Featured Post

WAGOSI WA KAYA WATAMBA, ATAKAYETUSOGELEA TU DAMU ITAMRUKIA!


Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Coastal Union ya jijini Tanga (Wagosi wa Kaya) leo (Jumamosi Septemba 30) itatupa karata ya tatu katika mechi za mzunguko wa kwanza katika Ligi daraja la Kwanza dhidi ya KMC ya jijini hapa.
Wachezaji na viongozi wamejichimbia pasipojulikana ili kukwepa hujuma na kuhakikisha inavuna pointi tatu muhimu katika dimba la Azam Complex, Chamazi ili kujihakikishia inamaliza ligi ikiwa kileleni na kurudi ligi kuu msimu ujao.
Akizungumza na mwandishi wetu msemaji wa timu hiyo kongwe nchini Hafidh Kido, alisema kwa sasa wanajipanga ili kutembeza dozi kwa kila timu itakayokuja mbele yao kwa sababu mchezo wa pili waliocheza na JKT Mlale mjini Songea walipoteza kwa bao 1-0.
“Kwa sasa ni kama Faru au Mbogo tuliojeruhiwa, kitendo cha JKT Mlale kutufunga bao 1-0 kimetushushia hadhi sana kwa sababu Coastal Union ni timu isiyoshikika katika michuano hii na tunaahidi mashabiki wetu hatutarudia makosa tena.
“Tunaanza kwa kuonyesha mfano kwa hawa KMC, watachezea kichapo ili iwe fundisho kwa wengine. Tunataka damu zitakazowatoka ziwarukie wengine kama ishara ya salamu kwao. Chamazi itageuka uwanja wa damu, hatuwatishi lakini tunatoa tahadhari,” alisema Hafidh Kido kwa kujiamini.
Aliongeza kuwa dhamira yao ni kuiona Coastal Union inarudisha heshima yake katika ligi kuu Tanzania bara kwa sababu watu wanaotakiwa kucheza nao kwa sasa wapo ligi kuu.
“Aina ya usajili tuliofanya ni wa ligi kuu si ligi daraja la kwanza, kwa hiyo wakati mwingine tunapata tabu kucheza na hizi timu ndogo. Tunatamani ligi kuu ikisimama tupate mechi za majaribio na timu kama Simba, Yanga, Azam au Mbeya City, wao nadhani wanatutambua vizuri, hakuna aliyewahi kutuchezea nyumbani au ugenini.
“Mambo mengine si ya kusema sana, lakini nawaomba wapenzi wa soka, wale wanaotaka kuangalia soko la kiuhakika waje Chamazi leo (Jumamosi), waone namna vijana wa Kitanga wanavyotandaza soka la uhakika. Hakuna longolongo wala hatusemi mengi lakini habari wataipata,” alisema Kido.
Hadi sasa Wagosi wa Kaya wanashikilia nafasi ya nne (4) ikiwa na pointi tatu kibindoni katika kundi B lenye timu nane ambazo ni Coastal Union yenyewe ya Tanga, KMC(Dar es Salaam), Mawenzi Market (Morogoro), Mbeya Kwanza(Mbeya), Mufindi United (Iringa), JKT Mlale (Ruvuma), Polisi Dar es Salaam (Dar es Salaam) na Polisi Morogoro (Morogoro).
Mechi ya kwanza dhidi ya Mbeya Kwanza katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Coastal Union iliibuka na ushindi wa bao 1-0 kabla ya kupoteza mchezo wa pili dhidi ya JKT Mlale katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Comments