Featured Post

MAMBO KANGAJA HUENDA YAKAJA, YANGA FADHIL BWANGA....

Yanga Bwanga (kushoto). Picha kwa hisani ya zenjdar.co.uk

Na Daniel Mbega
NAMKUMBUKA mtangazaji nguli wa kipindi cha michezo cha Radio Tanzania Dar es Salaam (RTC wakati huo - sasa TBC Taifa), marehemu Abdul Masoud, katika siku ambayo Yanga ilimsajili kiungo mshambuliaji machachari Yanga Fadhil Bwanga kutoka kwa 'Wagosi wa Kaya' Coastal Union mwaka 1976 kama sikosei. Nilikuwa mdogo sana wakati huo, lakini ndiyo kwanza nilikuwa ninapenda michezo hasa tukiwa tunajikusanya nyumbani kwa Balozi wa Nyumba Kumi, jirani yetu tu pua-na-mdomo, aliyekuwa na redio ya 'Mkulima' kila siku saa mbili kasorobo.

Siikumbuki vizuri siku hiyo, lakini ninachokikumbuka ni utangulizi wa habari kuu ya siku hiyo ambapo Abdul Masoud alisema: "Haya tena, mambo kangaja huenda yakaja... Leo katika Uwanja wa Mkwakwani Coastal Union yaifunga Yanga... Lakini Yanga Fadhil Bwanga ajiunga na Yanga!"
Naam, yalikuwa ni maneno mazito hasa ikizingatiwa ushabiki wa mpira wakati huo ulivyokuwa juu tofauti na sasa ambapo utandawazi umewafanya wengi wanashabikie timu za Ulaya wanazoziona kwenye luninga.
Vijana waliokuwa katika hirimu ya kaka zangu walikuwa na ubishani mkubwa na huo ndio uliotufanya hata sisi watoto kupenda michezo, hasa mpira. Wakati huo ndiyo burudani pekee ambayo tuliweza kuisikiliza kwenye redio ukiacha vipindi vya muziki wa Chaguo la Msikilizaji na vinginevyo.
Haikushangaza hata mara moja kukuta watoto tukigeuza maboga kuwa mpira, na wakati mwingine 'msambi' ambao ulitengenezwa na matambara. Ndiyo mipira iliyokuwa ikitumiwa na kaka zetu, magozi tuliyasikia tu redio.
Siku hiyo Yanga ilikuwa imefungwa na Coastal Union katika mchezo mkali wa kirafiki kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Mwaka huo Coastal Union haikufika fainali ya Ligi ya Taifa (sasa Ligi Kuu) baada ya kutolewa kwenye hatua ya Kanda.
Lakini kikosi chake kilikuwa imara mno. Ikumbukwe pia kwamba, Abdul Masoud wakati huo ndiye alikuwa Katibu Mwenezi wa Yanga baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi uliosimamiwa na serikali kufuatia mgogoro mkubwa uliokuwa umeikumba klabu hiyo na kuwafukuza wachezaji 20, ambao baadaye ndio waliounda Pan Africans, akiwemo Rais wa sasa wa TFF, Leodgar Tenga,Gibson Sembuli, Sunday Manara, Boi Idd 'Wickens', Ally Yusuf, na wengineo.
Pamoja na kuwa na wachezaji chipukizi, lakini Yanga ilishindwa kufua dafu mbele ya Wagosi wa Kaya.
 Baada ya mchezo huo Yanga wakamtorosha Yanga Fadhil Bwanga na kwenda 'kumhifadhi' kwa ndugu zake Pangani ili Coastal wasiushtukie mchezo huo. Coastal walipopata fununu waliweka mtego barabarani na kukagua kila gari iliyopita. Ilivumishwa kwamba Yanga Bwanga alisafirishwa na lori la mkaa, lakini (watanisahihisha wakongwe) inaelezwa kwamba baada ya kupumzika siku kadhaa Pangani, alipitia Bagamoyo na kuingia Dar. Hiyo ndiyo hadithi yake, naamini wakongwe wanaweza kunisahihisha katika hili.
Hata hivyo, hapa nazungumzia tukio lililofanywa na Yanga Bwanga katika mechi baina ya Yanga na Simba mwaka 1977 ambapo alivunja pambano hilo. 
Siku hiyo ya Jumapili Novemba 27, 1977 kwa mara nyingine Simba iliifunga tena Yanga kwa mabao 2-1 katika pambano ambalo lilivunjika dakika 12 kabla ya wakati wake kutokana na mchezaji Yanga Bwanga wa Yanga kukataa kutoka nje baada ya kuamuliwa na mwamuzi kufanya hivyo.
Bwanga, kwa makusudi kabisa, alimpiga daluga Nicodemus Njohole wa Simba kifuani ikiwa ni kulipiza kisasi kwa mchezaji huyo ambaye alikuwa amemtegea wakati wakiwania mpira. Bwanga alikuwa ameonywa mara ya kwanza kwa kadi ya njano katika dakika ya 16 alipomfanyia rafu Nicodemus tena na hivyo baada ya rafu mbaya kwa mara ya pili ikalazimika atolewe nje.
Lakini mchezaji huyo hakushtuka kwa amri hiyo badala yake akaendelea kurukaruka uwanjani akifanya mazoezi mepesi. Mwamuzi Stephen Lutayangirwa baada ya kusubiri kwa dakika 10 alipuliza kipenga cha kumaliza mchezo.
Mchezo wenyewe ulikuwa wa kwanza wa kuwania Kombe la Jitegemee, ambapo uliharibiwa kabisa kutokana na uchezaji mbaya wa wachezaji wa timu zote ambao walikuwa wakitembezeana madaruga na kuonyeshana ubabe wa dhahiri.
Kulikuwa na vipindi vichache sana vyenye msisimko na mara nyingi kulikuwa na rafu na mchezo wa hasira. Mwamuzi naye alistahili lawama kwa kufanya mchezo kuharibika zaidi. Hakuwa mkali inavyopasa kila wachezaji walipokuwa wakifanya makosa uwanjani.
Ukali pekee aliouonyesha wenye busara ni alipomtoa nje ya uwanja Daudi Salum 'Bruce Lee' wa Simba na Ayubu Shaaban wa Yanga walipokingiana ngumi. Kabla ya hapo alikuwa amewaonyesha kadi za njano Omar Mahadh na Daudi Salum wa Simba, na Yanga Bwanga wa Yanga.
Mameneja wa timu hizo Mohammed Viran wa yanga na Abdulrahman Khamis Muchacho wa Simba ndio walioonyesha urafiki baada ya kuvunjika kwa mchezo huo kwani walitoka nje wakiwa wameshikana mikono huku wapenzi wa timu hizo mbili wakilaumiana kwa mchezo mbovu wa timu zao.
Simba iliwazidi kimchezo wapinzani wao katika dakika za mwanzo hadi walipojipatia bao lao la kwanza katika dakika ya 18. Mpira uliotoka kwa Abdallah Kibadeni aliyeupeleka mbele ulimkuta Jumanne Hassan Masimenti ambaye naye alitoa pasi ya kichwa kwa George Kulagwa ambaye aliachia mkwaju mkali ambao kipa wa Yanga Isega Isindani alishindwa kuukumbatia. Rahim Lumelezi aliyekuwa karibu akauwahi na kuutumbukiza wavuni.
Kuanzia hapo hadi mapumziko mchezo ulipooza sana ingawa Yanga ilikuwa ikicheza kwa ufundi zaidi ambao ungewaletea goli la kusawazisha kunako dakika ya 22 kwa kiki ya nguvu iliyopigwa na Karabi Mrisho lakini ikapaa juu ya goli.
Yanga iliwaingiza Ramadhan Mwinda na Danny Mwalusamba badala ya Karabi Mrisho na Burhani Hemed kipindi cha pili kilipoanza, lakini mabadiliko hayo hayakuleta tofauti sana.
Katika mojawapo ya hatari langoni mwa Simba, Filbert Rubibira aliunawa mpira na mwamuzi akaamuru penalty ipigwe. Wachezaji wa Yanga walitegeana kupiga mpaka Charles Mwanga alipojitolea lakini alipopiga mpira ukaota mbawa kwa kupaa juu ya goli.
Simba ilijiongezea bao la pili dakika ya 54. Bao hilo lilianzia na mpira wa kona iliyochongwa na Abdallah Kibadeni na kusababisha kizaazaa langoni, Nico Njohole akatokea na kufunga kirahisi.
Bao pekee la Yanga lilifungwa na Ezekiel Grayson dakika ya 64. Mohammed Kajole ndiye aliyesababisha bao hilo baada ya kuuachia mpira ambao angeweza kuokoa akidhani kipa wake Omar Mahadh atauwahi. Ezekiel akatokea na bila taabu akafumua mkwaju uliotinga wavuni.
Yanga ikaanza kucheza vizuri kuanzia hapo hadi mchezo ulipovunjika, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda.
Yanga: Isega Isindani, Charles Mwanga, Fadhil/Boniface Makomole, Selemani Jongo, Hashim Kambi, Sam Kampambe, Burhani Hemed/Danny Mwalusamba, Ezekiel Grayson, Karabi Mrisho/Ramadhan Mwinda, Yanga Bwanga, Ayoub Shaaban.
Simba: Omar Mahadh, Daudi Salum, Mohammed Kajole, Aloo Mwitu, Filbert Rubibira, Athumani Juma, Rahim Lumelezi, Nico Njohole, Jumanne Hassan, Kibadeni, George Kulagwa.

NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Ukirejea ni lazima eleze chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.

Comments