Featured Post

USHIRIKISHWAJI KATIKA MIPANGO NA USIMAMIZI WA MATUMIZI BORA YA ARDHI VIJIJINI NI MUHIMU

MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI YA KIJIJI - 1
Wananchi wa jamii ya Kimasai wakiangalia mchoro wa ardhi wa upangaji wa ardhi ya kijiji chao.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
SUALA la matumizi bora ya ardhi limekuwa na changamoto kubwa vijijini ambapo ardhi imekuwa chanzo cha migogoro mingi kwa jamii mbalimbali.
MaendeleVijijini inatambua kwamba, migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji imesababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya Watanzania na bado kuna kila dalili za migogoro hiyo kuibuka katika mahali pengi nchini.

Lakini pia kumekuwa na migogoro ya ardhi baina ya wanavijiji na wawekezaji ambao wamehodhi maeneo makubwa ya ardhi baada ya kuuziwa na Serikali Kuu kupitia mashirika au Kituo cha Taifa cha Uwekezaji.
Ukiachana na hilo, wanavijiji wenyewe nao wamekuwa wakiuza ardhi yao kwa watu binafsi kwa nia ya kupata fedha huku serikali za vijiji nazo zikituhumiwa kuuza akiba ya ardhi ya kijiji, hali ambayo imefanya vijiji vingi leo hii kukosa hata ardhi kwa ajili ya huduma za jamii kama ujenzi wa shule, zahanati au hata makaburi.
MaendeleoVijijini imeshuhudia vijiji vingi katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa vikiwa havina ardhi, jambo ambalo ni la hatari hasa kutokana na ongezeko la idadi ya watu.
Hivi sasa wakati Serikali imekwishaweka utaratibu wa utoaji wa hati miliki za kimila za ardhi kwa kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA), ndipo wananchi wengi wanazinduka na kuona kwamba kumbe wanaweza kuyarasimisha mashamba yao na kupata hati miliki ambazo wanaweza kuzitumia hata kukopa mitaji katika taasisi za fedha.
Katika kutekeleza malengo ya MKURABITA, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi (NLUPC) ilitoa mwongozo wa utekelezaji kwa kuanza kupima ardhi za vijiji kwa kuzingatia Sheria Namba 5 ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, lengo likiwa kutekeleza misingi ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995.
Sera ya Taifa ya Ardhi inaelekeza, pamoja na mambo mengine, kwamba upangaji wa matumizi ya ardhi ufanyike kwa mfumo wa ushirikishwaji kwa kuwahusisha walengwa.
Utaratibu huu unapotumika maana yake unaondoa kwa kiasi kikubwa uwepo wa migogoro ya ardhi na kudumisha amani pamoja na kuweka mikakati madhubuti na lengo ya maendeleo kwa pamoja.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, katika kufanikisha zoezi hilo, NLUPC huandaa Miongozo ya Ushirikishwaji Katika Mipango na Usimamizi wa Matumizi Bora ya Ardhi Vijijini (Participatory Land Use Management – PLUM) kuanzia ngazi ya Wilaya na hatimaye katika ngazi ya kijiji huwa kuna kamati ya VLUM.
Miongozo hiyo inabainisha hatua kuu sita katika mchakato wa upangaji na utekelezaji ambapo hatua hizo zinapitia mchakato mzima wa maandalizi, upangaji, utawala na usimamizi wa ardhi, tathmini, ufuatiliaji, uimarishaji na urejeaji mipango.
Kwa kufuata mchakato huo, wilaya na vijiji vilivyokwishaanza utekelezaji wa PLUM kila wakati vinatakiwa view katika nafasi ya kujitathmini na kuelewa vyema vimo katika hatua gani ya PLUM kwa kufuata Mpango Kazi wa Jamii (Community Action Plan – CAP) waliojiwekea, ambao kimsingi huandaliwa katika Hatua ya Pili ya PLUM.
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, hatua hizo sita zilizoainishwa katika Mwongozo wa PLUM zinahusisha pia utawala na usimamizi wa ardhi kwa kuzingatia sheria za ardhi.
Hatua ya Kwanza ni maandalizi wilayani ambapo inahusisha uhamasishaji, kuunda timu ya PLUM ya Wilaya, na kuweka Mpango wa Utekelezaji wa PLUM wa Wilaya.
Hatua ya Pili ni kufanya tathmini ya Matumizi ya Ardhi Vijijini – PRA ambayo inahusisha uhamasishaji wa taasisi za kijiji na kuweka mpango kazi wa jamii – CAP.
Hatua ya Tatu inahusu Mipaka ya Ardhi ya Kijiji ambayo inahusisha kubaini, kuweka na kupima mipaka ya ardhi ya kijiji, utatuzi wa migogoro ya mipaka, msjala ya ardhi ya wilaya, pamoja na utoaji wa Cheti cha Ardhi ya Kijiji.
Hatua ya Nne inahusu upangaji wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji na mikakati ya usimamizi na utekelezaji wake, ambapo inahusisha ushirikishwaji katika mipango na usimamizi, kuainisha hatua stahili za usimamizi (Land Management Measures), na Sheria Ndogo za Usimamizi wa Matumizi Bora ya Ardhi.
Hatua ya Tano inahusu Utawala wa Ardhi ya Kijiji, ambayo inahusisha masjala ya ardhi ya kijiji, utoaji, usajili na usimamizi wa Hatimiliki za Kimila, na utatuzi wa migogoro ya miliki.
Hatua ya Sita inahusu Utekelezaji wa Hatua Stahili za usimamizi wa Ardhi na Uimarishaji, ambapo inahusisha mafundi sanifu wa kijiji, uendelezaji hatua stahili, uimarishaji, tathmini, ufuatiliaji na urejeaji mipango.

Uundaji wa Timu ya PLUM ya Wilaya
Uzoefu wa MaendeleoVijijini unaonyesha kwamba, Timu ya PLUM ya Wilaya huundwa na Halmashauri ya Wilaya husika, ikihusisha wajumbe 4 – 6 kutoka sekta kuu zinazohusika na matumizi ya ardhi ikiwemo Kilimo, Mifugo, Maliasili, Ardhhi na Maendeleo ya Jamii.
Kwa kawaida, mtaalam anayehusika na mipango ya matumizi ya ardhi wilayani ndiye huwa mratibu wa timu hiyo.
Majukumu ya timu ya PLUM ni kuratibu na kuwezesha uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi wilayani.
Katika kutekeleza hayo, hapana budi timu hiyo kuandaa mpango wa jumla wa utekelezaji, unaoonyesha jinsi gani wilaya inakusudia kuviwezesha vijiji vyake vyote kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi.
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, kwa kufuata vigezo vilivyoainishwa, hupendekeza kuteua baadhi ya vijiji kuwa vya kuanzia (vya mfano) ambavyo vitawezeshwa katika kipindi cha muda mfupi (miaka 2-3), vijiji vitakavyoongezeka katika muda wa kati (miaka 3-5), na muda mrefu (miaka 5 na kuendelea) kama inanvyoshauriwa kwenye miongozo ya PLUM.
Vilevile, timu hiyo huandaa Mpango Kazi (Action Plan) na kuhakikisha rasilimali zinazohitajika kwa utekelezaji kama vile fedha, nguvu kazi na vitendea kazi vinapatikana kwa wakati.
Kwa uzoefu uliopo, ni muhimu timu hiyo izingatie uhusishaji wa sekta zote husika (sectoral integration) katika upangaji na utekelezaji, ikiwemo miradi na taasisi zisizo za kiserikali (CBOs na NGOs) zinazohusika na matumizi ya ardhi na rasilimali zake.
Aghalabu, Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi (NLUPC) huwezesha warsha iliyoandaliwa na wilaya husika ili kuhakikisha wilaya inajiandaa vyema kutekeleza PLUM katika vijiji vyake.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, vijijini ambavyo vina mipango ya atumizi bora ya ardhi iliyoandaliwa kwa ushirikishwaji ikihusisha sekta kuu za matumizi ya ardhi, vina nafasi kubwa ya kutekeleza kwa ufanisi miradi ya kisekta kama vile PADEP (Kilimo), WMA na CBFM (Maliasili), na utoaji na usajili wa Hatimiliki za Kimila (Ardhi).
Uzoefu unaonyesha kwamba, baadhi ya miradi hiyo inataka kufikia hatua ya kumilikisha ardhi kwa wanavijiji katika maeneo wanayofanyia kazi.
Kwa mfano, Mradi wa Usimamizi wa Maeneo ya Wanyamapori (Wildlife Management Areas – WMA) ulishughulikia Vyeti vya Ardhi ya Vijiji na Hatimiliki za Kimila katika wilaya za Serengeti, Meatu, Iringa Vijijini na Kilolo.
Mradi wa Maji na Mazingira Vijijini (RWSSP) mkoani Simiyu ulishughulikia utoaji wa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji na Hatimiliki za Kimila kwa maeneo ya vyanzo vya maji katika Wilaya ya Bariadi, wakati huo ikiwa ndani ya Mkoa wa Shinyanga.
Aidha, Mradi wa Usimamizi wa Misitu kwa Kushirikisha Jamii (Community-Based Forest Management – CBFM) ulifanikisha utoaji wa hatimiliki za Kimila za maeneo ya misitu ya jamii katika wilaya za Liwale mkoani Lindi, na Iringa Vijijini na Kilolo mkoani Iringa.
Kwa ujumla, MaendeleoVijijini inaamini kwamba, hatimiliki za ardhi zikitolewa kwa kuzingatia matumizi ya sekta moja moja zinaweza kukwamisha maendeleo na kuleta migogoro ya matumizi ya ardhi wakati itakapofikia kukosa ardhi kwa matumizi mengine kwa vile sehemu kubwa ya ardhi itakuwa imemilikishwa kwa matumizi ya sekta fulani iliyowahi kuwa na mradi kijijini.
Mfano mzuri ni Kijiji cha Kiwere katika Wilaya ya Iringa Vijijini, ambapo kupitia mradi wa CBFM (Maliasili) mwaka 2005 kilitenga hekta 4,904 kama msitu wa hifadhi na hekta 1,500 kama msitu wa matumizi mbalimbali yakiwemo kuni, mijengo, mbao na kadhalika wakati kijiji kizima kina eneo la hekta 6,859.
Hiyo inamaanisha kwamba eneo lililotengwa kwa ajili yam situ ni asilimia 93 ya eneo lote la kijiji.
Kwa kuwa hawakutenga maeneo ya kutosha kwa shughuli nyingine, sasa wanautumia msitu huo kwa shughuli za kilimo na mifugo.
Katika hali kama hiyo, inabidi kusitisha utoaji wa hati miliki mpaka kijiji kinapokuwa kimeandaa mpango wa matumizi ya ardhi unaozingatia matumizi ya sekta zote kuu.

Kesho tutaangalia namna wananchi wanavyoshirikishwa katika tathmini ya ardhi ya vijiji.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974



Comments