Featured Post

WAKIMBU: KABILA LILILOGAWANA ENEO LA HIMAYA

Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea mkuki kutoka kwa Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa ikiwa ni ishara ya kusimikwa kuwa Chifu wa makabila ya Wakimbu na Wasafa katika mkutano wa hadhara aliouhutubia kwenye uwanja wa Sabasaba mjini Chunya Agosti 1, 2017.

Na Innocent Nganyagwa
KARIBUNI tena ndugu zangu kwenye safu yetu ya utopevu wa mambo ya kijadi, tunapopata fursa ya kufahamishana asili zetu kupitia makabila mbalimbali yaliyopo hapa nchini na kwingineko barani Afrika.
Baada ya kuwatembelea Warangi, leo tunapiga hodi kwenye kabila lingine ambalo linapatikana kwenye eneo mkabala na walipo Wanyiramba na Wanyisanzu.

Inawezekana makabila haya tunayoyatembelea sasa kwenye eneo tulilopo hujawahi kuyasikia sana, lakini yapo na yana mambo yao japo yana tofauti kidogo kulinganisha na makabila mengine tuliyowahi kuyatembelea awali. Tofauti kubwa hasa kama ambavyo tutaona kwa hawa Wakimbu, ni kuwa, maeneo yao yanamega mikoa kadhaa na kuyaweka makabila hayo katikati ya mikoa bila kugubikwa na kumezwa na makabila makubwa yanayowiana nayo.
Ndugu zetu hawa ambao wanatokea mbari ya Kibantu, wanapatikana katika nchi ya Ukimbu yenye eneo pana linalomega maeneo ya mikoa kadhaa. Nadhani tunaelewana nikisema nchi ya Ukimbu, maana hapo zamani sehemu au eneo linakopatikana kabila husika huitwa nchi ya kabila lile.
Mathalan, ni sawa na kusema kuwa nchi ya Uhehe ilipakana na nchi za Usangu, Upangwa, Uluguru na nchi za makabila mengine kwa pande husika. Ndiyo maana siku zote huwa nasisitiza kuwa, ni muhimu kufahamu kwamba mipaka ya nchi zilizoko kwenye ramani, ikijumuisha mipaka ya mikoa ni ya kiutawala wa kisasa. Lakini makabila yalikuwa na maeneo yake ya himaya, ambapo ndani yake pia zilikuwemo himaya za machifu kadhaa wa kabila husika.
Kwa maana hiyo, ndugu zetu hawa wapo kwenye eneo lililopo katikati ya mikoa minne ya Singida, Tabora, Iringa, Songwe, Katavi na Mbeya. Wapo kuanzia Sikonge, kupitia Uyui mashariki mwa Tabora, Igalula, Tura, Kizengi hadi Singida magharibi na Manyoni.
Na kwa upande wa ile mikoa ya Mbeya, Songwe na Iringa, eneo lao linaanzia Idodi, Pawaga, Mbarali, Chunya hadi huko Mpanda mkoani Katavi.
Hiyo ina maana kuwa wako kwenye eneo pana sana, wakiwa katika mafungu kadhaa kwenye hiyo nchi ya Ukimbu.
Katika eneo hilo kubwa kuna maeneo ambayo wanapatikana kwa wingi zaidi, kama vile Tyumba, Manyoni na tarafa ya Itigi.
Unapozungumzia Wakimbu, kama ambavyo mara kwa mara tumekuwa tuking’amua tunapotembelea makabila mbalimbali, unazungumzia mafungu ya jamii ambayo kwa pamoja ndiyo yanaunda kabila zima.
Basi hawa Wakimbu wako hivyo na walikuja kwenye eneo la Ukimbu wakiwa katika mafungu, wakitokea kaskazini zaidi mwa nchi yetu.
Ili uelewe vyema maana ya kusema kuwa hili ni kabila lililogawana eneo la himaya, inatubidi tuanze kuyatazama hayo mafungu yenyewe ya Wakimbu.
Kundi la kwanza la Wakimbu kuingia nchi iliyokuja kuwa Ukimbu hapo baadaye ni Wanyisamba, ambao waliingia kutokea upande wa Unyangwila, yaani Ugogoni. Hawa ndiyo hasa walijulikana kama Wakimbu mwanzoni, kwanza kwa kuwa wao ndiyo walitangulia kuingia nchi ya Ukimbu na kusababisha kuzaliwa kwa himaya nyingine za utawala kwenye eneo lao.
Hayo tutayaona kadiri tutakavyoendelea na simulizi zao.
Basi hawa Wanyisamba wakahamia kusini magharibi zaidi wakivuka Lupa (mkoani Songwe kwa sasa) na kuanzisha himaya ya Wikangulu.
Kilichowavusha na kuwafanya waende kuanzisha himaya hiyo ni ukame, mwanzoni wakati wanaingia eneo hilo walienda kulowea Chunya.
Kiongozi wao na mwanzilishi wa hiyo himaya ya Wikangulu alifahamika kama Mbela, huyu alikuwa na nduguze watatu ambao aliwatawanya na kuwamegea maeneo waliyoenda kuanzisha himaya zao.
Ndugu yake wa kwanza aliitwa Magulunjega, aliyeanzisha himaya ya Mwendo katika eneo la Lukwati.
Himaya ya pili ilikuwa ya Mweli iliyokuwa Igululilu, neno ambalo lina maana inayotokana na muunganiko wa maneno mawili; Igulu (juu) na lilu (kweusi), kutokana na jinsi vilima vinavyozunguka eneo hilo vilivyo virefu na kufanya kileleni kuwa na giza la mawingu.
Himaya ya tatu ya Ilasi iliyokuwa Itenda, ilianzishwa na aliyekuwa mdogo kuliko wote kati ya wale ndugu wa Mbela.
Tofauti na wale ndugu wengine ambao walimegewa maeneo ya kuanzisha himaya na ndugu yao mkubwa, huyu Ilasi alianzisha himaya yake kwa kuasi baada ya kutoroka.
Hakutoroka peke yake, bali aliambatana na wafuasi wake na kwenda kujitwalia eneo walilokwenda kuishi.
Kisa cha kutoroka ni kujisikia kinyongo kutokana na kuhisi kutotendewa haki, kwa kutomegewa eneo la kutawala kama walivyopewa wale nduguze. Baadaye kaka yake alipogundua jambo hilo, akaamua kumuidhinishia eneo hilo alilokimbilia na kujimegea kuwa himaya yake ya utawala, wakaridhiana.
Kwa kuwa eneo la Ukimbu ni kubwa sana likianzia Chunya hadi Singida kwa upande mmoja, pia Iringa hadi Mpanda kwa upande mwingine, wale ndugu watatu wa Mbela waliogawiwa maeneo ya kuanzisha himaya, nao waliwagawia watoto zao maeneo ya kuanzisha himaya zao.
Mweli alianzisha himaya za Kasekela na Ipili, himaya ya Mwendo ilizalisha himaya za Isungi na Isote, na yule Ilasi alinzisha himaya nyingine ya Nkila.
Kwa sehemu kubwa, himaya nyingi zilizokuwa ndani ya nchi ya Ukimbu zilianzishwa kwa maridhiano.
Na ukitazama ukubwa wa eneo lao kijiografia na idadi ya himaya zilizopo ndani yake, inabainisha kuwa Wakimbu walikuwa na maarifa na ujanja wa kuridhiana baina yao hata na wageni waliolowea kwenye eneo lao.
Lakini kuwiana huko na kuridhia wageni hakukumaanisha kuwa wao ni dhaifu, japo kuna baadhi ya wageni kwenye maeneo ya pembezoni waligeuza fadhila hizo kama njia ya kujitwalia na kuhodhi himaya kwa mabavu, kama tutakavyoona hapo baadaye.
Kwa kuweza kutangamana na wageni waliolowea na kuwapa maeneo ya kuishi na kuanzisha himaya, hasa pembezoni, kuliwezesha nchi ile ya Ukimbu kuendelea kubaki na ukubwa wake kama ilivyo, japo ipo kati kati ya mikoa kadhaa mkabala na makabila mengine.
Lakini licha ya hawa Wakimbu kugawana himaya kwa kuridhiana, wao wenyewe wakati wanaingia eneo hilo walitumia mabavu kuhodhi himaya.
Lile kundi la kwanza nililolitaja kwamba ndiyo lilitangulia kuingia nchi ya Ukimbu, yaani Wanyisamba, walipofika waliwakuta watu wafupi wenye maumbo madogo.
Wao waliwaita watu hao Wapantama, kutokana na tabia ya watu hao kujificha nyuma ya miti wanapoona maadui au watu wasiowajua.
Kupantama kwa lugha yao ya Kikimbu ni kufichama. Basi Wakimbu waliwapiga na kuwaua watu hao na kuteka eneo hilo walipoingia awali wakitokea kaskazini.
Katika utawala wao wa kichifu, awali ilikuwa kama ikitokea chifu amefariki, alirithiwa na mwanaye.
Lakini kutokana na matatizo yaliyojitokeza, hasa kwa watoto hao wa machifu kuuawa kwa mbinu na wale waliowaonea kijicho kabla hata ya kushika himaya wakati baba zao wako hai, walibadili mfumo huo.
Ikawa mtoto wa dada wa chifu ndiye anayetawazwa kuwa chifu badala yake, hiyo pia ni kutokana na kuwa na uhakika wa ukoo kwa damu, maana mtoto wa dada ni wa uhakika zaidi.
Hapa inabidi niwape ufafanuzi kidogo. Wakimbu kwa kawaida ni kabila la kiumeni, yaani ukoo kwa kuzaliwa huchuliwa upande wa baba.
Lakini kwenye koo za kichifu utambulisho wa ukoo ulichukuliwa upande wa kikeni, kwenye lugha ya kigeni yaani Kiingereza, wao kwa asili ni ‘patrilineal’.
Lakini kwa zile koo za kichifu ni ‘matrilineal’. Nadhani tunaelewana.
Kwa hili la koo za kichifu za Wakimbu, tunaweza kuwalinganisha na Wazaramo, japo si kiutawala. Wazaramo kiukoo ni patrilineal lakini miiko yao inatoka matrilineal, yaani upande wa mama, wenyewe huita mtala na hutambuana kwa urahisi kwa njia hiyo.
Mathalan, wanapokutana kwa mara ya kwanza na wakawa na majina yanayofanana, katika kuthibitisha kama wao ni ndugu basi huulizana: “Mwenzangu mtala wako nani?” Kama ambavyo Wakurya hutumia milango, yaani familia za akina mama ambao ni wake wengi kwenye kaya yao kwa mume mmoja.
Wahehe wanatambuana kwa miiko, yaani mathalan ukikutana na Nganyagwa yoyote ambaye ndiye mara ya kwanza kabisa kuonana naye, basi ili ujue kama yeye na wewe ni wamoja, itabidi umhoji.
Basi utamuuliza: “Mwenzangu umesusa nini?” yaani ni kitu gani kwake ni mwiko kula, akitaja mwiko ule ule ambao ni wako, basi huyo ni ‘Mnyahuvi’ mwenzako. Akitaja mwiko mwingine, basi huyo mmefanana majina tu, lakini ukoo wenu si mmoja.
Naam, huo ndiyo uhondo wa kujitambua kijadi, nakuchagiza nawe ujitafute na kujitambua vyema.
Haya, tumeshapiga hodi kwa ndugu zetu Wakimbu, wenye mambo ya kuvutia kuyafahamu. Basi kwa kuanzia matembezi yetu kwao, haya tuliyoyaona leo yanatosha.
Tutaendelea tena na mambo yao kesho.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Februari 21, 2009.

Comments