Featured Post

STANISLAV PETROV, ALIYEZUIA VITA VYA NYUKLIA WAKATI WA VITA BARIDI AFARIKI AKIWA NA MIAKA 77



MOSCOW, RUSSIA
OFISA wa zamani wa Jeshi la Muungano wa Usovieti ambaye anasifiwa sana kwa hatua yake ambayo huenda ilizuia vita vya nyuklia kati ya Marekani na muungano huo wakati wa Vita Baridi amefariki dunia akiwa na miaka 77.

Stanislav Petrov alikuwa kwenye zamu katika kituo cha Urusi cha kutoa tahadhari kuhusu nyuklia mapema siku moja mwaka 1983 mitambo ya kompyuta ilipofanya makosa na kutoa tahadhari kwamba kulikuwa na makombora yaliyokuwa yamerushwa na Marekani kuelekea Urusi.
Alichukua uamuzi wa busara kuamua kwamba tahadhari hiyo haikuwa sahihi.
Aidha, hakupiga ripoti kwa wakuu wake.
Kitendo hicho chake, ambacho kilifichuliwa baadaye, huenda kilizuia vita vya nyuklia.
Petrov alifariki dunia akiwa nyumbani kwake Moscow mwezi Mei, lakini taarifa za kifo chake zimefichuliwa wakati huu.
Katika mahojiano na Idhaa ya Kirusi ya BBC mwaka 2013, petrov alisema jinsi alivyopokea taarifa zilizopigwa chapa na kompyuta mapema asubuhi ya 26 Septemba 1983 ambazo zilikuwa zinadokeza kwamba Marekani ilikuwa imerusha makombora kadha.
"Nilikuwa na data zote [kudokeza kwamba lilikuwa shambulio la makombora ambalo lilikuwa linaendelea]. Iwapo ningeituma ripoti hiyo kwa wakubwa wangu, hakuna yeyote ambaye angezitilia shaka," amesema.
"Nilichohitajika kufanya ni kufikia simu; na kupiga simu ya moja kwa moja kwa makamanda wetu wakuu - lakini sikuweza kusongea kwenye simu. Nilijihisi kana kwamba nilikuwa nimekalia kikaangio."
Ingawa kwenye mafunzo yake alikuwa ameelezwa wazi kwamba anafaa kuwasiliana na wakuu wa jeshi la Usovieti mara moja akipokea tahadhari, Petrov badala yake aliamua kumpigia afisa wa zamu katika makao makuu ya jeshi na akasema kulikuwa na hitilafu ya kimitambo. 

Muungano wa Usovieti na Marekani wote wawili walikuwa wameelekezeana silaha nyingi za nyuklia wakati wa Vita Baridi
Iwapo angekuwa amekosea, milipuko ya kwanza ya nyuklia ingetokea dakika chache baadaye.
"Dakika 23 baadaye niligundua kwamba hakukuwa na chochote kilichokuwa kimetendeka. Iwapo lingekuwa shambulio la kweli, basi kufikia wakati huo ningekuwa tayari nimefahamu. Niliweza kupumua," anakumbuka.
Uchunguzi uliofanywa baadaye uligundua kwamba setilaiti za Usovieti zilikuwa zimetambua kimakosa miali ya jua ambayo ilikuwa inaakisi kutoka kwenye mawingu kuwa makombora yaliyokuwa yamerushwa.
Petrov, waliyestaafu akiwa na cheo cha luteni kanali, alifariki dunia 19 Mei lakini habari za kifo chake zilifahamika zaidi mwezi huu, kutokana na simu moja iliyopigwa kibahati.
Mwandaaji wa filamu kutoka Ujerumani, Karl Schumacher, ambaye alifanya habari kuhusu kitendo cha Petrov kufahamika zaidi kimataifa, alimpigia simu kumtakia heri siku ya kuzaliwa kwake mnamo tarehe 7 Septemba.
Hata hivyo, alifahamishwa na mwanawe wa pekee wa kiume wa Petrov, Dmitry Petrov, kwamba alikuwa ameshafariki dunia.
Schumacher alitangaza habari hizo mtandaoni na hapo ndipo zilipoanza kuenea kwenye vyombo vingine vya habari.
CHANZO: BBC

Comments