Featured Post

SOTOKA YA MBUZI - PESTE DES PETITS RUMINANTS (PPR)


UGONJWA wa Sotoka ya Mbuzi au 'Tauni ya Mbuzi na Kondoo' (Peste des Petits Ruminants – PPR) husababishwa na virusi na hushambulia kondoo na mbuzi ukiwa na dalili zote kama Sotoka (rinderpest) inayoshambulia wanyama kama ng'ombe, nyati, ngamia na wengineo.

Kwa taarifa tu ni kwamba ugonjwa wa Sotoka (rinderpest) ulitokomezwa duniani mwaka 2011 na Shirika la Afya Duniani (WHO) kufanikiwa kuudhibitisha.
Ugonjwa wa PPR ulisambaa sana miaka ya 1980 na kuathiri sehemu kubwa ya Afrika na duniani kote ambapo huwashambulia zaidi mbuzi kuliko kondoo.
Kwenye ng'ombe unaweza kuukuta kwa kupima damu, lakini kwa kawaida ng'ombe hawataonyesha dalili wala kuusambaza ugonjwa wa PPR.
Ugonjwa huu unaweza kuua wanyama kwa kiwango cha mpaka asilimia 100% kutegemeana na umri wa wanyama, afya, lishe na kuchoka kutokana na kufuata malisho umbali mrefu sana.
Kwa wanyama wenye umri kati ya miezi 4 - 8 hali huwa mbaya zaidi na pia wanyama wenye maradhi mengine ni rahisi kushambuliwa kutokana na kinga kuwa chini.

KUSAMBAA
Ugonjwa PPR husambaa kwa njia ya kugusana na virusi vya ugonjwa huu huwa kwenye matongotongo, makamasi, mate na kinyesi cha wanyama.
Kwa hiyo mnyama mwingine akigusa kimoja kati ya hivi ataambukizwa ugonjwa huu.

DALILI
Dalili kwa wanyama ni kama kuharisha.
-Homa kali kati ya siku 5 – 8
-Mnyama hutoa makamasi ya kawaida na baadaye kubadilika rangi na kuwa ya kahawia
-Kuziba pua na kusababisha ugumu wakati wa kupumua
-Michubuko kwenye pua na midomo
-Wanyama kutoona vizuri kutokana na matongo tongo kwenye macho
-Mnyama kuishiwa maji mwilini na pia mimba kutoka.
Matongotongo

UCHUNGUZI
Uchunguzi wa kitaalam ufanywe na maofisa ugani wa mifugo ili kugundua uwepo wa ugonjwa huo kwa kuukagua mwili kuona uwepo wa makamasi ya kahawia.
Watakagua pia kuona kama mnyama anatoa kinyesi cha maji maji chenye harufu mbaya.
Pia watachunguza njia ya hewa, chakula na sehemu ya juu ya mdomo (hard palate). Kwenye utumbo wa mnyama aliyekufa kwa ugonjwa huo huwa na mistari kama ya pundamilia.
Kuvimba kwa mitoki na usaha kwenye mapafu ni mojawapo ya mambo ambayo yanaweza kugunduliwa.
Baada ya hapo damu ya mnyama itachukuliwa na kupelekwa kwenye maabara ikisafirishwa kwenye hali ya ubaridi (refrigeration).
Utumbo wa mbuzi aliyekufa kwa Sotoka.


DAWA
Ugonjwa wa PPR hauna dawa ila kwa wanyama watakaoweza kuhimili dawa za kuua bakteria (antibiotics) zitasaidia kuzuia mashambulizi ya juu dhidi ya bacteria hao.

KINGA
Chanjo ya ugonjwa huu ipo. Unachotakiwa kufanya ni kuwasiliana na maofisa ugani wa mifugo katika eneo lako.
Chanjo ni muhimu mara moja kwa mwaka kabla ya kuanza kwa mvua za masika.
Tenga wanyama wapya wiki tatu kabla ya kuwachanganya na wengine.
Tenga wanyama wagonjwa na wazima mara ugonjwa unapoibuka.
Osha mabanda yako kwa dawa za kuulia virusi kama virukill au tumia dawa za madoa kama JIK kiasi cha lita moja kwa lita 30 za maji kisha pulizia.

Comments