Featured Post

KATIBA YA CHAMA CHA WADAU WA KUKU TANZANIA (PAT) YAPITISHWA

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria mkutano wa kupitisha rasimu ya tatu ya Katiba ya Chama cha Wadau wa Sekta ya Kuku Tanzania (PAT). 

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
JUMLA ya wajumbe 22 kutoka vyama 11 wamepitisha kwa kauli moja rasimu ya tatu na ya mwisho ya Katiba ya Chama cha Wadau wa Kuku Tanzania (Poultry Association of Tanzania – PAT) katika kikao kilichofanyika kwenye Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam, jana Jumatano, Novemba 29, 2017.

Kupitishwa kwa Katiba hiyo kumehitimisha mchakato wa takriban miaka 20 wa kuunda umoja huo wa wafugaji kuku nchini ili kuirasmisha sekta hiyo ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa pato la jamii pamoja na taifa.
Wajumbe waliopitisha rasimu hiyo wametoka katika vyama vya Arusha Poultry Keepers Association (APOKA), Tanzania Animal Feeds Manufactures (TAFMA), Tanzania Poultry Breeders Association (TPBA), Tanzania Commercial Poultry Association (TCPA), na African Women Agro- Network (Awan Tanzania Chapter).
Vyama vingine ni Umoja wa Wafugaji Kuku Dar es Salaam (UFUKUDA), Tanzania Veterinary Para Professionals (TAVEPA), Ushirika wa kufuga Kuku Morogoro (UWAFUKUMO), Tanzania Layer Farmers Association (TALFA), Tanzania Broiler  Farmers Association (TABROFA), na Kisutu Poultry Co-operative Society (KIPOCOSO).
Ni chama cha Mwanza Multipurpose Cooperative Society Limited pekee ambacho hakikuhudhuria mkutano huo ingawa katika taarifa yake kilieleza kuunga mkono hatua ambazo zingefikiwa.
Mbali ya kupitisha rasimu ya katiba hiyo, lakini wajumbe wa mkutano huo walichagua uongozi wa muda utakaokuwa chini ya uenyekiti wa Harko Bhagat, ambao pamoja na mambo mengine, utashughulikia usajili wa chama pamoja na kuweka mpango mkakati kwa ajili ya utekelezaji.
Katibu wa muda wa PAT, Manase Mrindwa, aliwaahidi wajumbe kwamba, marekebisho ya mwisho yaliyopitishwa na mkutano huo yatafanyiwa kazi na hatua za usajili zitaanza mara moja.
“Tumeanza mchakato huu tangu mwaka 1995, tunashukuru kwamba tumefika mahali tumekikamilisha kitu ambacho tumekuwa tukikililia usiku na mchana,” alisema Mrindwa.
Mwenyekiti wa mkutano huo, Sufian Kyarua, aliwapongeza wajumbe wote waliohudhuria na kufikia makubalino akisema hiyo imeonyesha mshikamano na nia ya dhati waliyonayo katika kuendeleza sekta ya ufugaji wa kuku nchini Tanzania.
Kyarua alisema kwamba, PAT ni chama mwamvuli wa vyama mbalimbali vinavyohusika na tasnia ya kuku Tanzania, na kwamba chenyewe siyo cha kibiashara wala hakifungamani na itikadi zozote za kisiasa, kidini au kijamii.
“Jukumu mojawapo la PAT, kama tulivyoona kwenye katiba yetu, ni kuwaunganisha wanachama wake pamoja na kuwapatia taarifa mbalimbali za masoko,” alisema.
Awali, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, mgeni rasmi kutoka Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Ezekiel Maro, aliwataka wajumbe hao kuunda chama ambacho hakitakuwa cha kiharakati wala kisiasa, bali kiwaunganishe wadau wa tasnia ya kuku kwa nia ya kuwaendeleza na siyo vinginevyo.
“Kama mtaanzisha kwa mtazamo wa kisiasa au kibiashara, huko mbele mtakwama, lakini mkianzisha kwa kuangalia maslahi ya wanachama wenu bila kuleta harakati mtafanikiwa,” alisema Maro, Ofisa Mifugo wa TMB ambaye anahusika na Usajili wa Wadau wa Tasnia ya Nyama Tanzania.
Maro alisema kwamba, ni vyema wakaweka kumbukumbu za kitakwimu katika shughuli zao ambazo ndizo zitakazowaongoza katika kujiletea maendeleo.
“Hivi sasa ni wakati wa soko huria, serikali inajitahidi kulinda bidhaa za ndani pamoja na wananchi wake kwa kutoruhusu kuingiza kwa wingi bidhaa za nje, lakini hili litawezekana ikiwa kutakuwa na takwimu sahihi kwa sababu mwisho wa siku takwimu ndizo zitakazoongea.

“Huwezi kusema vyakula vya mifugo kutoka nje visiingizwe wakati hatujui takwimu halisi za mahitaji pamoja na uzalishaji, lakini kama takwimu ziko sawa, basi hata kama italazimu kuruhusu bidhaa za nje itakuwa ni kwa kujazia pengo lililopo,” alisema.

Comments