Featured Post

UYUI WAZIPOKEA KWA MIKONO MIWILI MBEGU BORA ZILIZOFANYIWA UTAFITI KUTOKA COSTECH-OFAB

 Wanakikundi cha Upendo kilichopo Kijiji cha Magiri Kata ya Magiri katika Halmshauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora wakiwa pamoja na watafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha ARI-Maruku mkoani Kagera na Mwanahabari Coleta Makulwa wa RFA (wa pili kushoto), baada ya kukabidhiwa mbegu bora za Viazi lishe aina ya Kabode kwa ajili ya kuzipanda kwenye shamba darasa katika kata hiyo wilayani humo leo.
 Mbegu hizo zikiinuliwa juu baada ya kukabidhiwa.
 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, akimkabidhi mbegu za mihogo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Uyui, Hadija Makuwani kwa ajili ya kupanda katika shamba darasa katika Kijiji cha Isikizya wilayani humo. Wengine ni wakulima wa kijiji hicho.
 Wanakikundi cha Mapambano katika Kijiji cha Iberamilundi wakifurahi mbegu bora ya mihogo baada ya kukabidhiwa.
 Wakulima wa Kijiji cha Isikizya wakiwa kwenye uzinduzi wa shamba darasa.
 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, akizungumza na wakulima na wakulima wa Kijiji cha Isikizya (hawapo pichani). Kutoka kushoto ni Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange na Mtafiti kutoka COSTECH, Bestina Daniel.



 Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Uyui, Hadija Makuwani akizungumza na wakulima kabla ya kuzindua shamba darasa la mbegu ya mihogo katika Kijiji cha Isikizya.
 Wakulima wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Mkulima, Gervas Fungameza akiuliza swali.
 Mkulima Said Mirambo wa Kijiji cha Isikizya akiuliza swali.
 Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha ARI-Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akielekeza ubora wa mbegu ya mihogo aina ya mkombozi jinsi ya kuipanda
 Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, Hadija Makuwani akizindua shamba darasa hilo kwa kupanda mbegu ya mihogo.
 Diwani wa Kata ya Isikizya akipanda mbegu hiyo.
 Kaimu Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Uyui, Hamphrey Kilua akizungumza na wanakikundi cha Mapambano kabla ya kuzindua shamba la Viazi lishe katika Kijiji cha Iberamilundi.
 Wanakikundi cha Iberamilundi wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha ARI-Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akiwaelekeza wanakikundi cha Mapambano cha Kijiji cha Iberamilundi namna ya kupanda mbegu ya mihogo katika shamba darasa.
 Mwenyekiti wa kikundi hicho, Jumanne Said Mnubi akipanda mbegu hiyo.
 Katibu wa Kikundi hicho, Clementina Nyamizi akipanda mbegu katika shamba darasa.
Wanakikundi cha Upendo cha Kata ya Magiri wakiwa na mbegu zao mkononi za Viazi lishe

Na Dotto Mwaibale, Uyui Tabora

HALMASHAURI ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora imezipokea kwa mikono miwili mbegu bora za mahindi aina ya Wema, Viazi lishe na mihogo zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)

Mbegu hizo zimetolewa katika vijiji vitano vya wilaya hiyo kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa ambavyo vimetajwa kuwa ni kijiji cha Isikizya kilichopo Kata ya Isikizya ambacho kitakuwa na shamba darasa la zao la mihogo, Ibelamilundi ambacho pia zao lake ni mihogo, Kijiji cha Kigwa ambacho zao lake ni Viazi lishe, Igalula ambacho kitapandwa mahindi na Magiri ambacho kitakuwa na shamba darasa la zao la Viazi lishe.

Akizungumza wakati wa kupokea mbegu hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Hadija Makuwani alisema wao kama wilaya wamezipokea mbegu hizo kwa mikono miwili na watazifanyia kazi ili waweze kupata mazao yenye tija.

"Kwa kweli tunawashukuru sana COSTECH na OFAB kwa kutuletea mbegu hizi kwani tuna imani zitatuondelea changamoto ya kupata mazao machache kutokana na kutumia mbegu za kienyeji zilizozoeleka kwa wakulima wetu" alisema Makuwani.

Makuwani alisema hata yeye kwa kuwa ni mkulima anaomba apatiwe mbegu hizo ili akazipande kwenye shamba lake ili hapo baadaye nawe aweze kusambaza mbegu hiyo.


Diwani wa Kata ya Isikizya, Ally Mtelela alisema mbegu hizo zitazidisha ari kwa wakulima hao na wataondokana na kilimo kisicho na tija ambacho walikuwa wakitumia mbegu ambazo zilikuwa zikishambuliwa na magonjwa.

Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha ARI-Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura aliwaambia wakulima hao kuwa hekta moja ya mihogo iwapo watalipa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wataweza kupata tani 25 hadi 32 na kwa zao la viazilishe watapata tani 7 hadi 9 kwa hekta moja.

Alisema matokeo hayo watayapata endapo watafuata kanuni bora za kilimo cha mazao hayo kwa kuzingatia nafasi kati ya mche na mche na mstari kwa mstari na matumizi ya mbolea hivyo wataweza kuongeza uzalishaji zaidi tofauti na sasa ambapo kwenye hekta moja ya mihogo wanapata tani nane hadi kumi wakati kwenye Viazi lishe wanapata tani moja hadi tatu.

Kibura alisema Viazi lishe hivyo aina ya kabode vina vitamini A ambavyo ni muhimu kwa watoto kwa lishe na rangi yake ni vya njano na vinaisaidia serikali kuacha kutumia matone ya vitamini A badala yake mtu akivila anapata vitamini hiyo moja kwa moja.

Akizungumzia kuhusu mbegu Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, alisema mbegu hizo ya mihogo aina ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana ina uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa kama ya batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima na ya mahindi ikistahimili hali ya ukame na kutoa mazao mengi.

Mutagwa aliwaomba wakulima hao kuyatunza mashamba hayo ambayo yamegharimu fedha nyingi hadi kukamilika kwake hivyo wayaendeleze kwa ajili ya kuja kutoa matunda kwa wakulima wa wilaya hiyo na kupata chakula cha kutosha na ziada kuuza.

Mkulima Clementina Nyamizi wa Kijiji cha Iberamilundi ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Mapambano alisema wanaamini mbegu hizo zitawatoa katika umasikini na kuwa watazitunza na kuzilinda na wataachana kabisa na mbegu za kienyeji walizokuwa wakizitumia zamani.






Comments