Featured Post

TANZANIA YASHIKA NAFASI YA 10 KWA UZALISHAJI WA GESI AFRIKA

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
TANZANIA ni nchi ya 10 barani Afrika kati ya nchi 16 kwa uzalishaji wa gesi asilia, huku ikishika nafasi ya 66 duniani.
Hatua hiyo imetokana na ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia unaoendelea kufanyika, hali inayoleta matumaini kwamba taifa hilo linaweza kujikwamua kiuchumi ikiwa rasilimali hizo zitasimamiwa ipasavyo.

Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati wa Kimataifa (International Energy Agancy – IEA), nafasi ya Tanzania katika uzalishaji wa gesi asilia inatokana na rekodi za mwaka 2011, ambapo taifa hilo lilizalisha meta za ujazo milioni 860 kwa mwaka.
Hata hivyo, rekodi za sasa zinaonyesha kwamba Tanzania ina akiba ya gesi iliyothibitishwa ya meta za ujazo trilioni 17.0688 ambazo ni sawa na futi za ujazo trilioni 56.
Ongezeko hilo linatokana na kugundulika kwa akiba kubwa ya gesi katika maeneo mbalimbali tangu mwaka 2010 hadi 2015.
Katika orodha hiyo ya mwaka 2011, Tanzania iko mbele ya Angola (meta za ujazo milioni 752 kwa mwaka), Cameroon (meta za ujazo milioni 150 kwa mwaka), Gabon (meta za ujazo milioni 70 kwa mwaka), Morocco (meta za ujazo milioni 60 kwa mwaka), Ghana (meta za ujazo milioni 50 kwa mwaka), na Senegal (meta za ujazo milioni 20 kwa mwaka).
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, akiba iliyothibitishwa ya gesi asilia barani Afrika nayo imekua sana kutoka meta za ujazo trilioni 64.008 (futi za ujazo trilioni 210) mwaka 1980 hadi kufikia meta za ujazo trilioni 155.1432 (509 tcf) mwaka 2012, likiwa ni ongezeko la asilimia 140, huku ugunduzi mwingine mpya ukiendelea kushika kasi katika nchi za Tanzania na Msumbiji.
Nchi jirani ya Msumbiji inashika nafasi ya sita Afrika na 54 duniani kwa kuzalisha meta za ujazo bilioni 3.82 za gesi asilia kwa mwaka.
Kwa mujibu wa IEA, vinara katika orodha hiyo kwa upande wa Afrika ni Algeria, ambao hadi kufikia mwaka 2011 walikuwa wanazalisha meta za ujazo bilioni 82.76 kwa mwaka, wakishika namba 9 duniani.
Katika mwaka 2015 ilizalisha wastani wa gesi asilia meta za ujazo bilioni 2.9 kwa siku ambayo baada ya kuisindika katika mitambo yake mitatu imekuwa ikisafirisha kupitia mabomba mawili yanayokwenda Hispania na moja kwenda Italia.
Misri inashika nafasi ya pili Afrika na ya 15 duniani kwa kuzalisha meta za ujazo bilioni 61.26 kwa mwaka; Nigeria ni ya 28 duniani ikizalisha meta za ujazo bilioni 31.36; Libya ya 45 duniani ikizalisha meta za ujazo bilioni 7.855; Guinea ya Ikweta ni ya 47 duniani ikizalisha meta za ujazo bilioni 6.88; Tunisia inashika nafasi ya saba Afrika na 57 duniani kwa kuzalisha meta za ujazo bilioni 1.93; Ivory Coast inafuatia ikiwa ya 60 duniani kwa kuzalisha meta za ujazo bilioni 1.5 kwa mwaka; na Afrika Kusini inashika nafasi ya 61 duniani kwa kuzalisha meta za ujazo bilioni 1.28.
IEA ambayo inakusanya taarifa za nishati kutoka mabara yote matano duniani, inasema kwamba, kwa mwaka 2013 Marekani ndiyo ilikuwa kinara miongoni mwa mataifa 10 yanayoongoza kwa uzalishaji wa gesi asilia duniani ambapo ilizalisha meta za ujazo bilioni 689, likiwa ni ongezeko la asilimia 19.8 kulinganisha na mwaka uliotangulia.
Russia ndiyo iliyofuatia kwa kuzalisha meta za ujazo bilioni 671 (ongezeko la asilimia 19.3), Qatar ilizalisha meta za ujazo bilioni 161 (ongezeko la asilimia 4.6), Iran meta za ujazo bilioni 159 (ongezeko la asilimia 4.6), Canada meta za ujazo bilioni 155 (ongezeko la asilimia 4.5), China meta za ujazo 115 (ongezeko la asilimia 3.3), Norway meta za ujazo 109 (ongezeko la asilimia 3.1), Uholanzi meta zaujazo bilioni 86 (ongezeko la asilimia 2.5), Saudi Arabia meta za ujazo bilioni 84 (ongezeko la asilimia 2.4), na Algeria ikashika nafasi ya 10 kwa kuzalisha meta za ujazo bilioni 80 likiwa ni ongezeko la asilimia 2.3 kulinganisha na mwaka uliotangulia.
Mataifa hayo kumi kwa pamoja yalizalisha meta za ujazo trilioni 3.479 za gesi asilia.
Takwimu zinaonyesha kwamba, mwaka 2009 uzalishaji wa gesi asilia duniani ulishuka kwa asilimia 2.8 huku mataifa makubwa yanayoongoza kwa uzalishaji nayo yakiathirika na ndicho kipindi ambacho Marekani iliibuka kuwa kinara kwa kuzalisha gesi duniani ikiipiku Russia.
Hata hivyo, Russia ilirejea kileleni mwaka 2010 baada ya uzalishaji wake kuongezeka kwa asilimia 4.4 na kuimarisha uwiano wa uzalishaji uliokuwa umeshuka katika nchi za Ulaya kwa asilimia -9 licha ya kuongezeka kwa uzalishaji kwa nchi za Norway na Uholanzi.
Takwimu za Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi (OECD) za mwaka 2009 zilionyesha kwamba uzalishaji wa gesi asilia duniani kwa mwaka huo ulishuka kwa asilimia 0.1 huku Russia ikiongoza kwa kuporomoka kwa asilimia 12 na Algeria ikishuka kwa asilimia -6.
Katika Mashariki ya Kati, maendeleo ya uzalishaji wa gesi asilia yalishuka hadi asilimia 4 na kukua kwa kasi ndogo kuliko mwaka 2008 ambapo uzalishaji ulikuwa katika asilimia 7.
Kwa mwaka 2011, nchi za Nigeria, Algeria na Misri zilikuwa miongoni mwa nchi 20 bora duniani kwa kuwa na akiba iliyothibitishwa ya gesi asilia.
Wakati ambapo Nigeria ilishika nafasi ya 8 ikiwa na akiba ya futi za ujazo trilioni 187, Algeria ilikuwa ya 10 ikiwa na akiba ya futi za ujazo trilioni 159 na Misri ilikuwa ya 17 ikiwa na futi za ujazo trilioni 77, ambazo kwa pamoja ni sawa na asilimia 6.8 ya akiba yote iliyothibitishwa duniani.
Mwaka 2012 Afrika ilielezwa kuwa na akiba iliyothibitishwa ya gesi asilia iasi cha futi za jazo trilioni 509.406 kikitokana na akiba iliyopo katika nchi 20, huku Tanzania ikitajwa kushika nafasi ya 20 ikiwa na akiba ya futi za ujazo bilioni 230, ambazo kwa sasa zimeongezeka kutokana na ugunduzi mwingi uliofanyika, kikiwemo kiasi cha futi za ujazo trilioni 4.17 kilichogunduliwa katika Bonde la Ruvu na kampuni ya Dodsal ya Uarabuni.
Mataifa mengine na kiwango cha akiba iliyothibitishwa kikiwa kwenye mabano ni Nigeria (180.458 tcf), Algeria (159 tcf), Misri (77.2 tcf), Libya (52.795 tcf), Angola (10.947 tcf), Cameroon (4.77 tcf), Msumbiji (4.5 tcf), Congo Brazzaville (3.2 tcf), Sudan na Sudan Kusini kwa pamoja (3 tcf), Tunisia (2.3 tcf), Namibia (2.2 tcf), Rwanda (2 tcf), Guinea ya Ikweta (1.3 tcf), Ivory Coast (1 tcf), Gabon (1 tcf), Mauritania (1 tcf), Ethiopia (880 bcf), Ghana (800 bcf), na Uganda (500 bcf).
Kama ilivyoelezwa hapo juu, Tanzania hivi sasa itakuwa juu endapo takwimu mpya zitatolewa, kwani imefanikiwa kugundua gesi asilia katika maeneo mengi.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.


Comments