Featured Post

NDIGANA KALI (EAST COAST FEVER ) UGONJWA HATARI UNAOSHAMBULIA NG’OMBE, MBUZI, KONDOO NA NYATI

Ng'ombe aliyekufa kutokana na Ndigana Kali


UGONJWA wa Ndigana Kali au kitaalam East Coast Fever (ECF) hushambulia wanyama kama ng'ombe, mbuzi, kondoo, nyati na nyati wa India wakaao kwenye maji (Water Buffalo).

Ugonjwa huu husababishwa na vimelea (protozoa) vijulikanavyo kama Theileria parva ambavyo husambazwa na kupe wekundu wa kwenye masikio wajulikanao kama Rhepicephalus Appendiculatus.

Kwa kawaida, ugonjwa huu usipodhibitiwa unaweza kusababisha vifo vya wanyama wengi sana na pia ni aghali kuutibu kulinganisha na magonjwa mengine.
Ndigana Kali ni ugonjwa ulioenea sana hapa nchini kwetu na Afrika Mashariki, ambapo ng’ombe huanza kuugua siku 10 – 25 (wastani siku 14) tangu kuambukizwa.

DALILI ZAKE
-Joto kali hadi kufikia 42c badala ya joto la kawaida la ng’ombe la nyuzijoto 38c
-Homa kali
-Mnyama kushindwa kupumua vizuri
-Kukohoa
-Kuharisha
-Kuvimba matezi ya shingoni
-Manyoya ya mgongoni husimama muda wote na huwa na rangi ya udongo (brown) kwa mbali
-Kutoa makamasi laini
-Kupe aina ya rephicephalus appendiculatus wataonekana ndani ya masikio ya mnyama (sio lazima)
-Mnyama hushindwa kula vizuri
-Pua (muzzle) huwa kavu bila unyevu unyevu.

MATIBABU
Mnyama inabidi apigwe sindano ya dawa za PARVAQUONE au BUTALEX kiasi cha ml 20 (soma kimbatanisho cha dawa kwa maelezo zaidi) na kurudia baada ya siku moja kupita, yaani akichomwa leo unarudia dozi kesho kutwa.

Pia mnyama achomwe dawa ya OTC 20% kipindi chote cha matibabu.
Dawa aina ya BUTALEX ni maarufu sana hapa nchini kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huu, ni muhimu dalili za mwanzo zinapoonekana kumtaarifu mtaalam wa mifugo na ikithibitika ni Ndigana Kali tiba ianze mara moja ikiambatana na OTC 20% ili kushusha homa.

KINGA
Kinga kubwa ni kuogesha mifugo yako mara kwa mara kwenye majosho au kwa kuwanyunyuzia dawa za kuua wadudu wa mifugo.
Dawa ijulikanayo kama PARANEX hupatikana katika maduka yote ya kilimo na mifugo. Dawa nyingine nazo zinafaa kuogeshea kwa kufuata masharti ya mtengenezaji.

Comments