Featured Post

SERIKALI YALAUMIWA JUU YA UVUVI HARAMU BWAWA LA MTERA


Na John Mnubi, Iringa
Wavuvi wanaofanya shughuli za uvuvi katika Bwawa la Mtera Kijiji cha Migoli wilayani  Iringa wamelalamikia vitendo vya uvuvi haramu katika bwawa hilo.
Mvuvi, Albert Mkeleja alizitupia lawama mamlaka husika kwa kutolivalia njuga swala la uvuvi haramu ambalo limeshamiri sana kwa sasa katika bwawa hilo.
 Aidha, Mkeleja alisema hana imani na wanao endesha zoezi la kukamata wavuvi haramu akidai kuwa wanachelewa kurudia zoezi hivyo  watu wanatengeneza tena nyavu na kuendelea na  uvuvi haramu.
“Alikuja hapa Mkuu wa Wilaya wakati wa uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji tuliongea nae kuhusu uvuvi haramu akasema tatizo hili malalamiko ni mengi, akamwambia Diwani kazi yako hii. Halafu akasema kwamba nyinyi wavuvi ndo mnajua zaidi wanaovua uvuvi haramu kuliko mimi, hivyo mwaweza kudhibiti uvuvi haramu ukaisha kwa kushirikiana na uongozi wa idara ya uvuvi,” alisema Mkeleja.
Mvuvi mwingine, Mika Weston, naye alikiri kuwepo kwa  uvuvi haramu uliokithiri katika maeneo ya Bwawa la Mtera upande wa Mkoa wa Iringa.
“Kwa kawaida mvuvi unapotega nyavu inabidi ukae pembeni ulinde, lakini maofisa uvuvi wanakataza badala yake hudai wavuvi warudi forodhani wapaki mitumbwi na kurudi wanapokaa. Ukirudi kesho unakosa nyavu zako,” alisema Weston.
Ofisa huyu akiangalia nyavu zilizochomwa moto baada ya kukamatwa kutokana na kutokuwa na kiwango kinachotakiwa katika uvuvi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Migoli, alisema kuwa kumekuwa na matukio kadhaa ya wavuvi kuibiana nyavu na samaki kwenye maeneo ambapo wavuvi huvua kwa njia ya kutega.
 “Watu na zana hukamatwa kwa mfano, hivi karibuni kulikuwa na kesi hiyo ambapo watu walikamtwa wakiwa kwenye uvuvi haramu, na kwasababu huku kwetu kutokana na jitihada za makusudi za uhifadhi, samaki wanapatika mana samaki hupenda sehemu iliyotulia hivyo wavuvi toka mikoa mingine jirani hutamani samaki wanaopatikana huku,” alisema Bosco.
Aidha kwa pamoja  Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Makatapola, Msafiri Chansi na Mwenyekiti wa kijiji hicho , Felix Nzigilwa, waliwatupia lawama maafisa uvuvi wa mkoa wa Dodoma kwa kushindwa kutilia mkazo swala la uvuvi haramu kama wanavyo jitahidi maafisa wa upande wa Iringa.
“Maafisa uvuvi wa wilaya za Dodoma pamoja na wilaya za Iringa kwa pamoja wawe na mpango mkakati kutokomeza wimbi la uvuvi haramu usiachiwe upande mmoja,” alishauri Mwenyekiti Nzigilwa.
Kata ya Migoli ina asili ya ukame,wakazi wake wengi wanategemea bwawa la mtera kwa ajili ya kujipatia chakula na kipato kingine.

Comments