Featured Post

MAFUTA NA GESI: KILA RAIA WA NORWAY ANAMILIKI DOLA 173,000, MTANZANIA ANADAIWA SHS. 778,000.

KILA raia wa Norway, hata yule ambaye hajazaliwa, ana uhakika wa akiba ya Kroner takriban 600,000 wakati hapa Tanzania pekee, kila mmoja anadaiwa zaidi ya Shs. 700,000 kutokana na Deni la Taifa,” ndivyo anavyosema Profesa Patrick Lumumba, Mkuu wa Shule ya Sheria ya Kenya. 

Profesa Lumumba anasema kwamba, uchumi imara wa Norway unaotokana na usimamizi madhubuti wa mafuta na gesi, ukichangiwa na idadi ndogo ya watu ambao asilimia kubwa ni wazalishaji, umeifanya nchi hiyo kuwa mfano duniani katika ukuzaji wa uchumi. 
Profesa Lumumba alisema uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea hasa barani Afrika ambazo zina rasilimali mbalimbali unashindwa kukua kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uongozi mbovu, rushwa, uzembe pamoja na idadi kubwa ya watu. 
Hali hiyo, alisema inazifanya nchi hizo kuwa na mzigo mkubwa wa kuhudumia watu wake na kushindwa kutoa huduma bora kama elimu, afya na nyinginezo, hivyo kulazimika kukopa ili kuziba pengo lililopo.
“Norway ina watu milioni 5.2 tu, idadi ambayo ni sawa na wakazi wote wa Dar es Salaam, lakini uchumi wake ni mkubwa, wameweza kulinda rasilimali zao na kudhibiti kasi ya kuzaliana ili kuwa na nguvu imara inayopata huduma zote muhimu. 
“Kwa mujibu wa sharia inayosimamia Mfuko Maalum wa mapato ya rasilimali hizo (Government Pension Fund-Global), serikali imeruhusiwa kuchukua asilimia 4 ya fedha hizo ili kufanya shughuli nyingine za maendeleo, hususan uwekezaji, lakini kutokana na kujimudu kiuchumi, ni mwaka jana tu ndipo ilipanga kuchukua kiasi ili kuwekeza,” alisema Profesa Lumumba. 
Kulingana na takwimu zilizopo, Tanzania inaelemewa na mzigo wa deni la Shs. 35.01 trilioni huku ikijikongoja kukuza uchumi wake, wakati nchi ndogo ya Norway ina akiba ya Dola 900 bilioni katika Mfuko huo Maalum, ambazo ni takriban Shs. trilioni 1,939. 
Hali hiyo inawafanya raia 5,214,900 wa Norway, nchi inayotegemea uchumi mkubwa wa mafuta, kuwa na akiba ya wastani wa Dola 173,077 (Shs. 373,028,000) kila mmoja, fedha ambazo zimeanza kuwekwa kwenye mfuko huo kwa zaidi ya miaka mingi, lengo likiwa kuwekeza kwa vizazi vijavyo utajiri huo unaotokana na mafuta. 
Norway inaamini kwamba, ipo siku mafuta yatakwisha, hivyo wanapaswa kuweka akiba ya fedha kwa vizazi vijavyo ili navyo vije vinufaike kwamba nchi yao iliwahi kuwa na rasilimali za mafuta badala ya kusoma kwenye vitabu kama historia bila kuona manufaa yoyote. 
Kutokana na deni linaloikabili Tanzania, wachambuzi wa masuala ya uchumi na wanasiasa wamekuwa wakisema kwamba, kwa Watanzania milioni 45 waliopo sasa, maana yake kila mmoja anadaiwa Shs. 778,000, huku utafiti na takwimu ukionyesha kiwango cha umaskini vijijini kimepungua kwa asilimia 6.1 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. 
Dk. Joel Silas wa Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema kwamba, uwiano wa uchumi na idadi ya watu ni muhimu kuzingatiwa, kwani ndio unaoweza kupima maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. 
Mtaalamu huyo wa uchumi anasema, baadhi ya nchi zimepiga hatua kiuchumi kutokana na idadi ya watu na rasilimali zilizopo, na kusisitiza kwamba uzazi wa mpango ndiyo njia pekee inayoweza kufanikisha jitihada za mataifa yanayoendelea kujikwamua kiuchumi. 
“Huwezi kuzungumzia maendeleo bila kutazama idadi ya watu, hata nyumbani, chakula kinapikwa kulingana na watu waliopo, wakati mwingine katika hali ya umaskini, inalazimu watu waliopo, hata kama watakuwa wengi, wagawane chakula hicho hata kikiwa kidogo – ndiyo hali inayozikabili nchi zinazoendelea ambazo zinashindwa kukidhi mahitaji ya watu wake na kulazimika kukopa,” anasema. 
Ingawa Tanzania inajivunia kugunduliwa kwa uchumi mpya wa gesi na mafuta, lakini hauwezi kusaidia ikiwa kasi ya ongezeko la watu haitapungua, huku idadi kubwa wakiwa tegemezi. 
Wakati Tanzania yenye ukubwa wa kilometa za mraba 947,303 na idadi ya watu milioni 45, ni watu milioni 25.59 tu wanaofanya kazi na kuzalisha, ikizidiwa kwa mbali na Norway ambayo kati ya watu milioni 5.2, karibu watu milioni 3 (sawa na asilimia 69) wenye umri kati ya miaka 15-74 wanafanya kazi. 
Aidha, Pato la Taifa la Tanzania (GDP) nalo liko chini (Dola 48.06 bilioni) huku kipato cha mwananchi mmoja mmoja kikiwa Dola 768, wakati GDP ya Norway ni Dola 363.290 bilioni na kipato cha mwananchi mmoja ni Dola 69,712 kwa mwaka. 
Ongezeko la idadi ya watu duniani, ambalo linachangiwa na mambo mengi, yakiwemo ukosefu elimu na huduma za uzazi wa mpango, linatajwa kuwa janga linalokwamisha hata Malengo Endelevu ya Dunia
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, idadi ya watu duniani inaongezeka kwa watu 200,000 kila siku huku asilimia kubwa ikiwa ni katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania. 
Katika kipindi cha miaka 20 kati yam waka 1980 na 2000 idadi ya watu duniani iliongezeka kutoka bilioni 4.4 hadi watu bilioni 6, huku asilimia 85 ya ongezeko hilo ikitokea katika nchi maskini na zinazoendelea. 
Kupungua kwa idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi katika miongo kadhaa, kumesaidia kuongeza idadi ya watu lakini kumekuwa changamoto kubwa katika uchumi wa mataifa mbalimbali kutokana na kusababisha uhaba wa ajira pamoja na huduma nyingine muhimu za kijamii. 
Mahitaji muhimu kama chakula, huduma za afya, elimu, makazi, ardhi, ajira na nishati yanakumbwa na changamoto kubwa kwenye mataifa yanayoendelea ambayo uchumi wake unajikongoja. 
Mnamo Septemba 25, 2015, nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliridhia malengo 17 kwa nia ya kutokomeza umaskini, kulinda sayari dunia, kudumisha ustawi kwa wote ikiwa ni sehemu ya agenda ya maendeleo endelevu ambapo kila lengo limepangiwa kukamilika katika kipindi cha miaka 15 ijayo. 
Ili kuyafikia malengo hayo, serikali, sekta binafsi, taasisi za kijamii na jamii kwa ujumla inapaswa kushiriki kikamilifu katika njia zote ambazo zinaweza kuleta tija, lakini suala la uzazi wa mpango likipaswa kupewa kipaumbele.

1. Kutokomeza kabisa umaskini wa namna zote 
2. Kutokomeza njaa, kuhifadhi chakula na kuboresha lishe pamoja na kuhimiza kilimo endelevu 
3. Kuhakikisha maisha bora na kudumisha ustawi wa wote katika kila umri 
4. Kuhakikisha ushirikishwaji na upatikanaji wa elimu bora pamoja na kudumisha fursa za kujifunzia kwa wote 
5. Kufikia usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana 
6. Kuhakikisha upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na mazingira 
7. Kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu, ya uhakika, endelevu na ya kisasa kwa wote 
8. Kudumisha ukuaji endelevu wa uchumi wenye ushirikishwaji, na ajira za kudumu na zenye tija kwa watu wote 
9. Kujenga miundombinu bora, kudumisha ushirkishwaji wa maendeleo endelevu ya viwanda na kuchochea ubunifu 
10. Kupunguza matabaka ndani na miongoni mwa nchi zote 
11. Kuyafanya majiji na makazi ya watu kuwa ya ushirikishwaji, salama, bora na endelevu 
12. Kuhakikisha uwiano sawa wa uzalishaji na matumizi 
13. Kuchukua hatua za dharura kupambana na mabadiliko wa mazingira na athari zake 
14. Kutunza na kusimamia matumizi endelevu ya bahari na rasilimali za majini kwa maendeleo endelevu 
15. Kulinda, kuhuisha na kudumisha matumizi endelevu ya vyanzo vya maji, usimamizi endelevu wa misitu, kukabiliana na hatari ya jangwa, na kukomesha na kutunza ardhi ili kuokoa viumbe hai 
16. Kudumisha Amani na kushirikisha jamii kwa maendeleo endelevu, kudumisha upatikanaji wa haki kwa wote na kujenga taasisi imara na zinazowajibika katika ngazi zote 
17. Kuimarisha njia za utekelezaji na kutoa kipaumbele cha Ushirikiano wa Dunia kwa Maendeleo Endelevu


Comments