurura muda mwingi wa maisha yao.
Lakini wamefaulu kubaki kama walivyo, japo kuna athari ndogo ndogo za lugha yao kimatamshi kama tutakavyoona hapo baadaye.
Baadhi ya makabila hayo wanayopakana nayo tuliyoyataja jana ni pamoja na Wamaasai ambao wanatokea mbari ya Kinailotiki, Wasandawe ambao ni Wakhoisan, Wairaqw, Waburunge, Wasi na Wagorowa ambayo ni makabila ya Kikushi na Wambugwe ambao ni Wabantu.
Lakini, licha ya lugha ya Warangi kuathiriwa kwa mbali na makabila hayo wanayotangamana nayo na yale mengine waliyokutana nayo kwenye kipito chao, ndugu hasa wa Warangi si kwa lugha tu bali hata kwa asili ni Wambugwe.
Jamii za awali za Warangi zinatokea kaskazini na mashariki mwa bara letu la Afrika, walisafiri kupita eneo la bonde la ufa wakaingilia Kenya wakitokea Ethiopia.
Ndiyo maana katika kuingia kwao hapa nchini walifika Babati kwanza, kisha ndiyo wakajisogeza kwenye maeneo mengine hadi wakafika huko Kondoa.
Safari yao haikuwa rahisi sana, kwanza ukichukulia umbali waliotoka na pia mabadiliko ya hali ya hewa ukiwemo ukame, waliokumbana nao kwenye maeneo mbalimbali.
Hali hiyo iliwasababisha wabuni mbinu mbalimbali za kutafuta maji wakati wa kiangazi, walipofanikiwa kupata maji katika eneo husika waliamini mahali hapo panafaa kuishi na walilowea.
Kwa hiyo, wenzetu hawa tunaweza kuwaita kuwa wachimba visima hodari vya kutega maji, maana kwa kawaida walichimba visima virefu na kutumbukiza vyombo ndani yake.
Kisha waliendelea na safari zao na siku kadhaa baadaye walikuja kutazama kama vyombo hivyo vina maji, basi wakivikuta vina maji hufurahi sana na kuamini kuwa sehemu hiyo ina neema na inafaa kuishi.
Kimsingi hawa Warangi walipofika Babati waligawanyika makundi mawili wakati wakielekea mahali walipo hivi sasa.
Mgawanyiko huo ndiyo ulizaa sehemu mojawapo ya Wambugwe, kutokana na kutelekezwa na wenzao mahali hapo baada ya kwenda kuwinda kanga.
Siku moja, vijana hao wa jamii ya Kirangi walikwenda kuwinda kanga kwenye maeneo ya pembezoni na hapo walipofika, yaani Babati. Walikawia kurudi na waliporudi hawakuwakuta wenzao, walioendelea na msafara wao na hivyo wao waliachwa.
Hawakujihangaisha kuwafuata bali waliamua kubakia mahali hapo, ndipo wakajulikana kwa jina la watu walioachwa kwa sababu ya kuwinda kanga.
Kwa lugha ya Kirangi ndege huyo aina ya kanga anayefanana na kuku, huitwa ‘mbuwe’.
Basi wale watu kutoka jamii za Kirangi walioachwa kwa sababu ya kunogewa kuwinda mbuwe, wakajulikana kama Wambugwe tangu wakati huo.
Ndiyo maana ukisikiliza lugha ya Kimbugwe na Kirangi zina maingiliano ya karibu, kulikoni hata yale makabila mengine niliyokutajia wanayotangamana nayo.
Waliowaacha wenzao ndiyo waliokwenda hadi huko Haubi, mahali ambapo wakati wanafika walipakuta pana maji ya kutosha kutokana na vijito vingi vilivyokuwa hapo.
Na kwa kuwa maji ndicho kilichowahangaisha na kuwafanya wazurure tangu awali, kiasi cha kuchimba visima vya kutega, basi kwao hapo waliikuta neema waliyoitaka. Ndiyo sababu inayowafanya Warangi wengi waamini kuwa wanatokea hapo Haubi.
Lakini kwa uhakika kama nilivyokueleza, ni kwamba jamii zao zimetokea mbali sana kwenye eneo la Wahamitiki.
Nitawafafanulia baadaye juu ya Uhamitiki huo uliochanganyika na Ubantu wa hawa Warangi.
Basi hapo walipofika kwenye maji ya kutosha, ndipo walipoweza sasa kuanza shughuli za kilimo cha mahindi na mtama huko kusini magharibi mwa Kondoa.
Eneo hilo la kiini cha nchi ya Irangi lilikuwa na vijito vingi vidogo vidogo, lakini baadaye waligundua kuwa kukiwa na ukame mkali vijito hivyo hukauka.
Lakini hilo halikuwatatiza sana, maana kama vilijaa tena wakati wa misimu mingine basi wakati ule vijito hivyo vilipokauka, walitumia ile mbinu yao ya kale kwa kuchimba mashimo marefu kutafuta maji.
Kiini cha nchi yao kina maeneo ya vijiji mbalimbali kama vile Hurui, Mwaikisabe, Kibaya, Mangoroma, Mafai, Mesanga, Mnenya, Loo na Iyoli.
Tuliona pia kuwa hawa Warangi kutokana na jiografia ya eneo lao ilivyo waliishi kwenye makundi bila kupoteza asili yao, maana kutokana na vilima na miinuko ya uwanda wa nchi hawakuweza kutawanyikia maeneo ya mbali.
Hata baadhi ya makabila majirani nao yalikuwa maeneo ya pembezoni, baada ya mwendo wa umbali kadhaa kupitia kwenye misitu iliyowatenganisha nao.
Kwa mazingira hayo, Warangi ni jamii ya watu wanaopenda kujiweka karibu mno kwenye mambo yao na hujivunia sana asili yao na si rahisi kugubikwa na jamii nyingine.
Lakini namna yao ya kulinda hadhi yao ni kwa upole na si ubabe, maana kati ya makabila yenye sifa ya upole na ukarimu wa kiwango cha juu, hawa ni wamojawapo.
Mathalan, Mrangi akiongea na Mbugwe wanasikilizana na kuelewana, lakini Mrangi hapendelei kuongea Kimbugwe, hata kama anaelewa yanayotamkwa na Wambugwe atajibu kwa Kirangi.
Wenyewe Warangi katika kujivunia mambo yao hupendela sana kusema kuwa, Kimbugwe ukikisikiliza kinavyoongewa ni sawa na kumsikiliza mtoto mdogo wa Kirangi anavyojifunza kuongea.
Lakini hawa ni watu wa asili moja, isingekuwa yale mambo ya kuwinda kanga kama tulivyoona hapo awali, basi pengine wangeendelea kuwa wamoja.
Ndiyo maana haishangazi kuwa maneno yao yana muingiliano mkubwa, kama vile ‘ijova’ yaani jua kwa Kimbugwe lakini kwa Kirangi ni ‘ijuva’. Hicho ni Kirangi kilichotumika zamani, maana kwa sasa unaweza kusikia wenyewe wakiliita jua ‘mwaasu’.
Isikushangaze ndugu Mjadi, maana kama zilivyo lugha nyingine, istilahi za lugha za makabila hubadilika kutokana na sababu mbalimbali yakiwemo mazingira na kuchanganyika kwa jamii kwenye eneo moja.
Mathalan, mwenzenu kabila langu ni Mhehe, ambapo lugha yetu tunayoongea sasa si ile ya asili hasa.
Tuseme ni kama tunaongea Kihehe cha awamu ya tatu au ya nne hivi, ndiyo maana ukimsikiliza Mbena au Mzungwa akiongea lugha yake, utasikia matamshi ya Kihehe chetu cha kale.
Kwa sasa sisi Mungu tunamuita ‘Inguluvi’ lakini kwa Kihehe cha kale ni ‘Kimenya’ sawa na mtu akikupa pole ya kazi kwa Kihehe akisema ‘makasi’ unajibu ‘aale’. Lakini ukikutana na baadhi ya wazee wa Kihehe wakikujibu ‘oongo’ neno ambalo bado linatumiwa na Wabena, isikushangaze.
Naam, huo ndiyo uhondo wa kujitambua na kutambua mambo ya kwenu jinsi yalivyo, na pengine hata kuyajua makabila watani zako.
Usije siku ukamtania mtu ambaye pengine huna utani naye kwa asili, (nazungumzia utani wa kijadi), itakusababishia matatizo!
Basi hawa Warangi kwenye kiini cha nchi yao ya Irangi, hata kuoana awali ilikuwa baina ya jamii zao wenyewe.
Na kama ilitokea wakaoana na mtu wa jamii nyingine za pembezoni, basi yule mtu wa jamii ya pembezoni ndiye atakayegubikwa na silika zao na sio wao kubikwa na silika za ugeni.
Na hata sasa, si tu watakuvutia kwa namna hiyo, lakini bila kutia chumvi tuseme wazi kuwa ndugu zetu hawa wana maumbile ya kuvutia sana.
Tena wana rangi mchanganyiko sana, kama nafsi yako haina ustahimilivu unapokutana na mabibie wambuji (warembo) kwa asili, basi jaribu kukutana na mabibie wa Kirangi na utanielezea jinsi utakavyogubikwa na ulimbwende wao.
Tukizidi kusonga mbele na mambo ya Warangi, ni kwamba ndugu zetu hawa kwa asili ni Wabantu wa Kihamitiki.
Ndiyo maana licha ya kuzungukwa na yale makabila mengine, ambayo mengine walikutana nayo kwenye kipito chao, hawakubadilika.
Nimeyataja hapo awali kwenye simulizi ya leo, Wamaasai, Wabarbaig (Wanailotiki), Wasandawe (Wakhoisan), Wairaqw, Waburunge, Wagorowa na Wasi (Wakushi).
Katika bara hili la Afrika, Wahamitiki wengi wanatokea upande ambao jamii za awali za Warangi zinakotoka, yaani kaskazini.
Kuhusiana na mashariki, eneo hilo ni kipito cha jamii nyingi za upande wa kaskazini zilizokuja huku mashariki na kusini.
Hata baadhi ya Wakushi kama vile Warimi (Wanyaturu), walipita upande huo pia.
Nimekuwa na kawaida ya kuwafahamisha mara kwa mara maana ya mbari, ambazo ndizo huzaa makabila. Mbari ni fungu kubwa la jamii ambalo huzalisha makabila mengi, makabila yanayotokana na mbari moja huwa na maingiliano mno ya mambo yao ikiwemo lugha.
Afrika kuna takriban mbari zipatazo tano, Wabantu (ambao kimsingi walitoka kaskazini kabla ya kwenda kusini zaidi na kuja mashariki na kati kati). Kisha kuna Wanailotiki, Wahamitiki, Wakushi na Wakhoisan, kwa hiyo sehemu kubwa ya makabila yetu barani hapa yanatokana na mbari hizo.
Japokuwa pia kuna jamii zilizochanganyika kutoka mbari tofauti, hivyo kuzaa aina ya watu mchanganyiko sana.
Mathalan, Wanyaturu katika kipito chao kwenda Singida walichanganyika na Wanyantuzu (Wabantu).
Kwa hiyo, Mjadi usishangae ukikutana na Mnyaturu anayefanana mno na Mhabeshi, huyo damu yake imeelemea zaidi upande wa Ukushi.
Kuna Wanyaturu weusi wanene (wamechanganya Ubantu na Ukushi, kutokana na kuzaliana na Wanyantuzu).
Pia kuna weupe kama Waarabu wa sasa, (kutokana na maingiliano na Waarabu wa kale ambao nao wamo ndani ya Uhamitiki).
Naam, usichanganyikiwe sana, nilikuwa nakumegea kidogo kina cha ujadi maana ni kirefu na kuna mambo mengi.
Ila huwa nawazamisha kina hicho mara chache kutokana na fursa yenyewe, tukizama moja kwa moja naamini kuna baadhi yenu mtapoteza mwelekeo wa fikra za ujadi.
Lakini ni changamoto nzuri ya utopevu wa kijadi, basi turudi kwenye mambo ya ndugu zetu Warangi.
Hawa ndugu zetu licha ya kujitahidi kujilinda dhidi ya kugubikwa na makabila wayanayotangamana nao, lakini ukisikiliza lugha yao ina baadhi ya athari za makabila hayo.
Si katika ule msingi wa muundo, bali jinsi Kirangi kinavyotamkwa kinasababisha aina nne za utamkaji wa lugha hiyo.
Hayo mafungu manne yanatokana na maeneo yao, mathalan, matamshi ya Kirangi cha Kondoa (ambako ni magharibi mwa nchi ya Irangi) na Haubi (mashariki), muundo wake unafanana kwa karibu sana.
Kwa upande wa pili, matamshi ya Kirangi cha Kolo (kaskazini magharibi) na Mondo (kusini mashariki), nacho kinakaribiana kwenye muundo wa matamshi.
Maneno ni yale yale, lakini tofauti ndogo ndogo ni za namna ya utamkaji, kuna wanaovuta silabi za kimatamshi na wanaokata silabi hizo.
Hiyo ni moja ya athari za mtangamano na makabila mengine, kutokana na kuyaambukiza makabila hayo lugha yao.
Kuna makabila yanaongea Kirangi kama vile ni lugha yao, mojawapo ni Waburunge au ndugu zetu Wasi (Waalagwa). Lakini hivyo sivyo ilivyo, japo wanaweza kuwa na muingiliano na makabila hayo, lakini nao ni kabila linalojitegemea.
Hawa ndugu zetu Warangi si wengi sana kwa idadi japo pia si wachache. Lakini kinachokufanya uwatambue kuwa wapo, ni ile hali ya kujivunia asili yao. Maana katika sifa yao mojawapo ni kukuza na kupenda sana kuongea lugha yao.
Mrangi huzoeshwa kumudu kuongea kikwao tangu akiwa mdogo, kwa wale ambao wazazi wao wanazingatia mambo ya kabila lao.
Hiyo huwajengea hulka ya kujivunia asili yao, ndiyo maana ukibahatika kufika kwenye maeneo ya kiini cha nchi yao ya Irangi kule Kondoa kwenye maeneo ya Bereko, Kikilo, Kisese, Masange, Mnenia, Chandama, Chemba, Goima, Mrijo, Kolo, Soera, Changaa, Thawi, Kingale, Suruke na Dalai. Au maeneo ya Jangalo, Mondo, Paranga, Bumbuta, Busi, Haubi, Kalamba, Kwadelo na Pahi unaweza kushangazwa na baadhi ya mambo yao.
Huko tofauti na kwingineko, hata sehemu wanazofanya biashara zao za mazao, maana wao kwa sasa kwa sehemu kubwa wao ni wakulima, hutumia sana lugha yao ya Kirangi.
Hawa ndugu zetu hata barua zao hupenda kuzianza kwa salamu za kikwao, hata maandishi ya mapambo kwenye vyombo vya usafiri mengi huyaandika kwa Kirangi.
Tukutane kesho kwa simulizi ya kabila jingine.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Machi 21, 2009.

Comments