Featured Post

WANYAKYUSA-2: CHIFU MZEE ANAYEUGUA HULETA MKOSI

Nyumba ya asili ya Wanyakyusa.


Na Innocent Nganyagwa
KARIBUNI tena ndugu zangu kwenye safu yetu ya utopevu wa kijadi. Basi tuendelee na ziara yetu ya kuwatembelea ndugu zetu Wanyakyusa, wanaopatikana mkoani Mbeya.
Tulianza kuwatembelea jana, basi nitawakumbusha tuliyoyachambua juu yao tulipowatembelea kwa mara ya kwanza kabla hatujaendelea na uchambuzi wa mambo yao zaidi.

Tulisema kuwa ndugu zetu hawa ambao kwa asili huitwa pia Wasokile, Wangonde au Wankonde, wanapatikana kwenye eneo pana sana linaloanzia kaskazini mwa nchi jirani ya Malawi hadi kusini mwa nchi yetu huko mkoani Mbeya.
Wanyakyusa ni Wabantu na huzungumza lugha yao ya Kinyakyusa, japo ni watu wa jamii hiyo hiyo moja wenye majina tofauti kutokana na mgawanyiko wa makundi ya jamii zao kwenye eneo wanalopatikana.
Wanaoishi kwenye eneo la safu ya milima Livingstone kuanzia upande wa Mto Rukuru kaskazini, Karonga huko Malawi, hufahamika zaidi kama Wangonde au Wankonde.
Lakini walio upande wa pili yaani huku Mbeya hapa nchini, hufahamika kama Wanyakyusa.
Licha ya lugha ya ndugu zetu hawa kuwa Kibantu, lakini ina miundo tofauti ndani yake kwa matamshi na silabi zake zilivyo.
Ni lugha inayojitofautisha hata na baadhi ya lugha nyingine za Kibantu, za jamii wanazopakana nazo kwenye eneo la nchi yao.
Nadhani unafahamu kuwa mara nyingi tumerudia kufafanua kwenye safu hii kuwa makabila yanayotokana na mbari moja huwa na muingiliano wa utambulisho kwa baadhi ya mambo, yakiwemo matamshi ya baadhi ya maneno ya lugha.
Lakini pia lugha ikiingiliwa na lugha nyingine hasa jamii zaidi ya moja zinazowiana, lazima kutatokea mabadiliko kadhaa madogo madogo. Mabadiliko hayo baadaye huzoelekea na kukubalika kuwa matamshi halisi, japo ukifukua kwenye vyanzo vya utafiti utagundua mwanzoni haikuwa hivyo.
Tukirudi kwenye mambo ya Wanyakyusa tuliyoyaeleza, ni kwamba kundi hili la wanaoitwa Wanyakyusa zamani walipokuwa ‘Nyasaland’ yaani Malawi kandoni mwa Mto Songwe waliitwa Wangonde.
Lakini baada ya kuvuka na kuja huku ndiyo wakawa Wanyakyusa.
Awali utamaduni wao ulikuwa ukirandana kwa ukaribu kwa makundi yote ya pande mbili za eneo lao.
Hali hiyo iliwachanganya hata watawala wa kikoloni, maana kwa wakati huo upande wa Nyasaland ulikuwa chini ya Waingereza na huku kwetu tulikuwa chini ya Wajerumani.
Kutokana na kufanana mno kwa utamaduni wa jamii za pande hizo mbili watawala wa upande huu wa pili (Wajerumani), waliamua kupaita Konde wakifananisha na jamii za wale walio upande wa kwanza.
Lakini, kama ambavyo tumegundua mara kadhaa juu ya jamii za kale zilizokuwa na kawaida ya kuzurura na kuhamia maeneo ya mbali katika kutafuta maisha bora, basi hata hawa Wanyakyusa nao walikuwa hivyo.
Tukirudi nyuma zaidi kwenye chanzo chao, kwa asili walitokana na Malkia wa Kinubi aliyeitwa Nyanseba. Mtawala huyu alipinduliwa na wafugaji wazururaji, waliohamisha utawala kutoka kikeni kwenda kiumeni na kusimika Wafalme badala ya Malkia.
Lakini hila hiyo haikufaulu kufuta nguvu na uwakilishi wa kikeni ndani ya jamii za baadaye zilizozalisha kabila la Wanyakyusa, kutokana na mfumo wao wa utoaji majina ya watoto katika ujadi wao wa zamani.
Ilikuwa akizaliwa mtoto wa kiume huchukua jina la ukoo wa mama na wa kike la baba, Mjadi, tulipofahamishana jambo hilo tulifahamishana jambo lingine linalohusiana na utamaduni wa majina ya Kinyakyusa.
Lakini tuliona kuwa, jamii mbili za watu hawa yaani wale Wangonde waliobaki kule kusini mwa nchi yao na hawa Wanyakyusa, walitofautiana katika maendeleo.
Tofauti nyingine ni kuwa hawa waliofahamika kama Wanyakyusa, waliishi kwenye mikusanyiko midogo midogo wakisimamiwa na tawala nyingi ndogo ndogo za Kichifu.
Hata hivyo licha ya udogo na mgawanyiko wa tawala zao, lakini waliweza kuwakabili vyema maadui wa Kisangu, Kimerere na Kingoni waliowashambulia mara kwa mara.
Wanyakyusa hapo baadaye waliingiliwa na utamaduni wa Wakinga, waliosambaa upande wa magharibi mwa nchi yao ya Ukinga wanakopakana na Wanyakyusa.
Kanuni nyingi za Machifu wa awali wa himaya ndogo ndogo za Kinyakyusa, zilitokana na mchanganyiko wao na Wakinga na kusababisha utamaduni mchanganyiko.
Kwa kawaida watawala hao wenye nguvu za kimiujiza waliishi kwa kujitenga, lakini upeo wa madaraka yao ulidhibitiwa na mabaraza ya utawala.
Katika udhibiti huo kama mtawala akizeeka sana au kuugua kupita kiasi, waliamini anaweza kusababisha mkosi kwa himaya yake na kuisababishia janga la ukame litakalofanya mavuno yawe haba.
Ikifikia hali hiyo kwa Chifu kuzeeka na kuugua mno, wale wajumbe wa baraza la utawala waliamua kumnyonga Chifu huyo ili kuepusha mkosi kwa himaya yao.
Licha ya mfumo huo jambo lingine walilolitekeleza kwa mpangilio wao wa Kijadi, ni kuishi kwenye jamii yenye mafungu ya madaraja ya umri.
Mafungu hayo yaliyotokana na koo tofauti tofauti na si koo zenye undugu, licha ya mfumo huo ambao kwa juu juu unaonekana dhaifu lakini kwa ndani walikuwa imara.
Moja kati ya mambo ya kujivunia ya kabila hilo ni kuweza kujilinda wasichukuliwe utumwa, japo wale ndugu zao waliowaacha Konde kule Karonga walishawahi kufanywa watumwa.
Kwa hiyo, ukiangalia hata zile sababu zao za kuogopa mkosi kutokana na Chifu kuzeeka mno au kuugua, ni kwa sababu ndugu zetu hawa ni wakulima hodari wa mazao mbalimbali.
Kama unavyoyaona yalikuwa mengi, ndiyo maana yamechukua nafasi kubwa. Lakini nadhani ni vyema tukumbushane ili tuweze kuunganishia kutokea hapo.
Nafahamu kuwa ule muunganiko wa Malkia wa Kinubi aliyeitwa Nyanseba ndiyo unawachanganya, hasa ukichukulia kuwa sehemu kubwa ya Wanubi si Wabantu.
Jambo lingine walilokuwa na utaratibu nalo, ni kuamua na kutatua migogoro kwa mashtaka ya kijadi.
Maamuzi ya aina hii hayakuwa ya shinikizo la watawala au watu wenye nguvu za kijamii, mara nyingi walipenda ufumbuzi upatikane kwa usuluhishi wa majadiliano na maelewano baina ya waliokoseana wakisaidiwa na watu wengine.
Pia kutokana na ule mfumo wao wa kuishi kwenye madaraja ya umri kijamii yasiyolazimu ndugu kuwa kwenye eneo moja, awali hawakuwa na muendelezo wa majina ya ukoo kwa vizazi vitatu au zaidi mbele kutokana na mfumo huo.
Kwa mtindo wao huo wa maisha na hata utawala wa zile himaya ndogondogo, kimsingi hawakuwa walimbikizaji au wenye tamaa ya kuhodhi mali nyingi.
Japo mara kadhaa mifarakano ilisababishwa na kuingiliana kwenye mipaka ya maeneo yao waliyoishi.
Hawakuwa wawindaji na kama walilazimika kufanya hivyo, ni kwa ajili ya ulinzi wa maisha na himaya ya maeneo yao.
Japo hilo halikuwafanya wawe wazembe, maana walijilimbikizia silaha bora za kijadi kwa kujilinda endapo wangevamiwa.
Kwa kuwa himaya zao zilikuwa ndogo ndogo na zilijumuisha wakazi ambao si wenye undugu wa mfululizo wa vizazi vya koo zinazowiana, waliepuka sana kusafiri na kuondoka kwenye himaya kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo.
Na ikilazimu kusafiri, basi safari hiyo huchukua muda mrefu zaidi kwa sababu mara kwa mara iliwalazimu kujificha na kusoma mazingira wanayopita kama hayana uadui.
Safari hizi ninazozungumzia hapa ni zile za kijadi za zama hizo za ujima zilizotumia muda kadhaa hadi kufika kituo cha mwisho.
Katika ule mgawanyo wao wa kazi, ukamuaji maziwa ulifanywa na wanaume tu wanawake walikatazwa kabisa kufanya hivyo.
Pia mwanamke hakupaswa kujipa kipaumbele kwenye mambo ya mikusanyiko ya kijumuiya, walipaswa kuwa watiifu na wanyenyekevu kwa mabwana zao, kubishana na mume ni jambo lililokatazwa kabisa.
Lakini hilo halikuondoa thamani yao, mathalan, kwenye kuolewa ng’ombe walitozwa kama mahari na wakati mwingine kwa idadi kubwa.
Kwa upande wa ufundi wa kijadi, ndugu zetu hawa zaidi ya kutengeneza aina ya mikeka ya kikwao hawakuwa kama Wabantu wengine waliotengeneza vyungu, mitungi, nguo, kufua vyuma au kuzalisha chumvi.
Hili linaweza kukushangaza, maana nadhani unatambua ile sifa yao ya vyungu vya Mbeya vinavyopikiwa maharagwe.
Walijifunza baadaye usanii huo, japo watu waliochanganyika nao na kujifunza kwao walikuwa na utata wa uwiano nao. Nawazungumzia Wakinga ambao ndiyo kwa sehemu kubwa walifanya nao biashara ya mabadilishano ya bidhaa.
Wanyakyusa waliwapa chakula Wakinga, nao wakawapa silaha na zana za kilimo walizojivunia sana kuzimiliki.
Hata hivyo, licha ya kuwiana na kushirikiana na Wakinga kwa kiasi kikubwa, walijizuia kabisa kuchanganyika nao kwa kuoana nao.
Maana waliwachukulia wanawake wa Kikinga kutokuwa wasafi kuolewa nao, kwa kuwa waliwaona duni kulinganisha na jinsi wanawake zao wa Kinyakyusa walivyo.
Bado kuna mengi ya kuzungumzia kuhusu ndugu zetu Wanyakyusa, lakini kwa leo tuishie hapa tutaendelea tena na simulizi zao kesho.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Julai 18, 2009.

Comments