Featured Post

SUNGURA ANA KASI KUBWA YA KUZAA BILA MAHABA


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
SUNGURA ni mmoja wa wanyama wanaozaana kwa kasi kubwa. Sifa hii imekuwa chagizo katika mukhtadha mzima wa kuhamasisha ufugaji wa sungura kibiashara kwa sababu mkulima anaweza kuwa na kundi kubwa la sungura katika kipindi kifupi.

Lakini kwa dhima hii, ndipo wametokea baadhi ya watu wa kati – madalali ambao baadhi yao wamesajili makampuni kabisa kisheria – wanaowahamasisha wakulima kwa kuwapigia hesabu za kwenye makaratasi kwamba watakuwa mamilionea ndani ya kipindi kifupi bila kuzingatia uhalisia wenyewe.
Watu hawa, ambao asilimia 99 ni wale ambao hawajawahi kufuga wala kuona adha na changamoto za mifugo, wamefikia hatua ya kuwasainisha wakulima mikataba ya kinyonyaji kwa madai kwamba wao wanajua wapi masoko yalipo wakati ukweli biashara wanayoifanya ni ile ya ‘mkulima kwa mkulima’, yaani wanaangalia nani wamemsainisha mkataba na kama anao sungura wa mbegu wanakwenda kuchukua na kumuuzia mwingine.
Soko la namna hiyo tunaweza kulifanya sisi wenyewe wakulima kama tutaunda umoja wetu madhubuti badala ya kutegemea madalali ambao wanatunisha vitambi maofisini bila kujua adha iliyopo katika ufugaji wenyewe.
Nimewahi kuzungumza huko nyuma kuhusu suala la uzalishaji wa sungura, kwamba ni wanyama wanaozaa kwa kasi. Sungura wa jamii nyingi kipindi cha uzazi hudumu kwa miezi tisa kwa mwaka, kuanzia Februari hadi Oktoba.
Sehemu nyingine kama Australia na New Zealand, kipindi cha uzazi huwa kati ya Julai na Januari.
Sungura jike anafikia uwezo wa kuzaa anapokuwa na miezi sita wakati dume anakuwa amekomaa anapofikisha miezi saba.
Kipindi cha mahaba kwa sungura jike na dume huwa ni kifupi sana, ni kati ya sekunde 30 hadi 40 tu hivi. Unapotaka kupandisha, ni vyema kumchukua sungura jike na kumpeleka katika kizimba cha dume na siyo kinyume chake.
Tabia zao za mahaba zinahusisha kulambana, kunusana na hapo dume atamfuata jike. Kukojoa nayo ni moja ya tabia za mahaba kwa sungura.
Mimba hutungwa takriban saa kumi baada ya tendo la unyumba na baada ya hapo sungura jike huanza kujitengenezea kiota au shimo na kukinakshi kiota hicho kwa manyoya yake kutoka katika baadhi ya sehemu zake za mwili, hususan tumboni na eneo lenye matiti. Hii husaidia pia chuchu kuonekana ili iwe rahisi kwa watoto wake kuziona chuchu hizo watakapozaliwa, kwa vile watoto wa sungura huzaliwa vipofu na hawana manyoya.
Macho ya watoto wa sungura hufunguka siku 11 baada ya kuzaliwa na huanza kula wenyewe wanapofikisha siku 14. Watoto hao huwa hawana manyoya lakini ngozi yao hulindwa na aina fulani ya manyoya ya kitoto ambayo huanza kuota siku chache baada ya kuzaliwa.
Manyoya magumu huota baada ya wiki tano au sita na akifikisha umri wa miezi sita na nane manyoya hayo nayo hutoka na kurithiwa na manyoya mengine ambayo huishi nayo hadi mwisho wa uhai wake.
Sungura kwa kawaida anabeba mimba kwa siku 35 ingawa wengine wanaweza kuzaa kati ya siku ya 32 au 33 baada ya kubeba mimba.
Kwa kawaida, sungura jike aliyeshika mimba hujulikana kwa mwenendo wake, huwa mtulivu, na hula chakula kidogo.
Sungura anazaa watoto kati ya wanne na 15 kutegemeana na umri na afya yake na maumbile ya watoto hutegemea pia umbile la mama. Sungura wenye umbile kubwa huzaa watoto wakubwa na wenye afya.
Kwa kwaida sungura hunyonyesha kwa siku 30 ingawa sungura huacha kuwahudumia (kuwanyonyesha) watoto wake wanapofikisha umri wa wiki nne na tano. Kwa kuwa maziwa yake yana virutubisho vingi, sungura hunyonyesha watoto wake mara chache sana, takriban mara moja au mbili tu kwa siku.
Kwa kuwa ni mnyama ambaye hupata joto kila wakati, hata wakati ananyonyesha, sungura anaweza kupata ujauzito wakati wowote kama usipokuwa makini na afya yake na watoto wake.
Hiyo maana yake ni kwamba, ndani ya mwaka mmoja tangu anapoanza kuzaa, sungura anaweza kuwa na watoto, wajukuu na vitukuu takriban 800.
Kama unafuga sungura kibiashara na kwa tija – ingawa wana uwezo wa kuzaa hadi mara nane kwa mwaka – watengee muda ili wazae mara tano tu kwa mwaka. Hii maana yake kama atazaa wastani wa watoto nane kwa mara moja, kwa mwaka atazaa watoto 40.
Idadi ya watoto watakaokua itategemea mama yao ni mzuri kiasi gani katika unyonyeshaji na ubora wa afya yake pamoja na jitihada zako katika kuwatunza.
Sungura jike ambaye hawezi kufikia kiwango hicho cha uzazi lazima aondolewe. Kama sungura hazai, basi anakutia hasara kwa sababu anatumia chakula bila faida.
Wastani wa uzito unaotakiwa ni kati ya kilogramu 2 hadi 2.5 wakati sungura anapofikisha umri wa wiki nane hadi 10.
Muda huo hutegemea pia na matunzo yako unayompatia, aina ya sungura, mazingira, na kiwango cha protini unachomchanganyia kwenye lishe yake.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974


Comments