Featured Post

WANYAKYUSA-4: CHATU ALITUMIKA KUFANYA USHIRIKINA

Hili ni Ziwa Ngozi mkoani Mbeya ambalo inadaiwa lilikuwa likihama kimiujiza.


Na Innocent Nganyagwa
WAJADI wenzangu, karibuni tujumuike pamoja kwenye utopevu wetu wa kijadi kupitia safu hii. Leo tunaendelea na ziara yetu kwa ndugu zetu Wanyakyusa.
Rika ni kigezo muhimu sana, kwa watoto wa kiume wa Kinyakyusa. Kwa rika hilo walilazimika kufuata utaratibu wa kulima mashamba ya baba zao, hadi wafikie umri wa kuoa. Hilo liliambatana na kujifunza majukumu ya maisha watakapoanza kujitegemea, kwa wakati wote huo walitegemea mlo nyumbani kwa baba.

Lakini kundi la vijana wa rika moja waliishi pamoja kwenye vijiji vyao mahsusi, huko walikuwa na kanuni, uongozi na utaratibu wa maisha yao. Moja ya mambo waliyopaswa kuyazingatia, ni kujenga ukaribu baina yao na kuepuka kabisa uchoyo.
Ilikuwa muhimu sana kwa kijana wa kiume anapoenda nyumbani kwa baba yake kupata mlo, basi walau aambatane na vijana wenzake wawili au watatu kupata nao mlo.
Mimi nimewahi kuishi jirani na Wanyakyusa, kwa kweli uchoyo hauko kwenye hulka yao kabisa. Na kama ukikutana na Mnyakyusa mchoyo, basi huyo ana matatizo yake mwenyewe au ameiga tabia hizo kwingineko.
Maana kati ya vitu wanavyovipenda ndugu zetu hawa ni kula vizuri, ukipata nafasi tembelea mkoani kwao Mbeya ujionee mwenyewe maakuli ya ndizi, maparachichi, mchele na kadhalika.
Kwa hiyo kama kijana akija nyumbani kula peke yake, aliweza hata kuadhibiwa na baba yake. Kula pamoja kwa vijana wa kiume wenye rika moja, ilichukuliwa kuwa ni baraka.
Lakini pia kwa kijana wa kiume kula peke yake au na vijana wadogo au na wanawake, ilichukuliwa kuwa ni kujilaani. Kwa mfumo huo, wanawake walikula peke yao na watoto wadogo na mabinti ambao bado hawajaolewa walioko nyumbani.
Hawa ndugu zetu wana kanuni nyingi za kijadi zilizoongoza maisha yao ya kila siku. Mathalan, kijana wa kiume aliyepevuka lakini hajaoa bado hakupaswa kulala kwao, walitengewa vijiji vyao.
Kama wangeruhusu walale kwao, moja ya athari ni kusikia minong’ono ya wazazi wake kwa mazungumzo yao ya faragha ya usiku. Nadhani unanielewa namaanisha mazungumzo ya aina gani haya ya usiku.
Lakini pia kwa kijana kuwa kapera hadi makamu ya rika kubwa kidogo kulikuwa na faida zake.
Kijana wa aina hiyo alichukuliwa kuwa mpiganaji shupavu kuliko aliyeoa, vijana wa aina hiyo walikuwa muhimu sana kwenye yale mapigano ya himaya moja dhidi ya nyingine.
Hata wale vijana wakorofi waliokuwa wababe walivumiliwa na jamii bila kutengwa, maana wangetumika kama askari hodari wa kutegemewa mapambanoni.
Japokuwa hiyo haikuwa na maana kuwa wanaume waliooa hawakutiliwa maanani, hao walitumika kama askari wazoefu kwenye shughuli mahsusi za uvamizi wa kuteka mifugo ya himaya pinzani.
Kwa upande wa imani walihofu zaidi kuadhibiwa kwa mtu anayetenda uovu akiwa hapa hapa duniani, kwamba mtenda mema hunemeeka lakini mtenda maovu hulaanika.
Mathalan, ilidhaniwa kuwa mwanamke mgumba alipatwa na hali hiyo kutokana na maovu hasa kushindwa kutimiza majukumu yake, hivyo siku zote aliishi na hatia hiyo.
Dawa za kijadi ni muhimu mno katika kufanikiwa kwenye kulima, kufuga, mapenzi, mapambano, kuponya, kulinda, kulipiza kisasi au kumdhuru adui na kujilinda dhidi ya washirikina.
Mitishamba hiyo iliweza kutumika kuadhibu wezi, wazinzi au kulaani mashamba ya maadui yasitoe mazao kama ilivyotarajiwa. Matumizi yake yaliweza kuwa halali au haramu, kutegemeana na dhamira ya mtumiaji husika.
Pia niwafahamishe kuwa, kama tulivyochambua awali tulipoanza kuwatembelea ndugu zetu hawa, tulizingumzia juu ya Chifu kudhibitiwa na washauri wake.
Moja kati ya mambo hayo ni kuhakikisha kuwa Chifu husika hana ndumba na hawezi kufanya jambo lolote bila kuwashirikisha hao washauri wake ‘mafumu.’ Lakini msisahau kuwa, Chifu alikuwa na nguvu zake za kubariki himaya kwa kilimo na mambo mengine kama tulivyowahi kueleza.
Imani za kuwepo kwa ushirikina zina mashiko sana ndani ya kabila hilo, tena pengine ni tofauti na jamii nyingine ambazo tunafahamu baadhi ya mambo yao ya kishirikina.
Mathalan, naamini umewahi kusikia masimulizi ya watu wanaoruka na ungo au pembe, lakini kwao kuna wachawi wanaoruka na chatu. Usiogope, ni ujadi wa kishirikina huo! Aina hii ya wachawi wanaoruka na chatu, ndiyo walioogopwa zaidi kutokana na kudhuru watu na mifugo nyakati za usiku.
Wengi kati ya hawa walirithi ushirikina huo kutoka kwa wazazi au ndugu; waliutumia kwa dhamira mbaya ya kuwadhuru wenye mafanikio ya mifugo na mazao.
Mlo wa chatu hao wa kishirikina waliotumiwa na wachawi hao walioruka wakiwa watupu migongoni mwa chatu wao, ni nyama na maziwa yaliyotumiwa na waombolezaji wa wahanga wa ushirikina huo.
Tufundishane jambo moja japo lisikutishe nikikutaarifu jambo hilo, ni muhimu pia ukilifahamu. Mara nyingi mtu anapokufa kwa ulozi, wale walozi wake huwa si watu wanaotoka mbali na makazi ya mhanga, wanaweza kuwa hata majirani zake.
Na kama wamemuua kwa kifo cha bandia, yaani wamemchukua msukule, basi katika kusanyiko lenu waombolezaji msukule huyo huweza kuletwa na hao walozi ili wamtese tu hisia zake.
Kwa kushuhudia jinsi watu wanavyomlilia, wakati kiukweli ni kuwa hajafa. Lakini atakapokuja hapo, ninyi waombolezaji hamuwezi kumuona isipokuwa dalili kubwa ni kuongezeka kwa kilio hasa kwa nduguze wa karibu.
Mathalan, kama mama kafiwa na bintiye basi ndugu jamaa na majirani wanapokuja kumfariji atalia. Lakini kuna wakati anakuwa ametulia tu, lakini ghafla akianza kuangusha kilio kikubwa cha uchungu mkali naye alishalia mno tangu mwanzo, basi muda huo bintiye aliyechukuliwa msukule ameletwa eneo hilo.
Naye hulia sana muda huo sio kwa kuwa amemuona, bali ni ule muunganiko wa hisia za kiroho baina yake na mwanaye.
Basi hata hao chatu wa kishirikina niliowaeleza punde, wanapokuja kwenye mkusanyiko wa msiba wa aliyeuliwa na washirikina wao, hawaonekani kwa macho ya kawaida.
Isipokuwa kwa wachache wenye uwezo huweza kuwaona, hawa katika kabila hili huaminiwa kuwa walinzi. Wengi wao huwa wakuu wa vile vijiji vya mikusanyiko, nguvu za walinzi hawa na wale walozi ziko sawa.
Isipokuwa namna na matumizi yake ni tofauti, walozi ni waovu wanaodhamiria kudhuru na wale walinzi huzuia uovu kwa wema.
Kwa kawaida wale waliokuwa na uwezo wa kudhibiti walozi, waliwaadhibu na kulinda mifugo na mashamba. Waliweza kuwafanya walozi na watoto wao waugue, wakitumia nguvu ya chatu au laana iliyotamkwa kwa kunuizia pumzi.
Kunuizia kwa pumzi ni sawa na kwenye makabila mengine wanavyotumia mavumba ya ulozi, kwa kusema maneno ya kishirikina kisha kuyapulizia kwenye mwelekeo wa yule anayedhamiriwa kudhuriwa.
Lakini yote haya ya uwezo wa walozi au wale walinzi kutumia nguvu za chatu, si mambo yaliyowekwa hadharani. Maana kufanya hivyo ni kujisifu na kujivuna, jambo ambalo halikukubalika.
Wakati mwingine si wachawi tu walioadhibiwa kwa kutumia nguvu hizo, hata wale waliokuwa na tabia zisizokubalika kwenye jamii yao waliadhibiwa pia.
Mathalan, waliowakaidi wazazi wao kwa kiwango cha kukiuka au kuwadharau wakwe waliadhibiwa.
Mwanamke aliyemfokea mumewe au kumpiga, mwanamke aliyeendelea kuzaa huku binti mkwewe akiwa naye anazaa naye aliadhibiwa. Maana mwanamke wa aina hii alichukuliwa kutojua ukomo wake, hasa kama mwanaye wa kiume ameshaoa na sasa mkwewe anazaa naye bado anazaa, hiyo haikuonekana kama picha nzuri.
Lakini unielewe kuwa, adhabu za wakosaji wa kawaida na walozi zilitofautiana kwa viwango maana walozi hawakuvumiliwa kabisa. Ila hawa wakosaji wengine waliadhibiwa ili wajirekebishe, mara nyingi adhabu zao ilikuwa ni kufanywa waugue kwa kipindi kifupi ili wajirekebishe.
Inawezekana hata baadhi ya Wanyakyusa wenyewe hawajawahi kuyasikia haya. Lakini haya ni mambo yaliyoanzia tangu walipokuwa kule Konde-Karonga, hata walipoingia walipo sasa.
Kwa hiyo ushirikina upo kwenye kabila hilo tangu zamani na ulihofiwa sana, ndiyo maana walibuni namna za kuukabili ikiwemo kutumia nguvu zile zile za washirikina kuwadhibiti.
Pia waliwatenga waliobainika kuwa washirikina, kwa kuwafukuza kwenye vijiji au hata kwenye himaya kabisa. Kwa wanawake waliogundulika kuwa walozi, wengi waliachwa na waume zao.
Japokuwa kuna ajabu moja, mlozi hakuuawa kwa kuwa endapo ingetokea vita baina ya himaya anayotoka na nyingine, basi ufundi wake ulihitajika kushinda vita hiyo.
Haya ni mastaajabu ya kijadi hayo! Na katika kumtuhumu mtu kwa ulozi kama kulikuwa na mashaka yoyote basi walitumia ‘umwafi’ kwa kumnywesha, kama hakutapika basi ana hatia.
Familia zilizotuhumiwa kwa ulozi bila kujulikana ni nani hasa mlozi husika ndani ya familia hiyo, zilikuwa na hila ya kumchagua mtu wa familia yao ambaye akinyweshwa hiyo dawa angetapika kirahisi.
Maana iliaminika kuwa yeyote katika familia hiyo angepewa dawa hiyo, kama kuna mlozi ndani ya familia hiyo lazima ingebainika.
Masimulizi yetu ya utopevu wa kijadi yanazidi kunoga lakini nafasi yetu nayo imeishia hapa. Tukutane tena kesho ili tuendelee na ujadi wetu.

Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Agosti 15, 2009.


Comments