Featured Post

KIPEPEO: HUJIBADILISHA ASILIWE NA WADUDU

JAMII kadhaa za vipepeo wana uwezo wa kujigeuza na kujifanya waonekane kama ni wa jamii nyingine.
Jamii za vipepeo wa aina hii ni Batesian na Mullerian ambao wanajibadilisha na kujifanya ni wa jamii nyingine ili kupata faida kadhaa ikiwemo ulinzi, kwani jamii wanazojifananisha nazo zinaogopwa kwa kiasi fulani na wadudu na ndege wanaoweza kuwala.

Mathalan, wadudu wengi na ndege hawapendi kuwala vipepeo wa jamii ya Common Rose na Crimson Rose kwa sababu ya ladha yao mbaya.
Kwahiyo, vipepeo wa jamii nyingine, hasa Common Mormon majike ambao hupatikana zaidi huko India, hupenda kujigeuza kuonekana kama jamii hizo ili kukwepa kuliwa na wadudu wengine au ndege.
Jamii ya Mullerian wanapenda kujionyesha kama Aposematic kwa lengo lile lile la kuwahadaa maadui zao.
Jamii nyingine yenye sifa hii ya kujifananisha na jamii nyingine ni Heliconius inayopatikana zaidi huko Marekani.
Baadhi ya vipepeo wana michoro inayofanana na macho katika mabawa yao. Michoro hii ni moja ya vitu ambavyo vipepeo wanavitumia kujifananisha na jamii nyingine.
Katika jamii nyingine, hutumia sauti za mawasiliano kama njia ya kujifananisha na jamii tofauti na za kwao.
Wengi hutumia sauti wanazozitoa wakati wanapokuwa tayari kujamiiana.
Lakini wataalam bado hawajaweza kuthibitisha moja kwa moja kazi kuu ya michoro hii inayofanana na macho katika mabawa ya vipepeo.

Mabadiliko kwa msimu
Jamii nyingi za vipepeo katika maeneo ya Tropiki zinajibadilisha kulingana na msimu ambapo mabadiliko yao yanatokana na mabadiliko ya misimu ya hali ya hewa.
Mara nyingi mabadiliko haya huendana na misimu ya mvua, hivyo kuna mabadiliko wakati wa kiangazi na wakati wa masika.
Hata hivyo, ni jinsi gani vipepeo wanajibadilisha kulingana na msimu, ni jambo ambalo halijaweza kubainika wazi.
Kwa mujibu wa tafiti kwa kutumia kemikali, mabadiliko yanayotokea wakati wa kiangazi ni ya ajabu na inadhaniwa kuwa mabadiliko hayo yanamwezesha kipepeo kuhimilia mabadiliko ya hali ya hewa.
Baadhi ya vipepeo hupata rangi nzito nyeusi wakati wa masika. Inaaminika rangi hii huwasaidia kufyonza na kuhifadhi joto kutoka kwenye jua, kwani nafahamika kuwa rangi nyeusi inahifadhi joto kwa wingi.
Vipepeo jamii ya Bicyclus anynana ni moja ya jamii za vipepeo ambao huonyesha mabadiliko ya msimu.
Jamii hii ambayo hupatikana kwa wingi barani Afrika wana mabadiliko makubwa mawili kulingana na msimu.
Wakati wa masika, jamii hii huwa na alama za macho makubwa zinazong’aa lakini wakati wa kiangazi wanakuwa na alama za macho madogo sana ambazo ni vigumu kuziona kwa urahisi. Wakati mwingine alama hizo hupotea kabisa.
Lava wa jamii hii wanaokua katika mazingira ya joto kali na unyevunyevu wa masika, wanakua na kuwa na sifa za vipepeo wa msimu wa masika wakati wale wanaokua wakati wa kipindi cha kiangazi wanakuwa na sifa za vipepeo wa msimu wa kiangazi pale wanapopevuka.
Mabadiliko haya yanayohusu alama za macho yanawasaidia sana vipepeo hawa kuendesha maisha yao kirahisi kulingana na msimu. Mathalan, wakati wa msimu wa kiangazi, vipepeo hawa wanaishi katika majani makavu ambayo hayahitaji sana kuwa na alama hizo.
Kwa kutokuwa na alama hizi wakati wa kiangazi, wanaweza kujificha kwa urahisi katika majani makavu.
Hii inawasaidia kujilinda dhidi ya maadui. Wakati wa masika vipepeo hawa ambao aghalabu huwa na rangi ya kahawia, wanakuwa hawana namna nzuri ya kujificha kwa kutumia rangi zao kwa sababu majani wakati huu yanakuwa na rangi ya kijani.
Kwahiyo, alama za macho zinazotokea wakati huu huongeza rangi zao na kuwawezesha kuendelea kujichanganya na mazingira bila kugundulika kwa wepesi.

Tabia
Chakula kikuu cha kipepeo ni nekta kutoka katika maua. Baadhi ya jamii pia hula poleni kutoka katika maua pia.
Wengine hula majimaji kutoka katika magamba ya miti, matunda yanayooza, vinyesi na takataka nyingine.
Kutokana na hali hii ya kujitafutia chakula kutoka kwenye maua, kipepeo anafanya jambo moja kubwa la kusaidia kusafirisha poleni kutoka ua moja hadi jingine hivyo kusaidia kazi ya uchavushaji (uzalishaji) ingawa vipepeo hawabebi poleni nyingi kama walivyo wadudu wengine hususan nyuki, lakini wana sifa ya uwezo wa kusafirisha poleni katika masafa marefu kuliko wadudu wengine.
Wanapopevuka, vipepeo hula chakula katika hali ya majimaji tu ambayo huyafyonza kupitia mirija inayojulikana kitaalam kama Proboscis.
Kama ilivyoelezwa, vipepeo wanategemea zaidi nekta lakini pia hufyonza majimaji mengine kutoka sehemu yoyote wanayoweza kuyapata.
Kupitia majimaji hayo, vipepeo hujipatia maji na sukari ambayo huwaongezea nguvu na madini kama Sodium na mengineyo na kuwasaidia sana kuzaana.
Jamii kadhaa za vipepeo wanahitaji
Sodium kwa wingi kwa ajili ya kuzaana. Jamii nyingine huhitaji sodium nyingi kuliko ile wanayoweza kuipata kwenye nekta.
Ili kutafuta sodium hii ya ziada, vipepeo wanavutiwa na vitu vyenye chumvichumvi na matokeo yake wanajikuta wakati mwingine wakitua katika miili ya binadamu inayokuwa na chumvi kutokana na jasho.
Pamoja na kutembelea sehemu zenye majimaji, lakini inafahamika pia vipepeo hujipatia chakula hasa madini katika vinyesi vya wanyama, matunda yanayooza na mizoga lakini katika jamii nyingi za vipepeo ni madume tu ndio wanaokuwa na tabia ya kujipatia chakula kutoka kwenye vinyesi.
Tafiti zinaonyesha kuwa madume hutumia madini haya wanayoyapata kutoka kwenye vinyesi na vitu vingine kama zawadi kwa wapenzi wao wakati wa kujamiiana.
Hii ndiyo maana majike hawajihangaishi katika vinyesi na mizoga, wanajua tu kuwa watajipatia madini haya kutoka kwa wapenzi wao.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656331974.


Comments