Featured Post

WANYAKYUSA-3: MTU ALIYEUGUA HADI KUKARIBIA KUFA, ALITENGWA

Ngoma ya asili ya Wanyakyusa.

Na Innocent Nganyagwa
NAWAKARIBISHENI kwa mara nyingine tena kwenye safu yetu ya kina ya uchambuzi wa asili na fasili za makabila yetu.
Kwa mara ya tatu tunaendelea na ziara yetu kwa ndugu zetu Wanyakyusa, Wabantu kutoka kusini mwa nchi yetu, mkoani Mbeya.
Waama nilipowatajia chanzo cha Malkia Nyanseba, haikueleweka vyema kwa kuwa najua wengi wenu mnafahamu kuwa Wabantu hutokea kusini mwa bara hili. Lakini kwa uyakini jambo hilo si kweli, hasa ukifuatilia vyanzo vya kihistoria.

Pia mara nyingi nimewahi kuelezea juu ya mbari zilizozalisha makabila, ambapo wakati mwingine kuna mchanganyiko wa mbari zilizozalisha jamii mchanganyiko ambazo nazo huzalisha makabila.
Kwa hiyo, kama nilivyowaahidi kuhusu ufafanuzi juu ya Malkia Mnubi Nyanseba na kizazi chake kilivyochanganyika na Ubantu uliokuja kuzalisha Wanyakyusa, nitawafafanulia yote hayo kadiri tutakavyoendelea na uchambuzi wetu.
Basi kwa sasa tuendelee na ziara yetu, kwa kujielekeza kwenye awamu ya leo na yale tuliyoyadhamiria kuyazungumzia.
Wanyakyusa walijifunza sehemu kubwa ya ufundi wa kutengeneza vyungu kutoka kwa Wakinga, waliowagubika kwa utamaduni wao. Nilieleza kuwa nchi ya Ukinga na Unyakyusa zinapakana katika maeneo yake.
Kwa hiyo, uzalishaji chumvi, utengenezaji mitungi, kufua vyuma na kutengeneza nguo za kijadi ni mambo waliyojifunza kutoka kwa majirani zao hao wa Kikinga.
Ni majirani zao hao ndio waliofanya nao zaidi biashara ya mabadilishano ya bidhaa, wao waliwapa chakula kwa kuwa kwao wana nchi yenye neema na rutuba, nao Wakinga wakawapa silaha na zana za kilimo.
Lakini tulieleza pia kuwa licha ya kuwiana na Wakinga, kwa mambo ya ndoa hawakuchanganyika nao maana kwao wanawake wa Kikinga walikuwa duni mno kulinganisha na wanawake wao wa Kinyakyusa.
Hayo ni baadhi tu ya tuliyoyaona kwenye sehemu ya pili, pia kwa ufupi sehemu ya kwanza ya ziara yetu kwa ndugu zetu Wanyakyusa.
Kama tulivyoona umuhimu wa wale watawala wao wa himaya ndogo ndogo, machifu hao walikuwa na mfumo wa kuhudumiwa kwa kupewa sehemu ya mazao ya chakula, pamoja na mambo mengine ambayo wakiyahitaji ilikuwa lazima wapatiwe.
Kwa hiyo, ukitazama kwa muhtasari namna yao ya kuishi kijadi, mtawala alikuwa na ukiritimba wa baadhi ya mambo, lakini hakuwa na hodhi kamili ya madaraka.
Maana kuna sababu zilizofanya Baraza la Utawala kumuondoa madarakani, isipokuwa hiyo haikumuondolea umuhimu wake kama vile kubariki nchi yake kwa ajili ya msimu wa mvua.
Kwa upande wa wakazi wa himaya, waliishi kwenye jamii za marika za koo zisizo na undugu, lakini waliweza kulinda umoja kwa baadhi ya tabia kuwekewa kanuni za kutekelezwa kwa pamoja.
Mathalan, kushirikiana kwenye baadhi ya shughuli, kama vile kulima, kula na hata kunywa pombe pamoja ilikuwa ni jambo la muhimu. Katika shughuli hizo kama vile kilimo, licha ya kusaidiana mara kadhaa, lakini pia ilikuwa ni lazima uwezo wa kulima na kuhudumia mashamba baina ya kaya moja na nyingine ulingane.
Kwa mfumo huo, iliwezesha himaya nzima kuwa na uwiano wa neema ya mazao ya chakula, maana hakukuwa na waliowazidi wengine kwenye kulima na aliyezidiwa alisaidiwa.
Lakini sehemu kubwa ya mazao yaliyopatikana kwenye kilimo hicho kama yalifanyiwa biashara, basi ilikuwa baina ya zile himaya na wahamiaji, na siyo baina ya himaya na himaya kwa kuwa zote zilikuwa na aina moja ya bidhaa, hivyo isingefaa kwa biashara iliyokuwa ya mabadilishano.
Lakini pia kuna wakati himaya hizo zilikabiliana kwa mapiganao madogo madogo au kutishiana kupigana. Hilo lilidhihirisha udhaifu wa kutokuwa na uchifu mkuu, hali iliyosababisha mapigano ya mara kwa mara baina ya himaya japo yalikuwa madogo madogo. Mapigano hayo yalikoma baada ya uvamizi wa Wangoni.
Kwa sasa kuna mengi yamebadilika kwenye kabila hilo, lakini kuna baadhi ya mambo yalikuwa yakitendeka zamani ambayo yalikuwa ni sehemu ya maisha yao.
Mathalan, ilikuwa mtu akifa, aliachwa badala ya kuzikwa au akiugua hadi kukaribia kufa, hutengwa.
Usishangae mjadi, hayo ni mambo yao ya wakati huo! Licha ya simulizi hizo za jadi zao za kizamani, lakini pia Wanyakyusa walikuwa na mashujaa wao tangu enzi za Konde waliopigana dhidi ya jamii za wavamizi wakiwemo wakoloni.
Katika historia yao, mapigano ya Konde ya mwaka 1897 yaliyowahusisha Wamisionari wa Kizungu, Wajerumani, Wanyakyusa na Wakinga yanakumbukwa sana.
Baadhi ya wapiganaji wa Kinyakyusa walioshiriki mapigano hayo ni pamoja na Muambaneke, Chifu Masakiwande na Chifu Makelimba.
Kwa pamoja, Wakinga na Wanyakyusa waliwapiga vibaya mno wavamizi wa kigeni wa Kizungu kwa kutumia mfumo wa mapigano uliokuwa maarufu sana Uheheni.
Kwa hiyo, haishangazi kutumika kwa mbinu hizo za kivita za Kihehe, maana Wakinga waliwafundisha Wanyakyusa kwa kuwa ndio waliowauzia silaha katika zile biashara zao za mabadilishano ya bidhaa.
Wajerumani waliokuwa wanatawala upande wa Wakonde kuelekea Unyakyusani, walizinduka baadaye baada ya kipigo kikali na kutumia nguvu kubwa ili kushinda vita hiyo.
Nitaendelea kuwamegea taratibu mambo ya ndugu zetu hawa kadiri tutakavyoendelea na ziara yetu kwao.
Kesho tutazama kwenye kina zaidi, kwa kuchambua mambo yao ya kujamiiana na baadhi ya mila za ndani tofauti na yale tuliyoyasimulia hadi sasa. Basi nakusihi usikose kujumuika nami kwa utopevu zaidi wa ujadi wa Kinyakyusa.

Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Julai 25, 2009.


Comments