Featured Post

WATUMIA MACHELA KUBEBA WAGONJWA


Na Mwandishi Wetu, Kilolo
ZAIDI ya wakazi 40,000 wa kata tano wilayani Kilolo wanalazimika kutembea umbali mrefu huku wengine wakiwabeba wagonjwa kwa kutumia machela ili kuwafikisha kwenye vituo vya afya.

Uchunguzi uliofanywa umeonyesha kwamba, wananchi wa Kijiji cha Makungu kilichopo Kata ya Ukwega, yenye wakazi 12,195, wilayani humo wanalazimika kuwabeba wagonjwa kwa kutumia machela kwa zaidi ya kilometa 15 kuwafikisha kwenye zahanati iliyopo Kijiji cha Ipalamwa.
“Changamoto hii imegharimu uhai wa wenzetu waliopoteza maisha kabla ya kufika zahanati au vituo vya afya huku wajawazito wakilazimika kuhama makazi yao kwa mwezi mzima ili kusogea jirani na huduma za afya hasa Hospitali Teule ya Ilula iliyopo umbali wa kilometa 60,” alisema Brown Kikoti, mkazi wa kijiji hicho. 
Kikoti alisema, wananchi wasio na uwezo hutumia zahanati ya Isagwa iliyopo umbali wa kilometa 10 kutoka kijijini hapo, ambako hata hivyo, hakuna huduma za uhakika.
Fredy Nyaulingo alisema wenye magari wamekuwa wakiwatoza Shs. 280,000 ili kuwapeleka wagonjwa katika Hospitali Teule ya Ilula, kiwango ambacho wananchi wengi wanashindwa kukimudu.
Alisema hali hiyo inasababisha wananchi wengi kutumia miti shamba katika kujitibu, huku wajawazito wakijifungulia njiani baada ya kuanza kuumwa uchungu kabla ya siku walizokadiriwa kujifungua kufika.
“Tatizo hili la kukosekana kwa usafiri na umbali wa huduma ya afya linasababisha wajawazito kujifungulia njiani, wengine wamekuwa wakipoteza watoto,” alisema Nyaulingo.
Japhet Mlwale, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Makungu, alisema ubovu wa barabara ni sababu kubwa ya magari kushindwa kufika kijijini hapo hasa kutokana na jiografia ya eneo hilo kuwa lenye milima mikali na mabonde, huku msimu wa mvua kukiwa na utelezi.
“Barabara zetu kama mlivyoziona ni hatari, hazina matengenezo yoyote, kwani zingekuwa zinapitika wenye magari wangeweza kuleta usafiri, lakini wanahofia hali ya usalama hasa msimu wa mvua,” alisema Mlwale.
Wakati hali ikiwa hivyo katika kijiji hicho, wananchi wa kata za Kimala, Idete na Masisiwe nao wanakabiliwa na changamoto za aina hiyo kutokana na kukosekana kwa usafiri kunakosababishwa na ubovu wa barabara.
Eliya Nyamoga, mkazi wa Kimala wilayani humo, alisema ili kumfikisha mgonjwa kwenye Kituo cha Afya cha Kidabaga ni lazima mwananchi achangie Shs. 70,000 ‘za mafuta’ kwa gari la kituo hicho, ambazo hata hivyo hazikatiwi stakabadhi.
“Usipotoa fedha hizi hawawezi kumbeba mgonjwa, sasa kwa wananchi wa kawaida wanaotegemea zaidi kilimo watapata wapi fedha hizo?” alihoji.
Herieth Paschal Mponzi, mkazi wa Masisiwe, alisema ukosefu wa barabara unawanyima fursa muhimu ya usafiri ambapo inapotokea mgonjwa amezidiwa, hulazimika kukodi gari kutoka Kituo cha Afya Kidabaga kwa kiasi cha Shs. 80,000.
Kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2012, Kata ya Ukwega ina wakazi 12,195, Kata ya Idete ina wakazi 8,059, Kata ya Masisiwe ina wakazi 10,053 na Kimala ina wakazi 7,649, ambapo maeneo yote yanakabiliwa na changamoto hizo za usafiri na huduma za afya.
Taarifa kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilolo zinasema, wilaya hiyo ina jumla ya zahanati 50 tu kati ya vijiji 106 vilivyopo, huku vituo vya afya vikiwa viwili na hospitali teule moja ambayo ipo chini ya shirika la dini.
Inaelezwa kwamba vijiji vingi wilayani humo vinaonja adha ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu ya afya na akasema wilaya ina magari mawili tu ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ambapo moja ni la Kituo cha Afya Kidabaga na lingine la Hospitali Teule ya Ilula.
“Kweli wilaya yetu ina upungufu mkubwa wa vituo vya tiba, mfano katika tarafa nzima ya Kilolo hakuna kituo hata kimoja cha afya, tatizo hili linasababisha wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo, lakini hata upande wa usafiri pia tuna changamoto, kwani tuna magari mawili pekee ya kubeba wagonjwa,” zimesema taarifa hizo.

Imetayarishwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.

Comments