Featured Post

SERIKALI YALIPA MADAI YA WALIOKUWA WAFANYAKAZI WA TTCL SH. BILIONI 12.7

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji 

Benny Mwaipaja, Dodoma
SERIKALI imewalipa pensheni wafanyakazi 245 wa iliyokuwa Kampuni ya Simu ya TTCL, chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kiasi cha shilingi bilioni 12.7.

Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Ludewa Mhe. Deogratias Ngalawa, aliyetaka kufahamu, lini Serikali ingewalipa wafanyakazi wa TTCL wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki madai ya pensheni yao.
Dkt. Kijaji alisema kuwa malipo hayo yamefanyika kwa wafanyakazi 245 ambao wamelipwa fedha zao kwa mkupuo ambapo kati yao wastaafu 54 walifariki dunia na malipo yao kulipwa warithi wao.
“Wastaafu 198 wanaendelea kulipwa malipo ya nyongeza ya pensheni ya kila mwezi” alisema Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa malipo hayo yanafuatia uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi namba 69/2005 ambapo wafanyakazi hao 254 waliishitaki Serikali kupinga uamuzi wa kusitisha mfuko uliojulikana kama East Africa Non Contributory Pension Scheme.
 “Katika Shauri hilo, Mahakama Kuu iliamua kuwa, uamuzi wa Serikali kusitisha mfuko huo haukuwa sahihi kisheria na hivyo kuamua wafanyakazi 254 waliokuwa katika shauri hilo walipwe madai yao ambayo yalijumuisha malipo ya mkupuo, riba pamoja na pensheni yao ya kila mwezi” aliongeza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa baada ya uamuzi huo wafanyakazi wengine 324 nao walifungua kesi Makahama Kuu wakitaka walipwe pensheni kama wenzao walivyolipwa wakati hawakuwa sehemu ya wafanyakazi waliofungua na kushinda kesi hapo awali.
“Mahakama Kuu iliamua kuwa, wafanyakazi waliofungua kesi ya awali ndio walipwe madai yao, na kwamba deed of settlement iliyosajiliwa Mahakamani ilihusisha wafanyakazi hao pekee” alifafanua Dkt. Kijaji.
Alisema wafanyakazi wengine ambao hawakuwa sehemu ya kesi hiyo hawawezi kulipwa kwa kutumia hukumu na tuzo ya kesi ambayo hawakuwa sehemu yake na kusisitiza kuwa, Serikali haiwezi kulipa madai mengine ambayo hayakuthibitika kisheria.

Comments