Featured Post

WANANCHI WANA MAMLAKA KATIKA TATHMINI YA ARDHI YA VIJIJI

MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI YA KIJIJI - 2
Mikutano kama hii ya kijiji ni muhimu kwa wananchi kutolea uamuzi masuala mbalimbali yakiwemo ya matumizi bora ya ardhi ya kijiji.


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
MIGOGORO mingi katika jamii hutokana na wananchi kutokushirikishwa katika uamuzi hata wa miradi ya maendeleo kuanzia mwanzo.

Kwa kutambua hilo, ndiyo maana NLUPC imeweka utaratibu kwamba, suala zima la kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi ni lazima iwashirikishe wananchi wenyewe na wao ndio waridhie na kukubaliana kwa pamoja.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, timu ya PLUM hutembelea vijiji vilivyochaguliwa ili kuwezesha Ushirikishwaji katika Tathmini ya Vijiji (PRA) inayolenga matumizi ya ardhi.
PLUM, kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama Halmashauri ya Kijiji, Mkutano wa Kijiji, Vitongoji na kadhalika, huchambua na kutathmini matatizo na fursa za utatuzi katika matumizi ya ardhi.
Kwa kawaida, MaendeleoVijijini inatambua kwamba, taasisi hizo zinapaswa kuwepo kijijini na kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 7 ya mwaka 1982.
Tangu mwanzo, timu ya PLUM inapaswa kuhakikisha kuwa taasisi hizo zipo na zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria, vinginevyo zijengwe na ziendelezwe kufanya hivyo.
Kutokowepo kwa taasisi hizo, uchunguzi wa MaendeleoVijijini unaonyesha kuwa, huchangia kuwepo kwa migogoro mingi ya ardhi na hata kudumaa kwa maendeleo.
Mara nyingi ufanisi wa taasisi hizo, hususan mafanikio ya mikutano halali ndiyo yanayozaa tathmini nzuri inayoeleza matatizo na fursa za utatuzi.
Vilevile mikutano hiyo katika ngazi za mashamba, vitalu, vitongoji na kijiji ndiyo hutoa mipango ya matumizi bora ya ardhi inayoeleweka na kukubalika katika jamii husika.
Kama kuna tathmini shirikishi ya kijiji iliyokwishafanyika awali na sekta yoyote, hususan ya matumizi ya rasilimali au maendeleo vijijini inaweza kutumika kurejewa kwenda na wakati badala ya kuanza upya.
Wawezeshaji wanapaswa kuwa makini kuhakikisha kuwa jamii katika ngazi husika wanachambua matatizo, fursa za utatuzi, na kuweka vipaumbele kwa kuhusisha tatizo, chanzo chake na athari.
Mfano mzuri ni kwamba, baa la njaa linaweza kutokana na uzalishaji duni unaotokana na ukame na uharibifu wa ardhi ambao unaweza kuwa ni matokeo ya ufyekaji miti na usimamizi mbaya wa ardhi.
Hiyo inaweza kuchangiwa pia na kuwepo migogoro ya mipaka na miliki na kutokuwa na usalama wa miliki.
Uchambuzi wa namna hiyo ni muhimu na unwasaidia wanakijiji kulinganisha kati ya kushughulikia matatizo ya ufumbuzi wa papo na yale yanayohitaji upangaji wa muda wa kati au muda mrefu.
Vilevile ni muhimu kwa wanakijiji kuelewa kuwa uwekezaji unaohitaji kwenye sekta za huduma kama elimu na afya unatoka katika sekta ya uzalishaji.
Katika uchambuzi wa fursa, shughuli zinazohitaji msaada wa nje ya kijiji na nje ya majukumu ya timu ya PLUM zinaweza kurejewa kwa taasisi husika ndani na hata nje ya wilaya.

Mpango wa Utendaji Jumuiya
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, matokeo ya kazi ya PRA ni kuwa na mpango wa utendaji wa jumuiya unaolenga kwenye usimamizi wa matumizi bora ya ardhi (CAP).
Mpango kazi huo, ambao siyo mpango wa matumizi ya ardhi, utaandaliwa kutokana na mpango katika ‘Hatua ya 4’ ya PLUM ambapo utaweka bayana vipaumbele vya fursa za maendeleo, kazi zilizopendekezwa na mahitaji, kazi na majukumu ya watu binafsi na vikundi, ratiba ya kazi, uhusishaji wa miradi ya kijiji, wilaya na taifa, na maeneo yanayohitaji msaada kutoka nje.

Ujenzi na uimarishaji wa taasisi za vijiji
Ufanisi wa kazi zilizoainishwa unategemea zaidi kuwepo kwa taasisi imara katika ngazi ya kijiji na vitongoji vyake.
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) huendesha mafunzo mbalimbali kutokana na program ya maboresho ya Utawala Bora, kujenga uwezo katika taasisi ngazi ya kijiji, hususan Mkutano wa Kijiji na Halmashauri ya Kijiji.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, kifungu cha 55 cha Sheria ya Serikali za Mitaa kinaweka utaratibu wa kila kijiji kuwa na Mkutano wa Kijiji ambao ni mkutano wa wanakijiji wote wenye miaka 18 na kuendelea.
Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 katika Fungu la 8 Ibara ya 5, inaelekeza Halmashauri ya Kijiji kutogawa ardhi au kutoa hatimiliki ya haki za kimila za ardhi bila kwanza kupata kibali cha Mkutano wa Kijiji.
Vilevile katika Ibara ya 6, Sheria inaelekeza Halmashauri ya Kijiji kutoa taarifa katika Mkutano wa Kijiji na kuzingatia maoni ya Mkutano wa Kijiji kuhusiana na mambo yote ya usimamizi na utawala wa ardhi ya kijiji.

Mkutano wa Kijiji
Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Kifungu cha 103 kinaainisha mikutano ifuatayo inayohusu Mkutano wa Kijiji; Mosi, Kutaitishwa Mkutano wa Kijiji kila inapobidi kufanya uchaguzi na/au kuunda Halmshauri ya Kijiji na kuchagua wajumbe wake.
Pili, Kutafanyika mkutano wa kawaida wa kijiji angalau mara moja katika kila miezi mitatu; Tatu, Halmashauri ya Kijiji inaweza, ikiwa itaona lazima au inafaa kwa sababu yoyote ile kufanya hivyo, kuitisha mkutano usio wa kwaida wa kijiji, kujadili na kuamua juu ya suala lolote lenye manufaa kwa umma.
Kwa kawaida, katika usimamizi na utawala wa ardhi ya kijiji, Mkutano wa Kijiji hutoa uamuzi kwenye masuala ambayo yana umuhimu wa pekee kwenye jamii.
Hiyo ni pamoja na kuidhinisha mipango ya matumizi bora ya ardhi ya kijiji, ugawaji wa ardhi, upitishaji wa sheria ndogo za usimamizi wa matumizi ya ardhi, uundaji wa kamati za kusimamia matumizi ya ardhi, kuidhinisha Baraza la Ardhi la Kijiji na kamati za mazingira.
Uzoefu unaonyesha kwamba, mikutano ya kijiji ina manufaa makubwa katika kuiarifu jamii ya kijiji, kutoa maelezo kuhusu usimamizi wa ardhi, na kupata ridhaa ya wanakijiji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usimamizi wa ardhi.
Ni wakati wa mikutano hiyo ambapo wanakijiji binafsi, ambao siyo wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji au Kamati ya Usimamizi wa Ardhi, wanaweza kushiriki, kuchangia na kushawishi uamuzi kwenye ngazi ya kijiji.

Halmashauri ya Kijiji
Halmashauri ya Kijiji inaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 56 cha Sheria ya Serikali za Mitaa ambapo idadi ya wajumbe hutegemea ukubwa wa kijiji na idadi ya vitongoji katika kijiji husika, lakini ni lazima wasipungue 15 na wasizidi 25.
Kisheria, halmashauri za wilaya zimepewa mamlaka ya kupokea mapendekezo ya vijiji, na kutoa uamuzi juu ya idadi ya vitongoji na wajumbe wa Halmashauri ya kila Kijiji.
Wajumbe hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji ambaye huchaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji, wenyeviti wa vitongoji ndani ya kijiji, na wajumbe wengine wanaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Ili kuleta usawa wa jinsia, sheria inaagiza kwamba, ni lazima idadi ya wanawake katika Halmashauri ya Kijiji isipungue robo ya wajumbe wote.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji (Village Executive Officer – VEO) ambaye huajiriwa na Halmashauri ya Wilaya huwa Katibu wa Halmashauri ya Kijiji na Mkutano wa Kijiji.
Halmashauri ya Kijiji inayo madaraka ya utendaji ya kufanya uamuzi au mapendekezo ya kila siku ya usimamizi wa kijiji ikiwemo ardhi ya kijiji.
Katika kusimamia ardhi, Halmashauri ya Kijiji inaweza kutayarisha mapendekezo ya mipango ya matumizi bora ya ardhi ya kijiji, sheria ndogo, mikataba ya pamoja ya matumizi ya ardhi, kugawa ardhi, kutoa hatimiliki za haki za ardhi za kimila, kuunda kamati mbalimbali kuhusiana na matumizi ya ardhi, na baadaye kuwasilisha kwenye Mkutano wa Kijiji ambao una madaraka ya kuidhinisha au kukataa mapendekezo ya Halmashauri ya Kijiji.

Mkutano wa Halmashauri ya Kijiji
Ili mkutano wa Halmashauri ya Kijiji ufanikiwe, hakuna budi wajumbe waarifiwe mapema, kwa maandishi, kwa kuonyesha dondoo zitakazojadiliwa, na siyo kutangaza kwa baragumu tena kwa muda mfupi bila kuwaeleza wajumbe nini kitakachojadiliwa.
Halmashauri ya Kijiji hukutana wakati wowote inapoona lazima, lakini kama ilivyoelezwa awali, isiwe chini ya mara nne kwa mwaka (kila baada ya miezi mitatu) ili kuweza kuandaa agenda na mapendekezo ya kujadiliwa na Mkutano wa Kijiji.
Akidi ni angalau nusu ya wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji lazima wawepo wakati wote wa mkutano, kinyume chake uamuzi wowote utakaofanywa wakati wa mkutano huo hautatambuliwa kisheria.
Mkutano huo ni lazima uhudhuriwe na kufunguliwa na Mwenyekiti (au Kaimu wake) ambaye ndiye anayehusika na agenda na Katibu (Ofisa Mtendaji wa Kijiji) ambaye anahusika na kumbukumbu za mkutano.
Ni lazima kumbukumbu za mkutano uliotangulia zisomwe na kuthibitishwa na wajumbe na kutiwa saini na Mwenyekiti na Katibu kabla ya kuendelea na agenda nyingine.
Vilevile, yatokanayo na mkutano uliotangulia pia ni lazima yajadiliwe.
Mawazo ya agenda nyingine kama zilivyoonyeshwa kwenye barua ya mwaliko, pamoja na taarifa kutoka kwenye kamati zilizoundwa na Halmashauri zijadiliwe, halafu kuna mengineyo na hatimaye Mwenyekiti atafunga mkutano.

Umuhimu wa Mikutano
Ni vyema kusisitiza umuhimu wa kuwepo mikutano, kwani maeneo mengi yenye migogoro ya ardhi yamechangiwa na kupuuzwa na kutofuata taratibu za mikutano.
Katika vijiji vingi, uzoefu unaonyesha kwamba, uamuzi unaopaswa kutolewa na Halmashauri ya Kijiji, umekuwa ukitolewa na mtu mmoja tu (Mwenyekiti au Katibu) na kuchukuliwa kama ndio uamuzi wa Halmashauri ya Kijiji.
Baadhi ya watu huona mikutano inapoteza muda au kuchelewesha uamuzi, lakini mara nyingi kutokuhudhuria kwao kumekuwa na athari kwa sababu hao hao wasiohudhuria ndio wakati mwingine huanzisha migogoro kwa kuona kwamba uamuzi uliopitishwa kwenye mikutano husika haukuzingatia baadhi ya mambo ambayo kama wangehudhuria wangeweza kupendekeza.
Mfano mzuri ni katika Kijiji cha Sero huko Loliondo wilayani Ngorongoro ambako Mkutano wa Kijiji wa kugawa ardhi ulisainiwa na majina ya watu ambao baadhi ya wanakijiji walidai hawawajui kijijini mwao, hali iliyosababisha mgogoro mkubwa.
Aidha, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mzula wilayani Dodoma aliwahi kuwasilisha kwenye mkutano wa kijiji, kwa niaba ya Halmashauri ya Kijiji, majina ya watu wa kuunda Kamati ya Usimamizi wa Ardhi ya Kijiji, lakini wanakijiji wakachachamaa kuwa majina yote ni marafiki wa karibu au jamaa wa Mwenyekiti.
Ilibainika pia kwamba, Halmashauri ya Kijiji haikuwahi kukutana na kupendekeza majina hayo.
Hiyo ni baadhi tu ya mifano michache ambayo inapaswa kutoa tahadhari wakati taasisi za vijiji zinaposhughulikia masuala nyeti yenye maslahi makubwa ya jamii, kama ardhi.
Watu wachache wasipewe fursa kutumia vibaya mamlaka ambayo Sheria inatoa kwa taasisi za kijiji kushughulikia ardhi.

Mafanikio ya Mikutano
Ushirikishwaji katika mipango na usimamizi wa ardhi (PLUM) umejenga mhimili wake katika majadiliano na hatimaye kufikia makubaliano.
Wakati wote wa mkutano katika ngazi mbalimbali – kuanzia kaya, jamii, kitongoji, kamati, halmashauri, mkutano – wawezeshaji (wataalam kutoka nje ya kijiji) ni lazima wajiulize:
* Mahudhurio ya watu wa aina mbalimbali za kiuchumi jamii, walemavu, wazee, vijana, wanaume na wanawake yakoje?
* Kwa kiwango gani aina mbalimbali za kiuchumi-jamii, wanaume na wanawake wanachangia wakati wa majadiliano?
* Je, masuala yanaeleweka vizuri?
* Je, watu na kila aina ya watumiaji wa ardhi wanawasilisha vizuri matilaba na mapendekezo yao?
* Je, kuna mjadala na uchambuzi wa pamoja unaopelekea kwenye mipango ya utendajji na uhamasishaji wa washiriki?
* Je, wanakijiji wanafikia makubaliano ya bayana na mipango inayoakisi vipaumbele vya jamii (wanaume, wanawake, vijana) katika njia ya usawa na haki?
* Je, makubaliano na mipango inatarajiwa kuleta mafanikio?
* Je, hadidu za rejea zinaandikwa vizuri, kutayarishwa na kusambazwa katika muda unaotakiwa?
Wakati mkutano wa usimamizi wa ardhi kijijini unapokuwa hauna mafanikio mazuri kuliko ilivyotarajiwa, na moja au zaidi ya maswali hayo hayakujibiwa kwa usahihi, hatua za kurekebisha lazima zichukuliwe ili kuboresha utendaji katika mikutano inayofuata.
Marekebisho ya mikutano inayofuata yafanywe kwa kushauri Halmashauri ya Kijiji kurekebisha kasoro za mkutano uliotangulia.

Kesho tutaangalia namna kushughulikia mipaka ya ardhi ya kijiji.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974


Comments