Featured Post

HILI NDILO SCUD LA JANGWANI LILILOBOMOA MSIMBAZI MARA MBILI MWAKA 1991

Said Sued 'Scud' (wa tano kutoka kulia) akiwa na kikosi cha Yanga 1991

Na Daniel Mbega
ZIKIWA zimesalia siku tatu tu kabla ya pambano la Simba na Yanga, mashabiki wa timu hizo walikuwa wamepamba moto kucharurana mitaani, lakini wadadisi wa mambo walikuwa wamefikia uamuzi kwamba, pambano hilo lingekuwa kama fainali ya ligi hiyo, kwa sababu, timu yoyote ambayo ingeshinda Jumamosi Agosti 31, 1991 ingekuwa vigumu kuzuiwa na timu nyingine huko mbele isitwae ubingwa wa Tanzania Bara msimu huo.
Simba ilikuwa inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 36 baada ya michezo 26, ikiwa imeshinda 13, kutoka sare 10 na kupoteza mitatu tu, wakati Yanga ilishikilia nafasi ya pili ikiwa na pointi 34 kwa michezo 25, ikiwa imeshinda 13, kutoka sare 8 na kupoteza minne. Timu iliyokuwa inafuatia kwa karibu ilikuwa Pamba ya Mwanza, ambayo ilikuwa na pointi 31 kutokana na michezo 25, ikiwa imeshinda 8, kutoka sare 15 na kupoteza michezo miwili.
Tayari bendera za kijani na njano, na zile nyekundu na nyeupe zilikuwa zimekwishatanda jijini kuashiria kuwa, pambano la msimu lilikuwa limewadia. Tena safari hiyo, bendera hizo hazikutundikwa kwenye mitaa ya Uswahilini tu, bali zilikuwepo hata kwenye majumba ya Msajili katikati ya Jiji, nyingine zikiwa zimening’inizwa kwenye antena za TV.
Simba, ambayo ilikuwa bingwa mtetezi na kiongozi wa ligi, ilihitaji kutoka sare tu ili iendelee kuiacha Yanga kwa pointi tatu, japokuwa ilikuwa imeitangulia kwa mechi moja zaidi.
Kwa upande mwingine, kama Simba ingeshinda mechi hiyo, basi ingeiacha Yanga kwa pointi nne na ingekuwa vigumu kuzuiwa na timu yoyote ile kuhifadhi ubingwa wake. Kama ingeishinda Yanga, basi Simba isingeweza kutishwa na Coastal Union wala MECCO wala Ushirika katika mechi zilizokuwa zimesalia, kwani ushindi huo ungekuwa umeipa nguvu za kutisha kiasi cha timu hizo tatu kuachia pointi zenyewe bila ya kutaka.
Vivyo hivyo, kama Yanga ingeishinda Simba, basi ingekuwa si rahisi kwa RTC Kagera wala Pamba, African Sports au Maji Maji, kuizuia kutwaa ubingwa, ambao iliupoteza mwaka 1990 kwa wapinzani wake. Hali hiyo ndiyo iliyolifanya pambano hilo liwe na upinzani mkubwa zaidi.
Simba ilikuwa inacheza Jumamosi huku ikiwa imefungwa na Pamba magoli 2-0 Agosti 24, lakini Yanga ilikuwa inacheza huku ikiwa imeifunga Coastal Union 2-0 siku hiyo hiyo. Hivyo, Simba ilikuwa inaingia uwanjani ikiwa inajaribu kuwaondolea majonzi wapenzi wake huku Yanga ikiwa inataka kushinda mechi ya tatu mfululizo.
Timu zote nne zililihama jiji la Dar es Salaam kabla ya mechi hiyo. Wakati ambapo Simba ilikuja pole pole kutoka Mwanza ilikotoka kucheza na Pamba, Yanga ilikuwa imekwenda tena Unguja, ambako ilikwenda kabla ya pambano la Mei 18. Agosti 26 Simba ilicheza na Milambo mjini Tabora  na kufungwa goli 1-0 na Agosti 27 iliwafunga mabingwa wa Kanda ya Magharibi, Amka ya Nzega magoli 4-3 huko huko kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, na Yanga, Agosti 26 ilifungwa na Mlandege goli 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan kabla ya kuzifunga Shangani 3-2 Agosti 27 na Small Simba magoli 2-0 kwenye uwanja huo huo.
Pamoja na kwamba timu hizo zilikuwa katika mazoezi makali, lakini pia ukweli ni kwamba, ziliamua kukaa mbali na Dar es Salaam ili kuepuka wachezaji wake wasipewe fedha kwa nia ya kuwarubuni ili kupoteza ushindi na kambi zake zisiingiliwe kimazingara.
Simba ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, kwa sababu, mara kwa mara timu hizo zikutanapo Simba ikiwa imenyongea, kama ilivyokuwa miaka ya 1986 na 1988, mambo huwa mabaya kwa Yanga. Yanga ilitakiwa kujua kwamba, inacheza na golikipa Mackenzie Ramadhani, ambaye msimu huo alikuwa hafungiki kirahisi.
Redio Tanzania Dar es Salaam iliahidi kutangaza moja kwa moja pambano la Simba na Yanga Agosti 31, lakini ikawataka wafanyabiashara nchini kote kujitokeza kutoa matangazo yao kudhamini pambano hilo.
Habari hizo ziliwaondolea wasiwasi wapenzi wa soka Tanzania ambao walifikiri RTD ingeng’ang’ania msimamo wake wa kupata mdhamini mmoja tu wa kulipa shilingi 900,000/- kudhamini matangazo ya mpira wa miguu.
Agosti 24, mwaka huo RTD ilianza kutekeleza azma yake ya kutotangaza mapambano ya soka mpaka ipate mdhamini baada ya kutolitangaza pambano kali la Yanga na Coastal Union, na siku iliyofuata haikulitangaza pambano la Sigara na Tukuyu Stars.
Simba imefungwa tena na Yanga? Kila mwanachama, shabiki na mpenzi wa Simba alikuwa akijiuliza bila kupata jibu. Pengine msamiati sahihi ambao ungeweza kutumiwa kuelezea hali ya wakati huo iliyoikumba klabu ya Simba ni kwamba, walikuwa wamekubali kuitwa ‘Wateja wa Yanga’. Matokeo ya kufungwa tena goli 1-0 kwenye mchezo huo wa ligi yalidumisha mambo kadhaa yahusuyo mechi za Simba na Yanga katika kugombea ubingwa.
Kwanza; mfungaji wa goli hilo moja lililoizamisha Simba Agosti 31, alikuwa yule yule Said Sued ‘Scud’, ambaye alifunga goli lililoiangusha Simba Mei 18 katika mchezo wa kwanza msimu huo.
Pili; kocha Syllersaid Mziray alikuwa amezidi kutoka kifua mbele kwa mara ya nne mfululizo baada ya mechi za Simba na Yanga, ambapo mara ya kwanza ilikuwa Mei 26, 1990 wakati alipokuwa Kocha Msaidizi wa Simba, halafu ikaja Oktoba 20, 1990 akiwa kocha wa Yanga na Mei 18 na Agosti 31, 1991. Hivyo basi, ni kocha aliyejihusisha na timu hizo mbili kongwe, ambaye hakuwa ameonja uchungu wa kufungwa na mojawapo katika michezo minne iliyopita.
Tatu; tangu aanze kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wanachama, Rashid Ngozoma Matunda, hakuwa amefungwa na Simba katika mechi tatu alizosimamia.
Nne, hiyo ilikuwa mara ya tatu kwa Yanga kuishinda Simba katika mechi zote mbili katika msimu mmoja tangu mtindo huo wa ligi wa nyumbani na ugenini uanze kutumika mwaka 1982. Mwaka 1982 Yanga iliifunga Simba goli 1-0 katika mechi ya kwanza na kisha magoli 3-0 kwenye mechi ya marudiano, na mwaka 1987 Yanga iliifunga Simba goli 1-0 katika mechi zote mbili.
Kwa kuwa Simba na Yanga zilikuwa katika nafasi nzuri ya kucheza Ligi ya Muungano, basi zilitarajiwa kukutana mara nne msimu huo. Hali hiyo ilikuwa inaipa ari Yanga ya kutaka kushinda katika mechi zote nne mwaka 1991 na kuandika rekodi ya ajabu na ngumu kuifuta kama Yanga ilivyoshindwa kuifuta rekodi ya kufungwa magoli 6-0.
Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kilimshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Augustine Lyatonga Mrema, kwa ushirikiano wake na chama hicho, ambao ulipelekea mapato kuanza kuwa mazuri katika michezo ya kandanda kwenye Uwanja wa Taifa.
Katibu Mkuu wa FAT wa wakati huo, Meshack Maganga, alisema kwamba, FAT inaishukuru sana serikali kupitia kwa Mrema kutokana na juhudi za Waziri huyo katika kuhakikisha kuwa, kuna ulinzi mzuri wa amani na udhibiti wa uingiaji uwanjani.
Pia Maganga aliwashukuru polisi wote waliohusika na ulinzi katika mechi ya Simba na Yanga na akatoa shukrani za pekee kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Temeke, OCD Mhulo na Msaidizi wake, Matiku, ambao alisema, kazi yao ya kuhakikisha usalama katika Uwanja wa Taifa ilikuwa nzuri mno.
Vile vile aliwashukuru viongozi wa Simba na Yanga kwa kuanzisha vikundi vya sungusungu ndani ya klabu zao kuangalia udhibiti wa malipo katika mechi zao. Alisema utaratibu wa klabu kubadilisha wakaaji milangoni ni mzuri kuliko ule wa zamani wa kuweka watu wale wale kila siku.
Maganga pia alivipongeza vyombo vya habari kwa kazi yao nzuri kwa kuutangaza mchezo wa soka nchini.
Simba safari hii haikukata rufaa kupinga kuchezeshwa kwa Issa Athumani kama ilivyofanya katika mchezo wa kwanza uliofanyika Mei 18. Katika mechi hiyo ya kwanza, Simba ilifungwa na Yanga goli 1-0 lililotokana na pasi ya Issa. Lakini ingawa Issa alicheza tena katika mechi ya pili, hakuna rufaa iliyopokelewa na Kamisaa wa Mchezo, Luteni Kanali Gwaza Mapunda, ambaye alikaa Uwanja wa Taifa mpaka saa tatu usiku akisubiri malalamiko yoyote.
Baada ya mechi ya kwanza, Simba ilikata rufaa kupinga usajili wa Issa kwa madai kwamba, pia alikuwa amecheza ligi ya Oman, lakini kwa kutumia sheria za FIFA, FAT iliikataa rufaa hiyo na hata Simba ilipoipeleka rufaa hiyo BMT, ilikataliwa kwa misingi hiyo, na rufaa hiyo ikapelekwa kwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, ambaye naye alikubaliana na maamuzi ya FAT.
SIMBA: Iddi Pazi, Raphael Paul, Azizi Nyoni, Method Mogella, Frank Kassanga ‘Bwalya’, Iddi Selemani, Itutu Kigi/Jamhuri Kihwelu, Khalfan Ngassa, Bakari Iddi/Issa Kihange, Hamisi Gaga, Zamoyoni Mogella/Ayoub Mzee. Kocha: Hassan Affif.
YANGA: Stephen Nemes, Selemani Mkati/Freddy Felix ‘Minziro’, Kenneth Mkapa, Godwin Aswile, Salum Kabunda, Jumanne Shango, Abubakar Salum, Athumani China, Said Sued ‘Scud’/Joseph Machella, Issa Athumani (nahodha), Thomas Kipese/Sanifu Lazaro. Kocha: Syllersaid Mziray.
Mwamuzi alikuwa Taji Bakari wa Dodoma aliyesaidiwa na Joseph Mapunda wa Songea na Kamisaa alikuwa Luteni Kanali Gwaza Mapunda. Mgeni rasmi alikuwa Athumani Janguo, Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA).
NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Ukinakili hakikisha unareja chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.

Comments