Featured Post

SIKU BOLI ZOZO 'ALIPOIBUKIA' YANGA NA KUICHAPA SIMBA 2-0!

Kikosi cha Yanga cha mwaka 1994. Kutoka kushoto waliosimama ni Salum Kabunda 'Ninja', Constantine Kimanda, Steven Casmir Nemes, Kenneth Pius Mkapa, Selemani Mkati. Waliochuchumaa kutoka kushoto ni Nico Bambaga 'Machine', Sekilojo Chambua, Edibily Lunyamila, James Tungaraza 'Boli Zozo', na Said Mwamba 'Kizota'.

Na Daniel Mbega
YOUNG Africans, ambayo mwaka 1993 iliteswa sana na wapinzani wake wa jadi, Simba, baada ya kutamba misimu miwili ya nyuma, hatimaye Jumamosi Februari 26, 1994 iliingia kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwakabili ‘wanyama hao wakali’ wa Msimbazi, ambao mwaka huo walikuwa wameongeza makucha yao kwa kuwasajili wachezaji mahiri na wauaji wa mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara, Yanga.
Katika mchezo huo wa raundi ya nne ya Ligi Daraja la Kwanza ya Tanzania Bara, Young Africans waliingia uwanjani wakiwa wanadharauliwa kutokana na ubutu wa fowadi yao tokeo ligi hiyo ianze na kutokana na jinsi walivyoonyesha mchezo hafifu dhidi ya Moroka Swallows ya Afrika Kusini katika mechi ya Kombe la CAF kwenye uwanja huohuo Jumamosi ya Februari 19.
Licha ya kuwa na wachezaji kama Edward Chumila na Dua Said, ambao walikuwa wauaji wakubwa wa Young Africans, siku hiyo pia Nteze John Lungu aliongezeka katika safu ya wachezaji wa Simba waliokuwa na usongo na timu ya Jangwani, kwani makeke yake yalikuwa yanaeleweka wakati alipokuwa na Pamba ya Mwanza. Kwa upande mwingine, Young Africans kwa wakati huo haikuwa na mchezaji yeyote aliyekuwa na asili ya kuitisha Simba, hasa baada ya Said Mwamba kuumia na kulikuwa na hati hati ya kutocheza siku hiyo.
Mchezo huo ndio uliotarajiwa kudhihirisha mengi katika msimu huo wa ligi na hasa ulikuwa mtihani wa mambo kadhaa kwa timu zote mbili.
*Mchezo huo ulikuwa mtihani mkubwa zaidi kwa uongozi mpya wa Young Africans chini ya Mwenyekiti Dk. Jabir Katundu.
*Mchezo huo ulikuwa mtihani mkubwa kwa makocha wa kigeni, Tambwe Leya wa Zaire aliyekuwa akiifundisha Young Africans na Dragan Popadic wa Yugoslavia aliyekuwa akiinoa Simba.
*Mchezo huo ulikuwa mtihani mkubwa kwa wachezaji wapya wa timu zote mbili ili kudhihirisha kama usajili uliofanyika ni wa maana. Uwezo wa walinzi Constantine Kimanda na Ngandou Kazadi Ramadhani kutoka Burundi ulitarajiwa kuthibitishwa katika ngome ya Yanga, pia akina Philemon ‘Fumo’ Felician, Sekilojo Chambua, James Tungaraza, Nteze John, Masoud Shaaban, Dua na mdogowe Samora Said na wengineo, nao walikuwa wakiangaliwa wangefanya nini siku hiyo.
*Pia mchezo huo ulikuwa unaangaliwa kama ungeweza kusababisha migogoro mingine kwenye klabu hizo, ambazo kila mara zilikuwa zikiparaganyika baada ya mchezo kama huo.
Fowadi ya Young Africans, ambayo msimu huo ilikuwa inaelezwa kuwa butu, hatimaye siku hiyo ya Jumamosi Februari 26, 1994 iligeuka kuwa kali na kuwakata vibaya wapinzani wake wa jadi, Simba kwa kuicharaza magoli 2-0. Safu hiyo ya ushambuliaji ilionekana kuwa kali tangu mchezo huo ulipoanza, ambapo washambuliaji kama James Tungaraza, Sekilojo Chambua, Edibily Lunyamila, Mohammed Hussein walifanya kazi nzuri huku wakisaidiwa na mabeki walioongozwa na Warundi Constantine Kimanda na Ngandou Ramadhani.
Magoli yote mawili ya Yanga yalipatikana katika kipindi cha pili baada ya timu zote kukosa nafasi nzuri za kufunga katika kipindi cha kwanza, hasa Yanga, ambayo washambuliaji wake walitaka kuonekana butu kweli kabla ya kubadilika katika kipindi cha pili.
Mohammed Hussein alifunga goli lake la kwanza kutokana na juhudi zake za kuuwahi mpira baada ya George Masatu aliyelala chini kuuparaza kwa mkono. Lakini goli la pili ndilo lililokuwa la kiufundi zaidi, ambalo lilikaribiana na goli ambalo lilifungwa na Boli Zozo wa Stella Abidjan ya Ivory Coast dhidi ya Simba katika fainali ya Kombe la CAF mjini Dar es Salaam mwaka 1993, ambalo nalo lilikuwa la pili katika kipindi cha pili.
James Tungaraza, ambaye alifunga goli hilo, alipokea pasi kutoka kwa Sekilojo Chambua na kuanza kuwahesabu mabeki wa Simba mmoja baada ya mwingine hadi alipomuona Mohammed Mwameja alikokuwa ameelekea na kuujaza mpira upande mwingine wa nyavu, tena huko ndiko Boli Zozo alikoukwamisha.
Goli hilo liliwafanya mashabiki kulipuka kwa hoi hoi wakilitamka jina la Boli Zozo...Boli Zozo!!
Washambuliaji wa Simba, Nteze John, Madaraka Selemani, Edward Chumila (na baadaye Abdul Ramadhani Mashine) na Juma Amir, hawakuonekana walichokifanya na hata mabeki wa Simba, wakiongozwa na George Magere Masatu na Godwin Aswile walizidiwa maarifa na kumfanya kipa wao Mwameja mwenye majivuno mengi kuelemewa na mashambulizi ya Yanga.
YANGA: Stephen Nemes, Ngandou Ramadhan, Kenneth Mkapa, Method Mogella, Constantine Kimanda, Nico Bambaga, Sanifu Lazaro/Fumo Felician, Sekilojo Chambua, James Tungaraza, Mohammed Hussein, Edibilly Lunyamila/Alli Yusuf ‘Tigana’. Kocha: Tambwe Leya (Zaire)/Nzoysabah Tauzany (Burundi).
SIMBA: Mohammed Mwameja, Kasongo Athumani, Mustafa Hoza/Thomas Kipese, Godwin Aswile, George Masatu, Iddi Selemani, Athumani China, Edward Chumila/Abdul Mashine, Juma Amir, Nteze John. Kocha: Dragan Popadic (Yugoslavia)/Abdallah Kibadeni.
Waamuzi wasaidizi walikuwa Joseph Kimoho wa Morogoro na Leslie Liunda wa Dar es Salaam, wakati mgeni rasmi alikuwa Augustine Lyatonga Mrema, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za kuchapishwa. Ukinakili ni lazima uandike rejea kwamba ni kutoka mtandao wa www.maendeleovijijini.blogspot.com, vinginevyo unaweza kuchukulia hatua za sheria kwa Sheria ya Haki Miliki na Ujirani.

Comments