Featured Post

SHIRIKA LA GLOBAL AFFAIRS CANADA LAZINDUA MIRADI MUHIMU TANZANIA


BMG Habari 
Shirika la Global Affairs Canada la nchini Canada limezindua miradi mitano ya afya nchini ikiwemo mradi wa Uzazi Uzima unaosimamiwa na Shirika la Amref Health Africa, lengo ikiwa ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto. 

 Akizungumza jana kwenye uzinduzi huo uliofanyika Jijini Dar es salaam, Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Ian Myles alisema miradi hiyo inagharimu zaidi ya Dola Milioni 6O ambapo mashirika mengine yanayosimamia miradi hiyo ni pamoja na Aga Khan International, Care International na World Vision. 
 Waziri wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu alieleza kufurahishwa na ushirikiano uliopo baina ya serikali na wadau wa maendeleo katika kutatua changamoto za afya ikiwemo vifo vya akina mama na watoto na kwamba analipa kipaumbele eneo la Mama na Mtoto kwani ni muhimu katika sekta hiyo. 
 Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Amref nchini Tanzania, Dkt.Florence Temu aliwashukuru wafadhili wa wa miradi hiyo kutoka nchini Canada na kubainisha kwamba ufadhili wao utasaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto hapa nchini. 
 Shirika la Amref linatekeleza mradi wake katika wilaya tano za mkoa wa Simiyu ambazo ni Meatu, Itilima, Bariadi, Maswa na Busega ambapo mradi huo umeanza mwaka huu na utafikia tamati mwaka 2020 huku mashirika mengine yakitekeleza miradi yake katika mikoa ya Mwanza, Tabora pamoja na Rukwa. 

Comments