Featured Post

WANYAKYUSA-8: WALIPATA JINA LAO KABALE-MWAKALELI


Na Innocent Nganyagwa
NDUGU zangu, nawakaribisha kwa mara nyingine kwenye utopevu wetu wa ujadi, ambapo leo tunamaliza ziara yetu kwa Wajadi wenzetu wa Kinyakyusa.
Lakini licha ya kukamilisha ziara yetu ya kijadi kwao haimaanishi kuwa tumemaliza kuchambua kila kitu kinachowahusu.
Maana kama ambavyo siku zote huwa naainisha, mambo ya makabila ni mengi kihistoria na yana mchanganyiko mwingi wa jadi mbalimbali.

Kwa hiyo si rahisi kusimulia kila kitu, hasa kutokana na muundo na mfumo wa makabila yenyewe kwa kuzingatia historia yake, mafungu yanayounda kabila husika, mbari ambayo kabila linatokea, lilipo sasa na mabadiliko yaliyotokea ndani ya kabila husika kutokana na kuhama kwenye chanzo chake cha asili.
Katika hayo niliyoyataja, Wanyakyusa nao wana mambo yanayowahusu ambayo ni ya kina na ya kihistoria yasiyofahamika vyema hata na baadhi ya Wajadi wa kabila hilo.
Lakini yana mashiko na uthibitisho mwingi wa kutosha, kama ambavyo tumefafanua kwa takriban awamu kumi tulizowatembelea.
Basi kwa utaratibu wetu tuliojiwekea ambao tunautumia sasa, tutazame japo kwa ufupi makala yaliyopita kabla ya kuendelea na uchambuzi wa leo niliowatayarishia.
Katika kufafanua jambo mojawapo ambalo halikueleweka, niliwaeleza kwa kina kuhusu kigoli kujizoeza majukumu ya nyumba yake kwa mumewe mtarajiwa.
Utata ulitokana na maelezo yaliyohusu kujizoeza kujamiiana, japo tulisema si kwa ukamilifu, yaani ni aina fulani ya mchezo. Kuna maelezo ya kina ya jambo hilo, lakini kwenye staha ya ujadi wetu tulielezea kwa namna ya kulinda heshima ya ujadi wa ukurasa huu.
Lakini tuliona kuwa mume mtarajiwa aliyeshindwa kustahimili michezo kiasi cha kupitiliza, huwa amemvusha mchumba wake huyo kutoka daraja la uchumba hadi kuwa mke kamili kabla ya muda husika haujawadia.
Ikitokea hivyo basi alipaswa kumalizia sehemu ya deni la mahari anayodaiwa kwa kuharakisha kwake mambo, lakini athari itakayompata ni ugumu wa kujua kama mchumbawe huyo amejizuia kujamiiana na mtu mwingine zaidi yake. Kwa kuwa ameshamuanzisha na hataweza kuona ishara, nadhani naeleweka nikisema hivyo.
Lakini hayo yote yanatokana na kabila hilo kuwa na muelemeo wa ukiritimba mwingi wa kiumeni, kama tulivyoona ile hulka ya wanaume kujikusanyia wake wengi na kusababisha uhaba wa wake kwa vijana waliotaka kuoa.
Ningependa uelewe kuwa, kutokana na maeneo husika na fungu la kijamii husika ndani ya kabila hilo, ndiyo maana utaona kunakuwa na mabadiliko kuhusiana na baadhi ya mambo yao kama lilivyo suala hili la ndoa na mahusiano ya kijinsia.
Kuna jambo jingine nitawafahamisha kwenye ujadi wa leo, linalohusu mabadiliko yao ya kimafungu na kimaeneo.
Kwa hiyo, licha ya ule uhuru wa kucheza na mchumba wake lakini binti hukaguliwa kuhakikisha kuwa ameweza kujitunza na kustahimili kulinda ukomo.
Jukumu hilo la ukaguzi lilitekelezwa na shangazi wa mchumba wake, au mama yake mzazi. Nafasi ya baba katika jambo hilo ni kupewa taarifa tu, hasa ukomo ukikiukwa maana akishafahamu hali hiyo hulazimika kuamuru mahari iliyosalia ilipwe kama tulivyoeleza awali.
Ieleweke kuwa ukomo ukivukwa si kwamba hali hiyo ilichukuliwa kwa urahisi tu, kulikuwa na adhabu husika kwa binti kama aliridhia mwenyewe matakwa ya mchumba wake katika kuvushana ukomo.
Lakini kama yule mchumba ndiye aliyeshinikiza basi naye alihusika kupata sehemu ya adhabu hiyo, mojawapo ikiwa kuharakishwa kumalizia mahari iliyosalia.
Lakini kwa mabinti waliostahimili na kuvuka kikwazo cha kukiuka ukomo wa kucheza, wakithibitika kuwa hivyo husifiwa sana na hupelekwa kwa mume kwa vishindo vya nyimbo na sifa nyingi kutokana na kuweza kujihimili.
Kutokana na thamani ya binti wa aina hii mahari yake huwa na vitu vya nyongeza, tofauti na yule ambaye hakufaulu kuhimili kuvuka ukomo.
Mjadi, kutokana na maelezo hayo utaona kuwa kuna baadhi ya mambo kama hilo la mahusiano, yanabadilika sana kimaelezo mara kwa mara. Lakini ukweli ni kuwa kabila lenyewe lina mabadiliko mengi, kutokana na mchanganyiko wa baadhi ya mambo yake kutoka eneo moja hadi jingine. Hata kule kubadilika jina kutoka Wankonde na kuwa Wanyakyusa, ni sehemu ya mabadiliko hayo.
Makala iliyopita tulichambua kwa kifupi zaidi, ili tupate nafasi ya kutosha kuelezea baadhi ya mambo ambayo mlikuwa na maswali nayo tangu tulipoanza uchambuzi wa kabila hili, ambayo sikuwa nimeyaeleza.
Sasa tujielekeze kwenye ujadi niliowatayarishia leo, mtakumbuka tulisema kuwa nchi ya Unyakyusa inaanzia huko Konde-Karonga kwenye uwanda wa milima ya Livingstone nchini Malawi hadi Kusini mwa nchi yetu huko mkoani Mbeya.
Pia tuliona jinsi ukiritimba wa kiume ulivyogubika kabila hilo, lakini hali hiyo ikishindwa kufuta kabisa ile alama ya kikeni kutokana na kuchukua majina ya kikeni.
Nilipoeleza awali juu ya Malkia Nyanseba mwenye asili ya Kinubi, kuna baadhi yenu hamkunielewa. Kwa kuwa hawa Wanyakyusa ni Wabantu, lakini pia nilifafanua kuwa kwa asili Wabantu walitoka Kaskazini wakaja hadi Kusini kabisa kabla ya wengine kurudi tena Katikati.
Hapo nazungumzia Bara la Afrika, pia kuna masalia yao kwenye vipito takriban vitatu kutoka Kaskazini kuja Kusini, viwili kati ya vipito hivyo vikiwa Afrika Kati na Kaskazini-Mashariki kwenye eneo la Unubini.
Kwa hiyo katika yale mabadiliko yao ya mara kwa mara, baadhi ya tabia zao zina athari za Kinubi kwa damu ya Malkia Nyanseba huku nyingine zikiwa na athari za Kibantu zaidi na nyingine zipo kati kwa kati.
Tabia nyingine ni kutokana na athari za mgawanyiko kutoka Konde hadi Unyakyusani, na kama mtakumbuka tulifafanua kwa nini baadhi ya vijiji vya Upogoroni vina majina yanayoshabihiana na ya Unyakyusani; kwamba kuna Wankonde waliopitiliza kutokana na kukimbia mapigano ya wababe wa Kingoni, ambao ni tawi tanzu la Wazulu kutoka kusini.
Hawa Wangoni (kwa asili hasa wanaitwa Wanguni), walidhamiria kupiga jamii zote kutoka Kusini walikoingilia hadi maeneo ya Mashariki (Uluguruni).
Lakini walisimamishwa na mbabe wa kivita wa Wahehe, Mtwa Mkwavinyika (Mkwava), aliyewazungukia kutoka Kalenga na kuanza kuwarudisha nyuma kutoka Tanangozi.
Vita havikuwa na mshindi zaidi ya Mkwawa na jeshi lake kuishia mpakani mwa Iringa na Ruvuma, na baada ya hapo utani baina ya makabila haya ulianza.
Pia msisahau zile fungamano za Wanyakyusa na Wakinga, huku hao Wakinga wakiwa fungu tanzu lililotokana na Wahehe.
Unaweza kujiuliza, kwa nini nakueleza yote hayo? Nataka kukukumbusha ili nikueleze sasa chanzo hasa cha kuitwa Wanyakyusa, kutoka kule Konde-Karonga Malawi walikokuwa Wangonde au Wankonde.
Soma kwa makini sehemu inayofuata, ili akili yako itopee vizuri kwenye ujadi ninaotaka kukufahamisha.
Nimewahi kueleza sana kuhusu Wabantu mara kadhaa, Bantu ni moja kati ya mbari kuu tano za Waafrika. Ambapo kila mbari huzalisha makabila kadhaa, pia kuna makabila yanayotokana na mchanganyiko wa mbari.
Makabila mawili au zaidi yanayotokana na mbari moja, hufanana kwa baadhi ya mambo yake hata kama yako maeneo mbalimbali. Kwa Kibantu, neno ‘Banya’ linamaanisha ‘wanaotokana na’ au ‘wanaotoka kwa’.
Mathalan, Banyamwezi (ambayo kwa Kiswahili hutamkwa Wanyamwezi) ni ‘wanaotoka kwa’ sio kwenye mwezi, ila inamaanisha upande wa magharibi.
Kwa jiografia ya kijadi Wajadi wa maeneo ya pwani walifahamu fika kuwa, Wanyamwezi wanatoka upande wa Magharibi mkoani Tabora na upande huo ndiko mwezi mpya (mwandamo) hutokea.
Kalenda ya kijadi inahesabu miezi kwa kufuata kutokea na kupotea kwa mwezi, unaweza kushangaa na kuhisi mbona inafanana na Kalenda ya Kiislamu?
Hujakosea, sehemu kubwa ya makabila yenye Ukushi, Uhamitiki na Unailotiki, yanatokea Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali ambako ustaarabu ulianzia na kuna kiini kikubwa cha imani ya Kiislamu.
Tuliona jinsi Warangi walivyotoka Mashariki ya Mbali, eneo la Uhamitikini na wao ni Wahamitiki.
Sasa turudi kwa Wanyakysusa maana katika kukufafanulia nikikuzamisha sana kwenye kina cha utopevu wa ufafanuzi wa kijadi, nachelea nitakuchanganya.
Jina la Wanyakyusa kwa kabila hilo walilipata kwa nyanya (Bibi Mzee), kwa ule utaratibu wao wa kuchukua majina kikeni.
Kyusa ni jina la huyo bibi ambaye aliishi Kabale kwenye msitu wa tambiko kwenye Kijiji cha Suma, njia ya kuelekea mji mdogo wa Mwakaleli.
Kwa hiyo kusema Wanyakyusa (Banyakyusa) maana ni wale watokanao na huyo Bibi Kyusa, japo hiyo Kyusa pia ina maana yake pia.
Kwa hiyo kuna baadhi ya Wanyakyusa ambao hujitambua kuwa wanatoka eneo hilo, japo kwa uhakika Bibi Kyusa anatokana na kizazi cha waliokuja kutoa Konde-Karonga.
Kama tulivyoona awali ndugu zetu hawa ni wajasiriamali wa kijadi. Maana zamani kabisa kwenye miaka ya sitini kurudi nyuma, vijana wengi wa kabila hilo waliokosa uwezo wa kulipa mahari ya kutosha, walienda kutafuta maisha kwanza huko Zimbabwe Kusini na Kaskazini kwa kufanya kazi ya vibarua kwenye migodi.
Lakini endapo hawakufanikiwa waliwarubuni wazazi wa mabinti waliotaka kuwaoa kwa kutoa pesa kidogo na ng’ombe mmoja, kisha walifanya utekaji wa binti anayetakiwa.
Yaani mposaji wa ile mahari kidogo huwatuma vijana wenzake kumvizia binti husika mathalan akienda kuteka maji, kisha humnyakua na kumpeleka kwa aliyewatuma.
Kinachofuata ni kutuma ujumbe wa mshenga kwa wazazi, kuwataarifu alipo binti yao ili wasihangaike kumtafuta.
Hali hii huonesha taswira tofauti, binti anaweza kuvunga kutokukubaliana na hali hiyo au hata wakwe nao kuonesha kutopenda hali hiyo.
Lakini kwa familia ambazo mabinti hawakuposwa, ilionekana kama nafuu ya kuondoa mkosi kwa ahueni ya kupata mtu aliyemchukua.
Lakini lazima kijana husika atozwe faini, hili linaakisi mabadiliko mengine ya hulka tofauti za kabila hili.
Ndoa za kusombana tuliziona tulipotembelea baadhi ya makabila yaliyopita eneo la Afrika Kaskazini Mashariki wakati yanakuja hapa nchini, au ndani yake yana mchanganyiko wa jamii zilizotoka eneo hilo.
Lakini licha ya athari za mbari nyingine kwenye kabila hilo, bado wana sehemu kubwa ya mambo ya Kibantu hasa kwa ngoma zao kama ile ya Ipenenga na Ing’oma.
Ipenenga huchezwa na watu wazima hasa wale ‘Mafumu’ wasaidizi wa Chifu ambao ni wajuzi wa uganga. Ngoma hii huchezwa pamoja na wake zao siku za sikukuu kubwa, au kumalizia arobaini ya msiba wa mtu mkubwa au Chifu aliyefariki.
Na ile ing’oma huchezwa zaidi na vijana wakitumia fimbo na vibuyu, hii huchezwa wakati wowote haina muda mahsusi. Kama nilivyochelea awali kuwa hata tukiendelea kwa awamu ngapi hatuwezi kumaliza mambo yao ndugu zetu hawa.
Basi tuishie hapa kwa leo, nawashukuru Wajadi wenzangu wa Kinyakyusa tulioshirikiana vyema muda wote nilipokuwa nachambua mambo yao.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Septemba 12, 2009.

Comments