Featured Post

JUMA SALIM LAIZER UBAO 'KING MAKUSA': MMASAI WA LONGIDO MTUNZI WA 'ZOGOLO JANGU' ALIYEPIGA SOLO, SAX, KINANDA, TUMBA NA KUIMBA KATIKA SINGLE TRACK MOJA NDANI YA DAKIKA NNE!

Juma Ubao 'King Makusa' akicharaza gitaa.

Juma Ubao ‘King Makusa’ (alizaliwa mwaka 1950, Dodoma, Tanzania, akipewa jina la Juma Salim Laizer) ni mwanamuziki mahiri ambaye mwaka 1976 aliwaacha hoi watangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) baada ya kuimba na kupiga ala tano tofauti ndani ya dakika nane wakati akirekodi wimbo mmoja. 
Juma Ubao ni mwanamuziki mwenye vipaji vingi ambavyo ni watu wachache wanaojaliwa kuwa navyo na umahiri wake unakumbukwa kuanzia miaka ya 1970 hadi 1990 wakati muziki wa dansi ulipokuwa kwenye chati ya juu.
Juma Ubao anakumbukwa kwa kutoa mchango mkubwa katika kujenga taifa kutokana na kuhamasisha wananchi kwenda kujiunga katika Vijiji vya Ujamaa, ukimbizaji wa Mwenge, na Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika kupitia muziki.

Maisha yake ya awali
Jila lake halisi ni Juma Salim Laizer, aliyezaliwa mkoani Dodoma mwaka 1950 kwa mama Sheila Sindano na baba yake ni Mmasai Salim Laizer. Tunaweza kusema, Juma Ubao ni Mmasai wa kwanza kuwa mwanamuziki katika enzi zake ingawa hivi sasa wapo wasanii wengi wa Kimasai.
“Kabila langu ni Mmasai ingawa nimezaliwa Dodoma, lakini asili yangu ni Kijiji cha Mabebu kilichopo Longido, mkoani Arusha,” alipata kusimulia Ubao.
Juma Ubao 'King Makusa' (kushoto) akicharaza gitaa. Kulia na Andy Brown Swebe enzi za uhai wake.
Kutokana na kawaida ya Wamasai ambao huhama hama na mifugo wakitafuta malishi na maji, babu wa babu zake alijikuta amefika Kondoa, mkoani Dodoma na mababu zake hao wakasilimishwa katika Uislamu ingawa baadaye wakaweka maskani yao mjini Dodoma.
Baba yake Salim Laizer aliyeishia darasa la tano, alikuwa mhasibu katika Shirika la Reli la Afrika ya Mashariki (EAR) akifanyika kazi katika mji wa Iringa.
Jina la Ubao alipachikwa na wapenzi na mashabiki wa muziki baada ya kuridhishwa na upigaji wa ala nyingi kwa wakati mmoja, wakimlinganisha na ubao ambao hutumiwa katika kufanya kazi nyingi.
Juma Ubao alipata elimu yake katika shule ya msingi ya Wamissionari ya Consolata mjini Iringa hadi alipomaliza darasa la nane mwaka 1965. 
Alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo waliofaulu mtihani wa darasa la nane, akachaguliwa kwenda kujiunga katika shule ya Sekondari ya Tosamaganga ya mkoani humo hadi alipomaliza kidato cha nne mwaka 1969.
Miaka hiyo wasomi hawakuwa wengi nchini Tanzania, hivyo elimu ilikuwa mithiri ya ‘lulu’.  Elimu yake ya kidato cha nne ilimpatia kazi nzuri mwaka 1970 kwenye kitengo cha Colito Barracks iliyopo Lugalo jeshini, ambako alikuwa akijifunza muziki katika bendi ya muziki wa mapipa (brass band).
Hamu ya muziki ikaanzia hapo na mwaka 1972 alijiunga na bendi ya Polisi Jazz ‘Vangavanga’. Baadaye alijiunga katika bendi ya King Africa iliyokuwa na wanamuziki mchanganyiko kutoka Zambia na Wacongo akina Frolie, Monga Stanii na Tomaa ‘Kabotolo’. Bendi hiyo ilikuwa ikiporomosha muziki wake katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa ukimilikiwa na mfanyabiashara maarufu Fadhili Batengas, maeneo ya Tazara, Buguruni.
Mwaka 1973 kulipoanzishwa Vijiji vya Ujamaa nchini Tanzania, Juma Ubao alishiriki kikamilifu kuhamasisha wananchi kwenda kujiunga katika vijijini hivyo. 
“Tulinusurika kuliwa na Simba tukiwa porini huko Mkongo wilaya ya Rufiji, wakati wa oparasheni ya Vijiji vya Ujamaa,” alipata kukumbuka Juma Ubao.
Safari yake katika muziki iliendelea kwa kujiunga katika bendi ya STC Jazz iliyokuwa ikimilikiwa na Shirika la Umma la State Trade Corporation mwaka 1975. 
Baadaye STC ikabadilishwa kuwa Bodi ya Biashara ya Ndani (Board of Internal Trade) ambapo bendi hiyo nayo ikabadili jina na kuitwa Biashara Jazz. Juma Ubao alipigia bendi hiyo hadi mwaka 1982 wakati bendi ilipotoweka katika taswira ya muziki.
Ikumbukwe kwamba miaka ya 1970 baadhi ya mashirika ya umma yalianzisha vitengo vya michezo na burudani. Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) lilikuwa na bendi ya UDA Jazz waliokuwa wakipiga katika mtindo wao wa ‘Bayankata’, Kiwanda cha nguo cha Urafiki kilikuwa na bendi ya Urafiki Jazz wakitamba na mtindo wa ‘Chakachua’, Shirika la Bima la Taifa (NIC), nalo lilikuwa na bendi ya Orchestra Bima Lee wakitamba na mtindo wa ‘Magnet Tingisha’.
Mwaka 1976 akiwa Biashara Jazz ndipo alipopachikwa jina la King Makusa ambapo mwenyewe alipata kukumbuka tukio hilo akisema:
“Mwaka 1976 tulikwenda studio za Radio Tanzania (RTD), kurekodi nyimbo zetu. Niliwaacha midomo wazi watayarishaji na watangazaji wa wakati huo akina Khalid Ponela, John Luanda, Charles Hilary, Frank Kirumbi, Gilbert Boma na fundi mitambo wao James Mhilu na Crispin Lugongo, wakinishuhudia nikipiga sehemu sita katika wimbo mmoja ndani ya dakika nane. Nilitayarisha wimbo, nilipiga solo, niliimba, nilipapasa kinanda, nilipuliza saxophone, na kutwanga tumba katika ‘single track’ ndani ya dakika nane…”
Kwa watangazaji hao, ilikuwa ni kitu kipya ambacho hakikuwahi kufanywa na mwanamuziki mwingine yeyote. Ndipo hapo walipompachika jina la King Makusanya, likiwa na maana ya Mfalme Makusanya. Lakini wakashauriana na kufupisha kuwa ‘King Makusa’, jina ambalo lilivuma na kufunika majina yake mengine ya Salim Laizer.
Enzi zake wakati akipiga muziki ukumbini, alikuwa anapiga gita na kinanda, kila ala kwa wakati wake. “Wakati ninaimba gita huliweka ubavuni, saxophone huiweka mgongoni na kinanda pembeni huku watu wakinishangaa,” alijisifia Juma Ubao.
Mwaka 1987 Juma Ubao aliteuliwa kuwa miongoni mwa wanamuziki 57 waliounda kundi la Tanzania All Stars waliotoka na wimbo wa Fagio la Chuma ukiwa ni kauli mbiu ya Rais wa Awamu ya Pili, Alli Hassan Mwinyi, juu ya uwajibikaji.
Mwaka 1989, Juma Ubao alikuwa muasisi wa bendi ya Six Manyara akiwa na wanamuziki wakongwe akina Suleiman Mwanyiro, Hassan Bitchuka, Kassim Rashid ‘Kizunga’, Kasola Rajabu na Manicho Athumani. Wakiwa katika bendi hiyo walifumua vibao vya Batuli na Salama zikiwa ni tungo za Juma Ubao mwenyewe. Nyimbo nyingine zilikuwa Maselina, Fatuma Samahani Sana na Tabu.
Bendi hiyo ya Six Manyara iliundwa kwa madhumuni ya kutangaza fahari za utalii wa Tanzania zikiwemo mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro na vivutio vingine vilivyopo nchini humo. Bendi hiyo ilisafiri kwenda kutangaza utalii katika nchi za Uganda na Kenya mwaka 1991. Wakiwa Kenya walirekodi nyimbo nne katika kampuni ya PolyGram kwenye Long Play. Waliporejea nchini Tanzania wanamziki wake wengine walirudi katika bendi zao za zamani lakini yeye akaamua kubaki na bendi hiyo hadi sasa.
Juma alipumzika mambo ya muziki kwa muda na kuutumia muda huo kwenda kusoma masomo ya jioni akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, akisomea Uhasibu na Biashara na akatunukiwa cheti ambacho kilimpa nafasi ya ajira katika Shirika la Ndege Tanzania (ATC) kama mhasibu katika Klabu ya Jet. Baadaye akahamishiwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere ambako alipewa kitengo cha kusimamia vyakula vya kwenye ndege.
Katika kitengo hicho, Ubao alilipunguzia kwa kiasi kikubwa shirika hilo gharama za malipo zilizokuwa zikilipwa. Yeye alisimamia ipasavyo vyakula vyote kuandaliwa kutoka Klabu ya Jet, badala ya kuvinunua katika Hoteli ya Kilimanjaro.
Baadaye ATC ikaanza kuyumba kiuchumi hali iliyosababisha kupunguza baadhi ya wafanyakazi wake mwaka 2002, miongoni mwao akiwa Juma Ubao.
Mwaka 2000 Six Manyara ilirekodi nyimbo za Somo Somo, Leo Leo zilizopigwa katika mahadhi ya mduara. Wimbo wa Zogolo Jangu uliimbwa kwa lugha ya Kizaramo ikiwa na maana ya ‘Jogoo Langu’. Wimbo wa Sakina ulipigwa katika mtindo wa reggae na nyingine ni Msichana, na Tuluka Chibite ulirekodiwa kwa lugha ya Kigogo ukiwa na maana ya ‘Inuka Tuondoke’. Wimbo mwingine uliotia fora wakati huo ni Bide, ambao Juma Ubao alitunga na kuimba kwa lugha ya Kipogoro.
Juma Ubao akichangia mada kwenye mojawapo ya majukwaa ya sanaa na muziki, wakati akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA).
Demokrasia katika tasnia ya muziki ilifanya kazi yake pale mwaka 2008 Juma Ubao alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) akichukua nafasi hiyo baada ya Kassim Mapili aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, kumaliza muda wake.
Juma Ubao amekwisha pewa nafasi nyingi za uongozi katika tasnia ya muziki nchini Tanzania. Mwaka 2009, aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).
Juma Ubao aliiomba serikali kuwatambua wanamuziki wa zamani ambao walitoa mchango mkubwa kupitia tasnia ya muziki wakati wa kutafuta Uhuru, kuijenga nchi pamoja na kushirki katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.
“Kuthaminiwa kwa wanamuziki hawa si kwa kuwapa pesa pekee, la hasha, bali ni  kuwepo kwa utaratibu japo wa kuweka majina yao kwa baadhi ya mitaa, shule ama hospitali katika halmashauri za Manispaa zetu ili yawe kama vielelezo kwa vizazi vijavyo,” alifafanua.

Familia
Juma Ubao ni baba wa familia ya mke na watoto watano. Anamtaja mkewe Ashanti Mwinjuma kwamba katika kipindi chote katika muziki, ndiye aliyekuwa akimfariji na kumpa moyo kila alipokuwa akikwama.
Watoto wake ni Athumani, ambaye amefuata nyayo zake, yupo nchini Austria, akifanya mambo ya muziki. Laizer, Ibrahimu, Aboubakar na Salma.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. +255 656 331974. Ukinakili tafadhali taja chanzo hiki.

Comments