Featured Post

HII NDIYO SHULE ISIYO NA MWALIMU WA KIKE KWA MIAKA 30

Na Daniel Mbega, Mpwapwa
"HAPA kwetu hakuna matukio ya mimba kwa wanafunzi, labda kama wanatoa huko kabla ya kugundulika shuleni," ndivyo anavyodokeza mmoja wa walimu wa Shule ya Msingi Malolo katika wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Anaongeza: "Tutawezaje kuwagundua watoto kama wana mimba au la wakati hakuna mwalimu wa kike hapa? Ni vigumu kwa mwalimu wa kiume kumchunguza mtoto wa kike."
Shule hiyo yenye wanafunzi 386 (wavulana 189 na wasichana 197) haina walimu wa kike kwa zaidi ya miaka 30, hali inayoleta changamoto kubwa hasa kwa watoto wa kike.
Uchunguzi umebaini kwamba, licha ya changamoto nyingi zinazoikabili shule hiyo iliyo katika Kata ya Malolo, tatizo la uhaba wa walimu, hususan wa kike, limekuwa sugu kiasi cha kuleta mazingira magumu kwa wanafunzi wasichana ambao wameshindwa kupata elimu ya hedhi.
“Kukosekana kwa walimu wa kike ni changamoto kubwa, kwa sababu wasichana wengi wanapevuka mapema tangu wakiwa darasa la tano, hivyo wanaposhindwa kupewa elimu ya namna ya kujihifadhi wengi huamua kubaki nyumbani na kukosa masomo mpaka wanaporejea katika hali ya kawaida,” amedokeza mwalimu mwingine ambaye hakupenda kutajwa kwa kuwa si msemaji.
Mwalimu huyo amesema kwamba, ni vigumu kwa walimu wa kiume kuzijua changamoto za watoto wa kike, lakini kama wangekuwepo walimu wanawake ingekuwa rahisi hata kuwapatia elimu ya afya pamoja na suala zima la uhusiano ili kuepusha mimba za utotoni.
Aidha, amedokeza kwamba, ingawa shule hiyo haina rekodi za mimba, lakini ni muhimu ikiwa wanafunzi hao wakapatiwa uelewa ili waweze kujitunza.
“Mwalimu wa kike ndiye anayeweza kuwanasihi kwa kina kwa sababu ya uzoefu alionao kama mwanamke, anaweza kuwaelimisha hata namna ya kujitunza wanapokuwa katika hedhi, lakini ni vigumu kwa sisi wanaume kuketi na watoto wa kike na kuanza kuwaelewesha suala hilo kwa ufasaha,” alisema.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Boniface Massawe, alikiri kwamba ukosefu wa walimu wa kike ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wasichana ambao kwa mazingira ya vijijini, wengi wao wanapokuwa kwenye hedhi hujihisi kama wagonjwa na baadhi hutega masomo kwa kuwa hawajui jinsi ya kujihifadhi.
“Tuko walimu saba tu, wote wa kiume, na sijawahi kusikia kama alikuwepo mwalimu wa kike kwa miaka ya karibuni,” alisema Mwalimu Massawe.
Takwimu zinaonyesha kwamba, Wilaya ya Mpwapwa ina jumla ya walimu 1,283 ambapo kati yao 670 ni wanaume na 583 wanawake.
Bosco Paulo Mwaluga ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji ambaye pia anakaimu nafasi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Malolo, ambaye anabainisha kwamba kukosekana kwa walimu wa kike kunaleta ugumu wa kutambua hata watoto wanaopata ujauzito ingawa anasema hakuna kesi zozote za mimba.
“Kesi za mimba hakuna, kwa sababu ni lazima kuwepo na ushahidi… ingewezekana kuwagundua watoto waliopewa ujauzito kama wangekuwepo walimu wa kike,” anasema.
Ofisa Mtendaji huyo anasema, tetesi kadhaa zimewahi kuwepo kuhusu baadhi ya wanafunzi wa kike kuwa na ujauzito, lakini hakuna iliyothibitishwa.
“Mwaka jana kulikuwa na tetesi kwamba watoto wawili walikuwa na mimba, lakini baada ya uongozi wa shule kuwapeleka kupima walikutwa hawana, inawezekana kabisa wazazi ama jamaa zao waliwatoa mimba hizo kwa sababu mpaka mwanamume uone dalili kwamba huyu ana mimba, maana yake mama wa watoto tayari watakuwa wamegundua mapema na kuchukua hatua hata za kutoa mimba hizo.
“Ingekuwa rahisi kugundua mapema kama wangekuwepo walimu wa kike maana wao wanazijua dalili tangu mapema,” anasema Bosco.

Uhaba wa walimu
Shule hiyo ni moja kati ya shule tatu za msingi katika Kata ya Malolo ambapo nyingine ni Idodoma na Nzugilo, ambazo zote zimekuwa zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu bila kujali jinsia.
Mwalimu Massawe anasema kwamba, kwa miaka mitatu iliyopita shule hiyo ilikuwa na walimu wanne baada ya mmoja kwenda kusoma, ambapo mzigo wa ufundishaji ulikuwa mkubwa na hivyo kukwamisha maendeleo ya kitaaluma.
“Mimi nimefika hapa Januari, lakini kuna walimu wengine wawili wameongezwa ambapo mmoja ametoka Shule ya Mtejeta iliyoko mjini Mpwapwa na mwingine amejihamisha mwenyewe kutoka Shule ya Kimagai,” alisema.
Uchunguzi umebaini kwamba, licha ya kuongezeka kwa walimu hao watatu, bado shule hiyo inahitaji walimu wawili wa ziada kwani kwa sasa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi shuleni hapo ni watoto 56 kwa mwalimu mmoja, tofauti na uwiano wa kitaifa wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.
Maendeleo ya kitaaluma shuleni hapo yanaonekana pia kuwa duni, kwani kati ya watoto 54 waliomaliza darasa la saba mwaka 2016, ni 21 tu ndio waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Malolo, Bosco Mwaluga, anasema ukosefu wa walimu kwenye shule za msingi za kata hiyo ni changamoto kubwa ambayo inakwamisha maendeleo ya elimu.
“Hapa Malolo ameletwa Mwalimu Massawe ambaye alikuwa Nzugilo, Mwalimu Selemani Saidi kutoka Mtejeta na Mwalimu Emmanuel Kagali, ambaye amejihamisha mwenyewe kutoka Kimagai ili arudi hapa kijijini kwake,” anasema Bosco.
Shule ya Msingi Idodoma yenye wanafunzi 314 inao walimu wanne tu kwa mwaka wa nne sasa, ambapo uwiano ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 79.
Aidha, Shule ya Msingi Nzugilo yenye wanafunzi 507 ina walimu nane ukiwa ni uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 63.

Nyumba za walimu
“Tuna changamoto kubwa pia ya nyumba za walimu, hapa Malolo zipo nyumba tatu tu ambazo haziwatoshi walimu saba waliopo, zinahitajika nyumba nyingine nne,” anasema Mwalimu Massawe.
Hali hiyo, anasema, imewafanya walimu wengine kwenda kupanga mitaani kwa gharama zao wenyewe, jambo ambalo linawaongezea mzigo na gharama za maisha.
Anaongeza kwamba, kukosekana kwa nyumba za uhakika ni kikwazo kingine kinachoweza kukwamisha kuletwa kwa walimu wapya, hasa wa kike, hivyo kuiomba Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha makazi ya walimu yanapewa kipeumbele.
Akizungumzia masuala mengine, Mwalimu Massawe alisema changamoto ya ukosefu wa vitabu vvya kiada na ziada bado ni kubwa, ambapo kwa sasa kitabu kimoja za ziada kinatumiwa na wanafunzi nane badala ya wanafunzi watatu kama Sera ya Elimu na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) inavyoelekeza.
Suala la afya na usafi nalo ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975, ambapo ina matundu nane tu ya vyoo.
“Ni changamoto kubwa kwa sababu kuna wanafunzi 189 wa kiume na 197 wa kike, matundu haya hayatoshi kabisa,” alisema Mwalimu Massawe.

Kwa watoto wa kiume, tundu moja linatakiwa kutumiwa na wanafunzi 25 wakati wasichana 20 wanatakiwa kutumia tundu moja, jambo ambalo katika shule hiyo halipo kwa kuwa wastani tundu moja linatumiwa na wanafunzi 48.

Comments