Featured Post

WANYAKYUSA-6: MABADILIKO TANGU KONDE HADI MBEYA


Na Innocent Nganyagwa
KARIBUNI kwa mara nyingine tena ndugu zangu, katika utopevu wetu wa kijadi kupitia safu hii. Leo tunapiga hodi kwa mara ya sita katika ziara ya kuwatembelea ndugu zetu Wanyakyusa.
Basi kwa tuendelee na mambo ya ndugu zetu Wanyakyusa kwa kuanzia na muhtasari wa tuliyoyaona jana.

Katika ndoa za umri mdogo za mabinti wa kabila hilo, tulieleza jinsi binti alivyoanza kujizoesha baadhi ya majukumu ya nyumba yake tarajiwa.
Kufanya usafi wa nyumba, kupika, kuchota maji na kusafisha zizi la ng’ombe ni baadhi ya majukumu aliyoyatekeleza kwa mume mtarajiwa.
Pia kuna lile la kujizoesha kujamiiana japo si kwa ukamilifu, hili lilizua maoni kutoka kwa baadhi ya Wajadi wa Kinyakyusa waliowasiliana nami, nitafafanua zaidi hapo baadaye.
Lakini kwa mume mtarajiwa aliyepitiliza kwenye tendo hilo, hataweza kuwa na uthibitisho kama mchumba wake huyo hajawahi kujamiiana na mwanaume mwingine zaidi yake kabla ya ndoa.
Hilo likitokea kwa ridhaa bila yule binti kulazimishwa, halizui tatizo kubwa.
Lakini kwa kipindi hicho ieleweke kuwa binti husika huangaliwa kwa ukaribu na wazazi wake, kiasi kwamba hukaguliwa kubaini kama hajavuka ukomo wa mchezo na mume mtarajiwa.
Ukomo ukivukwa basi kwa amri ya baba yule aliyemvusha ukomo hutakiwa kumalizia kulipa ng’ombe wa mahari na kumchukua kigoli huyo, kwa kuwa amemharakisha yeye mwenyewe kuwa mke kamili kabla ya wakati.
Huo ni wakati huyo binti akiwa kigoli kuelekea kuvunja ungo, hebu sasa nifafanue kama nilivyowaahidi awali.
Mwanzo kabisa wakati tulipoanza kuwatembelea ndugu zetu hawa, nilifafanua juu ya nasaba na muingiliano wa Kinubi ndani ya Ubantu wao.
Tulielezea juu ya Malkia Nyanseba, japo kuna baadhi walitatanishwa na mchanganyiko wa mbari.
Nililazimika kurudia tena ufafanuzi wa maeneo ya mbari na kuchanganyika kwake, pia kufafanua kuwa kinachodhaniwa kila mara kuwa Wabantu kwao ni Kusini tu mwa Afrika si kweli.
Bali historia zinaonyesha kuwa walitoka katikati ya Afrika ya Kati na Magharibi, baadaye wakaja kusini kabisa na kusogea kutoka Kusini kuja Mashariki.
Ndiyo maana ukifika kuanzia maeneo ya Congo ya Brazaville, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Cameroon, kuna idadi kubwa ya Wabantu.
Kama unaifahamu vyema ramani ya bara hili na historia ya kuzurula kwa makundi ya kijamii kuingilia Kaskazini Mashariki mwa Afrika, kisha kuelekea Kati na kutoka Kati kwenda Kaskazini hadi Mashariki pia kutoka Magharibi kupitia Kati, ndiko kulikosababisha muingiliano wa mbari za Kibantu, Kinailotiki, Kikushi na Kihamitiki.
Kwa hiyo kwa Wabantu hawa wa Kinyakyusa kutokea kule Konde-Karonga-Malawi, walikuwa na mashiko ya Kibantu yaliyoingiliana na nasaba za Unubi wa Nyanseba kutoka eneo la Kaskazini Mashariki kuelekea katikati.
Hata baadhi ya mambo yao tuliyoyaeleza kwenye sehemu zilizopita za ziara yetu kwao, kwa kawaida hayatendwi na Wabantu wengi baada ya kufika Kusini.
Mojawapo ni hilo la kujizoesha kujamiiana japo si kikamilifu, ambalo ni mashiko ya Kinailotiki zaidi kuliko Ubantu. Lakini pia kutoka kule Konde hadi Mbeya, kuna mengi yaliyobadilika taratibu na kukumbatia mashiko ya Kibantu zaidi.
Nitaendelea na ufafanuzi huu baadaye kidogo lakini nikikukumbusha tena kuhusu tuliyoyaona juma lililopita, niliwafafanulia kuhusu historia zinazoonyesha kuwa Wanyakyusa ni mabaki ya Wangoni na Wapogoro waliopigwa kutoka Kusini hadi milima ya Upogoroni.
Kutoka hapo milima Upogoroni wakarudi kinyumenyume hadi milima ya Ukinga, hadi wakaishia mahali walipo hivi sasa.
Kuna majina mengi ya vijiji vya Upogoroni yanayofanana na majina yaliyoko Unyakyusani, nilifafanua msingi wa jambo hilo.
Kwamba kutoka Konde-Karonga hadi Unyakyusani ya sasa ni kutoka Kusini zaidi, hadi kuja Mashariki japo kwa kuishia njiani.
Kusini (Malawi) kwenye uwanda wa safu ya milima Livingstone, ni mapito ya makabila mengi yaliyotokea Kusini kabisa kuingia hapa nchini.
Wangoni (Wanguni) ni mojawapo ya makabila hayo, Waluguru pia walipita njia hiyo wakati jamii zao za awali zilizotokea Angola zilipoingia hapa nchini.
Mapigano yaliyozikumba baadhi ya jamii za awali za Wakonde ambazo ni jamii tanzu za awali za Wanyakyusa walipokuwa Karonga, yaliwakimbiza hata kupitiliza eneo waliloko sasa.
Majina ya Kinyakyusa yaliyopo Upogoroni yalianzia tangu Konde-Karonga na yapo Mbeya hivi sasa, kama mtakumbuka tulieleza kuwa hata wakati wa ukoloni hali ya kurandana kwa jamii mbili zilizogawanyika kutokana na jamii moja kuliwachanganya hata wakoloni.
Wajerumani waliokuwa upande wa Mbeya mpakani na Konde, walitaka kupaita Konde kutokana na lugha na baadhi ya mambo kufanana mno na upande wa pili (Malawi) uliokuwa chini ya Waingereza.
Kwa hiyo makala iliyopita tulimalizia kwa kutoa tahadhari, juu ya fungamano tofauti baina ya makabila tuliyoyatembelea muda mrefu upande wa Kaskazini na haya ya Kusini.
Nilifafanua pia kuhusu uwiano wa Unyakyusa na milima ya Ukinga, maana mwanzoni kwenye ziara yetu kwa Wanyakyusa tulifafanua kwa kina ushirikiano wa makabila hayo.
Na kuhusu fungamano tofauti za makabila ya Kusini na ya Kaskazini, niliwatahadharisha mshangao utakaowakumba tutakapowafikia Wasangu kabila litakalofuatia baada ya uchambuzi wa hawa Wanyakyusa.
Wana fungamano fulani na Wahehe, kiasi kwamba kuna koo za Kihehe zenye mashina yake Usanguni.
Kwa hiyo haishangazi kukuta Wasangu wanaoongea Kihehe kama Wahehe, kutokana na kuwa matawi ya jamii moja.

Niliwakumbusha tena kuwa Wahehe ni kabila linalotokana na mchanganyiko wa Wangazija, Wahabeshi na Wabantu.
Na baadaye kabila hilo nalo lilizalisha makabila ya Wakinga, Wabena, Wabena-Manga na sehemu ya Wagogo.
Basi tukiendelea, mtakumbuka mwanzoni kabisa tulipoanza ziara yetu kwa hawa Wanyakyusa niliwatajia baadhi ya mambo yaliyobainisha yaliyofuata kwenye sehemu za mbele za uchambuzi huu.
Kwanza hawa waliitwa Wasokile, Wangonde au Wankonde na wanapatikana kuanzia Kaskazini mwa Malawi hadi Kusini mwa nchi yetu, eneo lote hilo ndilo nchi ya Unyakyusa.
Lugha yao ni lugha tanzu ya Kibantu, yaani ina mashiko na lugha nyingine ambazo kwa asili si za Kibantu.
Matamshi yao ukiyasikiliza hayaweki msisitizo wa mvunjiko wa silabi, kama sehemu kubwa ya Kibantu kilivyo. Hata baadhi ya misamiati yake si kama ya lugha nyingi za Kibantu, hata za Wabantu wengine wanaowiana nao.
Hadi kwenye miaka ya mwanzoni mwa 1990 walikuwa takriban milioni moja na ushei hivi, huku asilimia 75 ya idadi hiyo wakiwa upande wa nchi yetu ya Tanzania.
Asilimia kama 25, ndiyo waliosalia upande wa Malawi lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka kutokana na kupita takriban zaidi ya miongo miwili na nusu (miaka 27).
Na kupita Mto Songwe kwenye iliyoitwa Nyasaland zamani (Malawi kwa sasa), ndiko walikobakia wakiitwa Wankonde na upande wa pili ndiko wanakoitwa Wanyakyusa.
Nyasaland ilikuwa chini ya Uingereza na upande huu ulikuwa chini ya Wajerumani, ambao walitumia sana kupaita Unyakyusani kuwa Konde kutokana na ufanano wa ukaribu na Wankonde.
Ambacho hawakukijua ni kwamba, hiyo ni jamii moja iliyotenganishwa na mipaka ya kikoloni na kule kuhama.
Wengi wenu hutatizwa sana na mipaka ya kimikoa na nchi katika kutopea kina cha ujadi.
Ndiyo maana mara nyingi huwa nawatahadharisha kuwa, mkitaka kufaidi kina cha uhondo wa ujadi msikubali kufungwa na fikra za maamuzi ya watu wa kuja waliosababisha fikra za sasa.
Kwamba kabila fulani ni la mkoa fulani kweli yapo baadhi ya makabila ya aina hiyo, lakini kwa sehemu kubwa kuna makabila ambayo si ya mkoa mmoja.
Unaweza kuyakuta makabila hayo kwenye uwanda mzima, au hata ndani ya zaidi ya mkoa mmoja. Mtakumbuka tulipowatembelea Wakimbu, tuliona kuwa wanapatikana Iringa, Mbeya, Tabora, Katavi, Songwe, Rukwa na Singida.
Sasa sijui ukitaka kulipanga kabila hilo kwenye mkoa mmoja, utasema wao ni watu wa wapi?
Nchi ya Ukimbu inamega maeneo ya mikoa hiyo saba, kwa hiyo usishangae ukikutana na Wakimbu watano tofauti na kila utakayemuuliza kwao ni wapi akakutajia mkoa tofauti na wenzake katika ile saba.
Kwa hiyo Wajerumani hawakuweza kutofautisha hadi kwenye miaka ya 1930, kwamba huku upande wa pili kwa sasa sio Konde ni Unyakyusani.
Ufafanuzi mwingine Mjadi ni kuwa, hawa ndugu zetu kama tulivyoona kuwa wana ndoa za mitala ya wake wengi.
Lakini kiwango chao cha mahari ni cha kutosha hasa, ndiyo maana kwenye kukiuka ukomo wa ustahimilivu nilisema kuwa mkiukaji hutakiwa kumalizia kulipa mahari na kumchukua binti aliyemvusha daraja la mke kabla ya muda kubaliwa.
Unaweza kuona hilo kutokana na kiwango chenyewe cha mahari, pia tulisema awali kuwa utumwa ulisalia kule Konde Karonga.
Mkutano wa kiji katika eneo la Konde nchini Malawi, taswira inayoonyesha nyumba ambazo zinapatikana pia Unyakyusani.

Huo ulikuwa utumwa kwa jamii ile uliofanywa na jamii za wageni, lakini taratibu walivyosogea Unyakyusani mambo hayo yaliisha taratibu japo kulikuwa na sehemu ya utumwa wa ndani.
Jambo lingine ambao usipolifahamu litakutatanisha, kuna utopevu mkubwa wa kiimani za Kigeni mkoani kwao hivi sasa.
Lakini ukweli ni kama tulivyoeleza sehemu mbili zilizopita, mambo yao ya kijadi ya kiimani yana mashiko makubwa.
Na imani hizo ni tangu mababu na mababu zao, japo kuna baadhi ya mambo hayawekwi wazi zaidi. Mabadiliko mengine ni urithi wa uchifu; kulikuwa na mifumo miwili: wa awali ni tangu Konde wa urithi wa moja kwa moja kwa watoto.
Ambapo kwenye zile himaya zao ndogondogo za kichifu, chifu aliweza kurithiwa na watoto wake wawili wa kiume wa kwanza kuzaliwa na mke mkubwa na anayefuatia.
Na urithi huu si lazima chifu afariki bali akishafikia uzee kiasi cha kutoweza kutimiza majukumu ipasavyo, huku watoto wake hao wakiwa wameshafika umri wa kuweza kukabili majukumu hayo.
Chifu huagwa kwa sherehe, ambayo pia huitumia kugawanya eneo la himaya yake kwa wanawe wawili na kuzalisha himaya mbili.
Hilo ndilo lililosababisha utitiri wa himaya ndogo ndogo zisizo na uchifu mkuu, maana kama hao wanawe wawili wakishakuwa machifu na wakijiuzulu nao watatumia mfumo huo.
Kwa mfumo huo kama ililazimika, himaya za zamani hasa za machifu waliojiuzulu, huzipisha himaya mpya za warithi kwenye sehemu kubwa ya eneo hilo.
Mfumo huo ni tofauti na ule ambapo wale ‘Mafumu’ (wasaidizi wa Chifu) huwa na sauti zaidi, kama tulivyoona sehemu zilizopita.
Kuna mabadiliko mengi ya kimsingi kutoka Konde hadi Unyakyusani, japo pia kuna mashiko ya zamani yanayodumu hadi sasa.
Nikisimulia baadhi ya mambo hayo yaliyotendeka Konde yanaweza kusababisha taharuki, lakini kwa kuwa huwa tunachuja basi tunayaweka kando na hatuyaaniki hapa ukurasani.
Leo tulikuwa na ufafanuzi zaidi uliochanganyika na muendelezo wa ujadi wa Kinyakyusa.
Basi tukomee hapa na tutaendelea tena kesho.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Agosti 29, 2009.

Comments