Featured Post

HIZI HAPA NDIZO LESENI 26 ZILIZOTOLEWA KWA KAMPUNI 18 KUTAFITI MAFUTA NA GESI!

Vitalu vya gesi katika eneo la Bahari Kuu (Offshore).

 Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
JUMLA ya leseni 26 zimetolewa kwa kampuni 18 zinazojishughulisha na utafiti wa mafuta na gesi asilia katika vitalu mbalimbali nchini Tanzania tangu mwaka 2001 hadi Julai 2014.
Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kwamba, leseni 23 kati ya hizo ni za utafiti wakati leseni tatu ni za uendelezaji.

Aidha, leseni nyingine 22 bado hazijatolewa katika vitalu kadhaa ambapo mbili (katika Kitalu 4/1B na 4/1c) ziko chini ya uangalizi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na vitalu vinne vimeombwa na kampuni ya Shell ya Uholanzi.
Vitalu hivyo, ambavyo bado havijajadiliwa ni Kitalu Namba 9, Namba 10, Namba 11, na Namba 12, ambapo mchakato wa kuyapitia maombi hayo unaelezwa kwamba unafanyika na kuna uwezekano mkubwa kwa Shell kupatiwa vitalu hivyo kwa sababu inakidhi vigezo vyote.
Shell, ambayo sasa ndiyo kampuni kubwa iliyowekeza maeneo makubwa zaidi hasa baada ya kununua hisa nyingi katika kampuni ya BG ya Uingereza ambayo inamiliki vitalu vingi, ndiyo ilikuwa kampuni ya kwanza kabisa pamoja na BP ya Uingereza kufanya utafiti katika Tanganyika mwaka 1952 katika maeneo ya Visiwa vya Pemba, Unguja na Mafia.
Pengine baada ya kutanua makucha kwa kuinunua kampuni ya BG kutaifanya Shell kuaminika zaidi na huenda ikafikiriwa kupewa baadhi ya maeneo iliyoomba.
Vitalu nane kati ya 22 bado zabuni ziko wazi na vinahusisha Kitalu Namba 5 katika maji ya kina kirefu, Kitalu cha Bonde la Kisangire, Bonde la Ziwa Eyasi Wembere, Bonde la Mandawa, Kitalu cha Luwegu, Bonde la Ziwa Rukwa Kaskazini (liliachwa na kampuni ya Heritage), Kitalu cha Selous, na Kitalu cha Tunduru.
Aidha, leseni nyingine nane ziko katika mzunguko wa sasa wa zabuni na zinahusisha maeneo ya Kitalu Namba 4/2A, 4/3A, 4/3B, 4/4A, 4/4B, 4/5A, 4/5B pamoja na Kitalu cha Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika.

Leseni za utafiti
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, leseni tatu zimetolewa kwa kampuni za BG na Ophir kwa pamoja katika Vitalu Namba 1, 3 na 4 katika maji ya kina kirefu wakati kampuni ya Dodsal Resources Limited yenyewe ina leseni ya Kitalu cha Bonde la Ruvu na tayari imegundua akiba kubwa ya gesi asilia.
Kampuni ya Heritage Oil na Petrodel zina leseni mbili katika Vitalu vya Latham na Kimbiji, lakini Heritage pia ina leseni nyingine mbili katika Bonde la Rukwa (Kusini) na Bonde la Kyela.
Ndovu Resources ina leseni mbili za utafiti katika Vitalu vya Mtwara na Kisiwa cha Nyuni wakati Leseni ya utafiti katika Visiwa vya Pemba na Unguja imepewa kampuni ya Atrim Resources huku Jacka Resources ikiwa na leseni katika Bonde la Ruhuhu na Beach Petroleum ikimiliki leseni ya Kusini mwa Ziwa Tanganyika.
Swala Energy ina leseni mbili za Bonde la Pangani na Kilosa, Dominion Petroleum ina leseni ya Kitalu Namba 7 katika maji ya kina kirefu, Maurel et Prom ina leseni za Bigwa wilayani Mkuranga na Mafia, Ophir ina leseni ya East Pande, Motherland Industries ina leseni ya Bonde la Mto Malagarasi na Mnazi Bay Kaskazini leseni iko chini ya kampuni ya Hydrotanz.
Kampuni ya Afren na Petrodel zina leseni moja katika Kitalu cha Bonde la Tanga, Petrobras na Shell kwa pamoja zina leseni ya Vitalu Namba 6 na 8, wakati Statoil na ExxonMobil kwa pamoja zinamiliki leseni ya Kitalu Namba 2.

Leseni za uendelezaji
Maeneo yanayozalisha gesi nchini Tanzania ni machache na ilichukuwa miaka mingi kuanza uzalishaji huo kutokana na matatizo ya miundo mbinu, kukosekana kwa soko la ndani, na kushindikana kusafirisha gesi nje ya nchi kutokana na akiba ya gesi kuwa kidogo. 
Eneo la uzalishaji la Songo-Songo, ambalo linasimamiwa na kampuni ya Pan African Energy, kwa sasa linazalisha gesi asilia yenye akiba ya ujazo futi milioni 110 kwa siku. SongoSongo imekuwa ikizalisha gesi tangu mwaka 2004. Gesi inayozalishwa SongoSongo inachangia kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme unaotumika kwenye viwanda na kwa wateja wa kawaida katika jiji la Dar es Salaam. 
Eneo la uzalishaji la Mnazi Bay lilianza uzalishaji wa gesi Januari 2007 kupitia bomba lenye urefu wa maili 17 kwenda kwenye kituo cha kuzalisha umeme wa megawati 12 kilichopo Madimba, Mtwara. 
Mnazi Bay inasimamiwa na kampuni ya Maurel et Prom, Wentworth Resources na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). 
Septemba 12, 2014, kampuni hizo zilitiliana saini makubaliano ya kuuziana gesi na serikali kwa lengo la kupeleka futi za ujazo milioni 130 za gesi asilia kwenye bomba jipya la gesi linalotoka Mnazi Bay kwenda Dar es Salaam. Bomba hilo ambalo linamilikiwa na serikali, limeanza kutumika mwaka 2015.
Eneo la Kiliwani Kaskazini nalo limeanza uzalishaji wake wa kwanza tangu Aprili 4, 2016 na Ndovu Resources ndiyo yenye leseni hiyo. Gesi ya kwanza ilichimbwa katika kisima cha Kiliwani North-1, eneo ambalo liko jirani na eneo la Songo Songo, ambako gesi itakayopatikana huko itasafirishwa hadi katika mtambo wa kuchakata gesi wa Songo Songo.
Uzalishaji huo umeanza kwa kuzalisha futi za ujazo kati ya milioni 25-30 kwa siku katika siku 90-100 za kwanza kabla ya kuanza uzalishaji mkubwa, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, gesi hiyo itauzwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa bei kama inavyoelekezwa katika Mkataba wa Uuzaji wa Gesi uliosainiwa na pande zote mbili.

Utoaji wa leseni
Leseni zote hizo zimetolewa kwa awamu tangu mwaka 2001 ambayo ndiyo ilikuwa awamu ya kwanza kabisa. Utoaji huo wa leseni wa kwanza wa utafiti na uzalishaji wa gesi na mafuta ulitangazwa Juni 2000 na kufungwa tarehe 19 Aprili 2001. Ulifanyika jijini London, Uingereza. 
Vitalu sita (6) vilivyokuwa kwenye kina cha maji kati ya mita 200 na 2,000 ndani ya mwambao vilinadiwa, lakini ombi moja tu kutoka kampuni ya Petrobras ndilo lililopokelewa. Hatimaye, kampuni ya Petrobras ilipewa Mkataba wa Kuchangia Uzalishaji wa kitalu namba 5.
Awamu ya pili ya utoaji wa leseni ilifanyika Houston, Texas, Marekani ambapo zabuni zilifunguliwa Juni 3, 2001 na kufungwa Julai 5, 2002. 
Katika awamu hiyo, vitalu saba (7) vilivyokuwa kwenye kina cha maji kati ya mita 200 na 2,000 baharini, kikiwemo kimoja kilichokuwa kwenye maji yenye kina kifupi zaidi kusini mwa Zanzibar, na sita (6) kwenye kina kirefu cha maji pembeni mwa kisiwa cha Pemba na Unguja vilinadiwa. Eneo hili lilichukua ukubwa wa kilometa za mraba 114,123. 
Maombi mawili yalipokelewa kutoka kampuni ya Shell International na Global Resources. Kampuni zote ziliomba vitalu namba 9-12. Kamati ya wataalamu kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Wizara ya Nishati na Madini ilibaini ombi la kampuni ya Global Resources kuwa halikidhi masharti kwa kuwa halikuonesha ushahidi wa uwezo wa kifedha wala uzoefu wa utafutaji wa gesi na mafuta ndani ya bahari. Shell bado inasubiri uamuzi baada ya kuomba tena zabuni hiyo ilipoitishwa, na ina nafasi kubwa ya kushinda kwenye vitalu vyote – namba 9-12. 
Ufunguzi wa zabuni katika awamu ya tatu ulitangazwa Mei 2004 na kufungwa Mei 2005. Ufunguzi ulifanyika Denver, Colorado, Marekani na ulihusisha eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 71,103.
Leseni za vitalu saba (7) vilivyokuwa kwenye kina cha maji kati ya mita 200-2,000 zilinadiwa, na vitalu vitatu (3) – kitalu namba 1, 2 na 6 – vilitolewa. Kitalu namba 1 kilitolewa kwa kampuni ya Ophir Energy, kitalu namba 2 kwa kampuni ya Statoil na kitalu namba 6 kwa kampuni ya Petrobras.
Mwezi Aprili 2006, leseni za vitalu namba 3 na 4 zilitolewa moja kwa moja kwa kampuni ya Ophir Energy na serikali.
Mwezi Julai 2006, serikali ilitangaza zabuni kwa ajili ya vitalu viwili vilivyokuwa vimebaki kwa wakati huo na mnamo Januari 19, 2007, leseni ya kitalu namba 7 ilitolewa kwa kampuni ya Dominion Petroleum na kitalu namba 8 kwa Petrobras.
Utoaji wa leseni awamu ya nne ulizinduliwa rasmi Oktoba 25, 2013 wakati wa mkutano na maonyesho ya pili ya sekta ya gesi na mafuta Tanzania.
Zoezi hilo lilipaswa kufanyika Septemba 2012, lakini lilicheleweshwa kutokana na kusubiriwa kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Gesi Asilia Tanzania.
Awamu hii ilifungwa Mei 15, 2014 na ilihusisha eneo la mwambao Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika na vitalu saba (7) vya baharini kwenye kina cha maji kati ya mita 2,000 na 3,000.
Vitalu hivyo vinatofautiana ukubwa kutoka kilometa za mraba 2,545 mpaka zaidi ya 3,600, na vipo mashariki na karibu na maeneo ambayo yameshagundulika kuwa na gesi. 
Vitalu vingine viwili (2) viliachwa kwa ajili ya TPDC, na inatafuta mshirika kupitia njia ya ushindani ili kuendesha utafiti kwenye vitalu hivyo. 
Miongoni mwa vitalu hivyo, vinne viliombwa: Kitalu namba 2A kiliombwa na kampuni ya Mubadala Petroleum; kitalu namba 3A na China National Offshore Oil Corporation (CNOOC Ltd), Statoil kwa kushirikiana na ExxonMobil nao walikiomba; Kitalu namba 3B na Gazprom; na kitalu cha kaskazini mwa Ziwa Tanganyika kiliombwa na Ras Al Khaimah Gas LLC (Rakgas). 
Vitalu vinne (4) vya baharini 4A, 4B, 5A and 5B, havikuombwa.
Kampuni za BG Group na Ophir Energy, ambazo zimekuwa zikiendesha shughuli zao za utafutaji wa gesi asilia nchini, hazikuwasilisha maombi yao. 
Maombi yaliyowasilishwa yanapitiwa na TPDC kuhakikisha kwamba yametimiza vigezo na masharti yaliyowekwa na serikali. Waombaji watakaofanikiwa watakutana na TPDC na serikali kujadiliana vipengele vya Mkataba wa Kuchangia Uzalishaji. 

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974

Comments