Featured Post

MAGONJWA YA SUNGURA: MAAMBUKIZI YA BAKTERIA KATIKA NGOZI (PYODERMA)


MAAMBUKIZI ya bacteria katika ngozi ya sungura kitaalam huitwa pyoderma

Mara nyingi maambukizi haya hutokea wakati ngozi ya sungura inapochanika, au wakati ngozi inapokuwa wazi hasa katika mazingira ya unyevu nyevu, hivyo kuathiri hali ya kinga iliyomo ndani.
Kwa kawaida, bacteria wa afya hupatikana katika ngozi ya sungura na hasa katika ute wa juu.
Hata hivyo, wakati mwingine hali hiyo inaweza kuathiriwa na kuruhusu bacteria wabaya kumea humo na kuleta madhara.

Dalili

Dalili nyingi za pyoderma hutegemea na aina ya maambukizi ya bacteria kwa sungura, lakini baadhi ya dalili ambazo aghalabu huonekana ni pamoja na:
* Kunenepeana hovyo
* Kuhara damu
* Maumivu ya misuli
* Kutokwa na majimaji puani (na mara chache kwenye macho)
* Maambukizi ya njia ya mkojo
* Hali ya uchafu
* Kukunjamana kwa manyoya (hasa katika sehemu ya haja kubwa, mapaja na tumboni)
* Wekundu katika eneo lililoambukizwa
* Ugonjwa wa meno (kuvimba kwa fizi na kuoza kwa meno).

Chanzo 

Kwa kawaida maambukizi ya bacteria kwenye ngozi hutokea wakati ngozi ya sungura inapokuwa imechanika, mara nyingi hutokea wakati ngozi hiyo inapokuwa wazi katika mazingira duni, yakiwemo ya unyevu.
Inaweza kutokea pia wakati anapokuwa na majeraha au msukumo dhaifu wa damu mwilini.
Pyoderma, kwa kiasi kikubwa, huonekana mara nyingi kama ilivyo kwa majeraha  na michubuko kwa binadamu, hasa watoto.
Bacteria wanaosababisha pyoderma ni pamoja na:
 * Staphylococcus aureus
* Pseudomonas aeruginosa
* Pasteurella multocida.
Bacteria wanaweza pia kupenya kwenye sehemu zilizo wazi au kunaswa kwenye manyoya yaliyokunjamana, hususan kwa sungura walio dhaifu au wenye kunenepeana hovyo.

Uchunguzi

Bwana mifugo atahitaji kutazama sababu zote kabla ya kuanza uchunguzi wa kina, kwani kuna baadhi ya mambo ambayo yanaweza kufanana na maambukizi ya ngozi.
Hayo ni pamoja na:
* Utitiri kwenye masikio (Ear mites), ambao unaweza kusababisha michubuko pembezoni mwa masikio, na kusababisha kunyonyoka kwa manyoya pembezoni mwa masikio na kwenye mfereji wa sikio
* Chawa, ambao wanaweza kusababisha kunyonyoka kwa manyoya na kukunjamana kwa manyoya katika maeneo mengi ya mwili
* Hali ya ngozi baada ya kuchomwa sindano ya chanjo, ambayo inaweza kusababisha michubuko na hata vijipu
* Kaswende ya Sungura (Rabbit syphilis), hali ambayo mara nyingi husababisha kunyonyoka kwa manyoya.
Kama mojawapo ya sababu hizi hazitaonekana, basi bwana mifugo anaweza kuchukua sampuli ya ngozi au culture ili kubaini visababishi vya tatizo.

Tiba

Kutibu maambukizi ya bacteria kwenye ngozi ya sungura hufanyika kwa njia ya nje ya mwili.
Sungura wengi watahitaji kuogeshwa; eneo husika linapaswa kukaushwa ili kuondoa unyevu.
Kama maambukizi ni makubwa, eneo linalozunguka litahitaji kunyolewa.
Bwana mifugo anaweza kuandika dawa za jamii ya antibiotics ili kupakaa eneo lililoathirika.

Kinga

Ni muhimu kuwapa sungura mlo kamili. Kuzuia kunenepeana hovyo kutapunguza athari za maambukizi katika ngozi.
Kupunguza manyoya marefu na kuwasafisha kwa brashi manyoya yao kutapunguza pia uwezekano wa maambukizi.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974


Comments