Featured Post

CHETI CHA ARDHI YA KIJIJI KINAWAPA FURSA WANANCHI KUMILIKI ARDHI

MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI YA KIJIJI - 5

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
MARA mipaka ya kijiji ikishakuwekwa na kupimwa, mamlaka husika (Kamishna wa Ardhi) atatoa Cheti cha Ardhi ya Kijiji kwa Halmashauri ya Kijiji kwa mujibu wa Fungu la 7 (6-12) la Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999.
Hii ni hati muhimu inayopaswa kutunzwa na Halmashauri ya Kijiji ambayo inatumika kumaanisha mamlaka ya Halmashauri ya Kijiji kutawala na kusimamia ardhi ya kijiji.

Cheti cha Ardhi ya Kijiji kinakuwa badala ya Hakimiliki ya Ardhi ya Kijiji zilizotolewa kwa baadhi ya vijiji, ambazo zinapaswa kufutwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999.
Usimamizi wa ardhi ya kijiji ni pamoja na uwekaji na upimaji mipaka ya kijiji, upangaji kwa ushirikishwaji wa matumizi ya ardhi ya kijiji, ugawaji na umilikishaji wa maeneo ya ardhi kwa taasisi na watu binafsi (wanakijiji), kutoa Hatimiliki za Haki za Ardhi za Kimila, na kuanzisha na kutunza Masjala ya Ardhi ya Kijiji, ambayo inapaswa kuwa sehemu ya Masjala ya Ardhi ya Wilaya.

Maana ya Cheti cha Ardhi ya Kijiji
Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 inabatilisha Hatimiliki ya Ardhi ya Kijiji na badala yake Halmashauri ya Kijiji kupewa Cheti cha Ardhi ya Kijiji.
Halmashauri ya Kijiji inapokuwa na Hati ya Kumiliki Ardhi ya Kijiji inamaanisha wanakijiji hawawezi tena kumiliki ardhi ndani ya kijiji hicho.
Vinginevyo itamaanisha kumilikisha ardhi hiyo hiyo kwa mtu au taasisi mbili, yaani hati pandikizi (double allocation) kati ya Halmashauri ya Kijiji na wanakijiji, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Pengine Halmashauri ya Kijiji ikiwa na Hati Miliki ya Ardhi ya Kijiji inaweza kuazimisha (sub-lease) ardhi kwa wanakijiji wake.
Kuazimisha huku hakuna hadhi ya dhamana kwa aliyeazimishwa, bali haki ya kutumia ardhi tu.
Mwenye haki ya dhamana anabakia kuwa mmiliki wa ardhi, yaani Halmashauri ya Kijiji.
Hata hivyo, Halmashauri ya Kijiji haiwezi kutumia hatimiliki ya ardhi ya kijiji chote kama dhamana katika taasisi za fedha, kama benki.
Ikithubutu kufanya hivyo inaweza kutoa fursa kwa benki kunadi ardhi yote ya kijiji, kama Halmashauri ya Kijiji itashindwa kutimiza masharti ya dhamana, kama kushindwa kulipa mkopo.
Kwa kuzingatia matatizo hayo, ndiyo maana Sheria ya Ardhi ya Vijiji imebainisha kwamba, wanaohitaji kutumia hatimiliki ya ardhi kama dhamana ni wanakijiji na wala si Halmashauri ya Kijiji.
Utawala wa kijiji unapaswa kuwa na hadhi ya kuweza kusimamia na kutawala ardhi ya kijiji, kiasi cha kuweza kutoa hatimiliki kwa wanakijiji wake kama anavyofanya Kamishna wa Ardhi kwa Ardhi ya Kawaida.
Hivyo basi, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 inatoa mamlaka kwa Kamishna wa Ardhi kutoa Cheti cha Ardhi ya Kijiji kwa kijiji chochote ambacho mipaka yake imeshakubalika, imeshawekwa, na au kupimwa.

Utoaji wa Cheti
Cheti cha Ardhi ya Kijiji kinatolewa kwa jina la Rais, akikasimu mamlaka yake kwa Halmashauri ya Kijiji kusimamia Ardhi ya Kijiji.
Cheti hiki kinahakikisha kukaliwa na kutumia kwa ardhi ya kijiji na wanakijiji kwa kuzingatia taratibu na kanuni za kimila zinazotumika katika ardhi, ambako kijiji kipo.
Cheti cha Ardhi ya Kijiji kinaandaliwa na Ofisa Ardhi wa Wilaya kwa kutumia Fomu ya Ardhi ya Vijiji Namba 16, kuwekewa mchoro wa mipaka ya kijiji na eneo lake, na kisha kusainiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji na Ofisa Mtendaji wa Kijiji, halafu kusajjiliwa wilayani na kupewa namba ya usajili.

Fomu ya Ardhi ya Vijiji namba 16

Hatimaye Cheti hutumwa kwa Kamishna wa Ardhi kusainiwa na kuwekwa lakiri.
Ofisi ya Kamishna hubaki na nakala moja kwa kumbukumbu, nakala mbili hutumwa kwa wilaya husika, ili nakala moja ibaki katika Masjala ya Ardhi ya Wilaya, nakala nyingine hupelekwa kwenye Masjala ya Ardhi ya Kijiji husika.
Ni wajibu wa Halmashauri ya Kijiji kuangalia na kutunza kwa usalama Cheti cha Ardhi ya Kijiji.
Inapotokea mipaka ya ardhi ya kijiji ikabadilishwa vyovyote vile, ni wajibu wa Halmashauri ya Kijiji kumjulisha mapema Kamishna wa Ardhi mabadiliko hayo.
Vilevile Halmashauri ya Kijiji inapaswa imtumie Kamishna wa Ardhi Cheti cha Ardhi ya Kijiji, ili Kamishna afanye mabadiliko yaliyotokea katika cheti husika. Kwa mintaarafu hiyo, Kamishna wa Ardhi atatunza Daftari ya Ardhi za Vijiji.

Usajili wa Vijiji
Utoaji wa Cheti cha Ardhi ya Kijiji usichanganywe na Usajili wa Vijiji unaofanywa na Msajili wa Vijiji kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 7 ya mwaka 1982.
Usajili wa Kijiji ni uthibitisho wa kuanzishwa kwa kijiji, ambacho mipaka yake inapaswa kutambuliwa na kuandaliwa Cheti cha Ardhi ya Kijiji.
Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 inatambua na kujumuisha mamlaka haya, katika Fungu la 7 (12).

Masjala ya Ardhi ya Wilaya
Samba na wilaya kuanza kushughulikia Vyeti vya Ardhi ya Vijiji, inapaswa vile vile kuwa na Masjala ya Ardhi ya Wilaya itakayohusika na usajili wav yeti hivyo.
Masjala hiyo itahusika pia na usajili wa hatimiliki za kimila kwa mashamba na ardhi ya watu binafsi na taasisi nyinginezo.
Kamishna wa Ardhi ameishatoa maelekezo kwa Halmashauri za Wilaya jinsi ya kuanzisha masjala hizo.
Kesho tutaangalia namna upangaji wa matumizi bora ya ardhi unavyoweza kuepusha migogoro.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974


Comments