Featured Post

ARUSHA JAZZ BAND NDIYO SIMBA WANYIKA!


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
KIZAZI cha sasa cha muziki hakiwezi kuelewa, lakini ukweli ni kwamba, bendi iliyojipatia umaarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki, Simba Wanyika, awali ilijulikana kama Arusha Jazz kabla ya kubadili jina.

Historia ni mwalimu mzuri, nami napenda historia, hivyo nitawamegea kidogo.
Wakati wanandugu Wilson na George Peter Kinyonga walipoachana na bendi ya Jamhuri Jazz ya Tanga walikwenda Arusha ambako walianzisha bendi hiyo ya Arusha Jazz mwaka 1971, wakiwa na ndugu yao mwingine William Peter Kinyonga.
Ukiangalia kwenye albamu  ya Simba Wanyika Greatest Hits Vol. 1, nyimbo kadhaa ambazo zimerekodiwa humo kwa jina la bendi ya Simba Wanyika, kama "Pamela," "Kenya Yetu," na "Marceline," awali zilikuwa zimerekodiwa chini ya jina la Arusha Jazz.
Sasa ilikuwaje hata wakajiita Simba Wanyika?
Mnamo mwezi Juni 1971, bendi hiyo ya Arusha Jazz iliyoundwa na wanandgu watatu ilihamia mjini Mombasa, Kenya na ikajipachika jina la utani wakijiita wao ni “Simba Wanyika” (Lions of the Wilderness).
Lakini huo haukuwa mwisho wa jina la "Arusha Jazz"
Mwandishi mashuhuri wa masuala ya muziki wa Afrika, Peter Toll, anasema, "Simba Wanyika ni jina ambalo wanandugu wa familia ya Kinyonga waliamua kulitumia baada ya kutoka Arusha na kuhamia Mombasa mwaka 1971 lakini waliendelea kulitumia jina la Arusha Jazz kwa muda.
“George alisema kwamba wakati walipoanza maisha mjini Mombasa walikuwa wakitumia mabango mawili kwenye maonyesho yao, moja likiwa na jina la 'Simba Wanyika,' na jingine 'Arusha Jazz.' Hata hivyo, inaonekana kwamba kuanzia mwaka 1973 waliamua kuachana kabisa na ‘Arusha Jazz’ na kutumia jjina la Simba Wanyika."
Long Player za mapema kabisa za bendi ya Arusha Jazz mwanzoni mwa miaka ya 1970 ni pamoja na Mama Suzie / Mary Mtoto (7" 45; Polydor POL 185); Tutengane Salama / Mama Niache (7" 45; Polydor POL 186); Eliza Wangu b/w Jose Twende Zaire (7" 45; Polydor POL 187) ilirekodiwa mwaka 1973.
Mnamo mwaka 1987, Wilson Peter Kinyonga alirekodia albamu akiishirikisha Arusha Jazz kwa kurekodi upya nyimbo za mwaka 1973 iliyokwenda kwa jina la Mama Suzie (Cassette; ASL [Nairobi] CASLP 2009).
Albamu hiyo iliyokuwa kwenye kaseti ilikuwa na nyimbo za Mama Suzie, Mary Mama, Bado Nakupenda, Eliza Wangu na Jose Twende Zaire.
Nyimbo nyingine zilikuwa Kwaheri Mpenzi, Sela Mbaa-Mbaa, Usinelewe Vibaya, Mbaya Wako Rafikiyo na Ewe Kijana.
Naamini tuko pamoja. Endelea kuperuzi MaendeleoVijijini ili kujua mengi zaidi.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.

Comments