Featured Post

‘MZEE WA MIUJIZA’ TAMBWE LEYA, NDIYE ALIYEMUIBUA NONDA SHAABAN 'PAPII'

Alikuwepo kwenye mgogoro mkubwa wa mwaka 1976 na mwaka 1994 
Tambwe Leya (kushoto) akiwa na Mangala Tabu Mangara mwaka 1974.
Yanga Yosso ya mwaka 1995. Kutoka kushoto waliosimama kipa Mahmoud Nyalusi, Reuben Mgaza, Nonda Shaaban 'Papii', Sylvatus Ibtahim 'Polisi', Ally Yussuf 'Tigana', Sammy Bitumba Iyela, James Tungaraza na kipa Sadiq Kalokola na kiongozi wa Yanga. Waliochuchumaa kutoka kushoto Mzee Abdallah Ngauja, Bakari Malima 'Jembe Ulaya', Stephen Nyenge, David Mjanja, Mohammed Hussein Daima 'Mmachinga', Salvatory Edward na Benny Luoga.   

Na DANIEL MBEGA
HISTORIA ya Tambwe Leya, mtu aliyejulikana zaidi nchini Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) kama ‘Mzee wa Miujiza’, ilifikia kikomo usiku wa kuamkia Jumamosi, Juni Mosi, 2002. Safari ya mvaa miwani huyo mashuhuri na mgumu wa kuongea ilihitimishwa Juni 3, 2002 baada ya mamia ya wanamichezo kumsindikiza na kumlaza katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Tambwe Leya alifariki katika hospitali kuu ya Jeshi la Wananchi ya Lugalo baada ya kuugua kwa muda mfupi, akiwa anasumbuliwa na maradhi ya tumbo. Hadi mauti yalipomfika, kocha huyo raia wa ‘Zaire’ alikuwa akifundisha timu ya vijana wa umri wa chini ya miaka 17 katika shule ya sekondari ya Makongo inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambako aliwaibua wachezaji kama akina Henry Joseph na wengineo.
Tambwe alizaliwa mwaka 1938 katika kijiji cha Kolwezi katika Jimbo la Katanga lenye utajiri wa madini ya shaba, akiwa anatokea katika kabila la Wasonge. Kocha huyu alikuwa na historia ndefu nay a aina yake katika soka ya Tanzania na nyumbani kwao ‘Zaire’.
Itakumbukwa kuwa, kikosi cha timu ya taifa ya Zaire, Les Leopards, kilichonyakua Kombe la Mataifa Huru ya Afrika na kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Ujerumani Magharibi mwaka 1974 kilikuwa na majina makubwa ya wachezaji waliotokana na juhudi za Tambwe. Miongoni mwao ni golikipa Kazadi na mshambuliaji Etepe Kakoko, ambao aliwasuka kutoka yosso na kuwa nyota waliotisha, akaisuka klabu ya Imana, ambayo katika miaka ya 1970 ilikuwa inaiadhiri vibaya Vita Club ya nchini humo na kutishia ubora wake katika soka ya nchi hiyo.
Tangu alipoingia Yanga mwaka 1974 baada ya kuondoka nchini kwa kocha Dakta Victor Stanculescu wa Romania aliyekuwa amewapika vijana chipukizi, timu hiyo iliweza kuja juu chini ya Tambwe na kufanya maajabu makubwa nchini ikiwa ni pamoja na kutwaa ubingwa wa taifa mwaka huo Jumanne ya Agosti 10, kwa kuwachabanga watani wao wa jadi, Simba, mabao 2-1 katika mechi ya kihistoria kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Si hivyo tu, bali Tambwe aliweza kuiongoza tena timu hiyo ikaichapa Simba mabao 2-0 katika fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar mwaka 1975 na kuivua ubingwa huo, huku kikosi hicho kikiwa kinaundwa na vijana wengi chipukizi aliowapandisha kutoka kikosi cha pili wakiwemo akina Mohammed Rishard ‘Adolf’, Juma Matokeo na wengineo, yakiwa ni matunda aliyoyaacha Dk. Victor.
Tambwe Leya alikuwa na taaluma nyingi. Alikuwa mtaalamu wa masuala ya Bima, alikuwa mchezaji na kisha kwenda kusomea ukocha nchini Brazil na Ufaransa, na zaidi aliwahi kuwa Meneja Utawala, pengine ndiyo maana aliweza kuwadhibiti vilivyo wachezaji katika kila sehemu aliyofundisha na wachezaji wote walikuwa wakimheshimu kwa nidhamu ya hali ya juu na kuyazingatia maelekezo yake.
“Ukitaka kujenga timu yenye nidhamu lazima kwanza wato wote; wachezaji na viongozi, waelewe kwamba, wewe ndiye bosi…vinginevyo unaweza kuwa na wachezaji wazuri lakini kutokana na ukosefu wao wa nidhamu wakaiharibu timu,” alipata kusema enzi ya uhai wake akielezea ni kwa nini wachezaji huheshimu maelekezo yake na kutii kila alilokuwa akiwaambia.
“Wakati nakuja Yanga mwaka 1974 niliikuta timu ina wachezaji wengi wazuri, tena chipukizi ambao walikuwa wamelelewa vizuri sana, lakini walikosa kitu kimoja tu – nidhamu. Kila mmoja alikuwa akijiamulia mwenyewe kufanya atakalo, hata kwenye mazoezi, lakini mimi nikasema kwamba lazima tabia hii ibadilike ndipo tunapoweza kufanya mambo makubwa.”
Mambo yote yalianzia mwaka 1958 wakati Tambwe akiwa na miaka 20 wakati huo, alipojiunga na klabu ya Tout Puissant Englebert (sasa T.P. Mazembe) akiwa mchezaji, ambapo alidumu nayo kwa miaka miwili. Enzi zake alikuwa anamudu kucheza namba zote isipokuwa kukaa langoni tu.
Kutoka Elizabethville (sasa Lubumbashi) ilikokuwa T.P. Englebert, Leya akatimua hadi Leopoldville (sasa Kinshasa) ambako alijiunga na klabu ya Imana ya huko. Baada ya kama mwaka mmoja hivi, Tambwe likawa jina maarufu mjini humo, akiwa tegemeo kubwa la klabu hiyo ya Imana, ambapo aliweza kuitwa kwenye timu ya taifa ya Zaire, Les Leopards (sasa Simba). Mwaka 1963 alilazimika kutundika daruga kutokana na matatizo ya macho, na tangu hapo akaanza kuvaa miwani mpaka mwisho wa uhai wake.
ANAANZA UKOCHA:
Ilikuwa mwaka huo wa 1963 wakati akiwa bado anacheza soka, wakati timu ya taifa ya Ghana, Black Stars – timu iliyokuwa inatisha kweli katika soka ya Afrika enzi hizo – ilipozuru jijini Leopoldville. Timu ya taifa ya Zaire ilipata mkong’oto wa mabao 3-0 kutoka kwa Waghana hao mbele ya Rais (wakati huo alikuwa Joseph Kasavubu). Kipigo hicho kilikuwa kama ncha kali ya kisu moyoni mwa Tambwe, ambaye siku hiyo aliacheza pia.
“Niliamua pale pale kwamba lazima niwe kocha. Kipigo kile hakikuvumilika…watu, watu wetu maelfu kwa maelfu, viongozi wetu, wote walikuwa pale uwanjani. Kwa nini Ghana watuadhiri kiasi kile?" alisema Tambwe katika mahojiano yaliyofanyika mwaka 1974 alipoingia nchini kwa mara ya kwanza.
Ushindi wa Ghana ukamhamasisha Tambwe, ambaye baada ya kutundika daruga kutokana na matatizo ya macho, akaamua kuunda timu ya yosso iliyojulikana kama Doring Matete. Timu hiyo iliundwa na watoto wa shule za msingi ambao hawakuwa na kazi za kufanya katika muda wao wa ziada. Miongoni mwa yosso hao walioibuka na kuwa tegemeo la taifa ni pamoja na Etepe Kakoko, Mavuba, Tubilantu, Kazadi na wengineo ambao mwaka 1974 walibeba bendera ya Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Ujerumani Magharibi wakiwa pia mabingwa wa Afrika wa mwaka huo.
Baada ya timu yake kutwaa ubingwa wa ligi ya yosso klabu ya Imana ikaona kwamba mchezaji wao huyo wa zamani angeweza kuwasaidia kama kocha. Mwaka 1966 wakamwita na kumpa mikoba na nyota wa kwanza kuibuka chini yake alikuwa Mayanga, mpachika mabao mashuhuri wa timu ya taifa ya Zaire.
Wakati huo Tambwe, ambaye tafsiri yake ni Simba katika kabila la Wasonge, alikuwa akihudhuria mafunzo ya ukocha na elimu ya viungo katika chuo kimoja mjini Kinshasa kilichokuwa chini ya Elonga Emmanuel, ambaye katika miaka ya 1970 alikuwa kocha wa Imana.
Baada ya T.P. Englebert kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo mwaka 1967 iliyokuwa inahusika na michezo ikamwajiri kama kocha ili kuinoa kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika. Wakati huo pia alikuwa mwajiriwa wa kampuni ya Kilo Moto Iron Ore kama Meneja Utawala.
Katika klabu ya Englebert, Tambwe aliwafundisha nyota kama Bwanga, Kazadi, Mukombo, Chinabu, Kalambai na Kunesh. Pia kulikuwa na Said na Kalala, aliowafundisha kule Imana. Umaarufu wa nyota hao ulikuja kuanzia mwaka huo ambapo Englebert ilitwaa ubingwa wa Afrika, na ndipo Tambwe alipoanza kuwaniwa kutokana na kuongoza vyema timu hiyo kwenye michuano hiyo mikubwa kabisa ya klabu za Afrika, ambayo sasa inajulikana kama Ligi ya Mabingwa Afrika. Wakati alipoiongoza tena Englebert kutwaa ubingwa huo mwaka 1968, timu nyingi zikaanza kumwania. Zote zikitaka akazifundishe, lakini akakataa.
Tambwe aliiacha Mazembe mwaka 1970 na kuamua kufanya shughuli zake binafsi. Baadaye akarejea tena uwanjani kuifundisha Imana katika msimu wa 1972-73, ambapo iliichapa Vita Club mabao 2-1 katika mechi mbili za ligi, kabla ya kupata nafasi ya kwenda kusomea ukocha nchini Brazil.
Alikaa huko kwa mwaka mmoja, na kutokana na ukali wake wa masomo darasani, aliweza kuibuka wa kwanza kati ya wanafunzi watano waliokuwa wakichukua mafunzo hayo. Kutokana na ‘kupasua’ mtihani vizuri, Wabrazili wakamshawishi abakie huko ili azifundishe klabu za huko, lakini akakataa.
Mwaka 1974 akakutana na viongozi wawili wa Yanga – Joseph Mbwambo na Pazi – wakati timu hiyo ilipokwenda kuzuru Brazil, ambao walimshawishi aje Tanzania kuinoa timu hiyo baada ya mkataba wa Dk. Victor kumalizika, naye akakubali na mwaka huo akaisaidia timu hiyo ya Jangwani kurejesha taji lao la ubingwa wa Tanzania ililolipoteza kwa Simba mwaka 1973.
Tambwe aliweza kuwapandisha wachezaji kadhaa kutoka timu ya pili ya Yanga, Young Boys, ili kuchukua nafasi za wakongwe kama akina Omar kapera, Hassan Gobbos na wengineo, na kwa kweli timu hiyo ilikuwa kali sana.
AONDOKA NCHINI 
Hata hivyo, mgogoro mkubwa ulioibuka mwaka 1976 baada ya timu hiyo kushindwa kutetea ubingwa wa Afrika Mashariki na kati kule Mombasa, Kenya ulisababisha kocha huyo aondoke nchini. Mgogoro huo ulianza kufukuta kabla timu hiyo haijaondoka kwenda Mombasa, na wakati ikiwa huko ukapamba moto ambapo uamuzi ukatolewa na wanachama wa kumfukuza Katibu Mkuu wa wakati huo, Mohammed Misanga, wakati akiwa bado huko huko Mombasa. Timu ikaendelea hadi fainali na kutolewa na Luo Union (baadaye Re-Union) ya huko.
Kizaazaa kikubwa kilitokea wakati timu iliporejea nchini. Uongozi uliamua kuchukua basi la Ikarus na kulipeleka uwanja wa ndege ili wachezaji wakifika wapande hadi klabuni, lakini walipofika uwanjani, wachezaji wakagoma kupanda na badala yake kutumia usafiri mwingine.
Katika ripoti yake alisema kwamba wachezaji hawakujituma, walikuwa kwenye mgomo baridi, hivyo uongozi ukaamua kuwatimua wachezaji nyota 20 waliokwenda Morogoro kujiunga na Young Africans ya huko waliyoibadili jina na kuiita Nyota Afrika kabla ya kurejea Dar es Salaam na kuunda klabu ya Pan African chini ya Mangara Tabu Mangara.
Mgawanyiko huo pia ukawagawa wanachama, abapo kundi la makabwela lilijulikana kama Yanga Kandambili na lile la mabwanyenye lilijulikana kama Yanga Raizoni, na hili ndilo lililokwenda kuanzisha timu ya Pan African.
Baada ya kuondoka kwa wachezaji hao, uongozi ukamuuliza Tambwe kama alikuwa na uwezo wa kuunda timu, yeye akasema ‘nitaunda kikosi imara kwa kutumia wachezaji wa timu B’. Kweli akafanikiwa kuisuka upya timu hiyo ambayo ilishiriki kwenye ligi ya wilaya ya Ilala na Jumamosi Machi 20, mwaka huo ikafungwa na Simba mabao 2-1. Wachezaji waliokuwepo walikuwa Isega Isindani, Charles Mwanga, Zitto Kiaratu, Selemani Jongo, Sudi Pipino, Twaha Shaaban ‘Ufunguo’, Shaaban Katwila, Ibrahim Kiswabi, Ahmad Omar, Burhani Hemedi, nahodha Ramadhan Mwinda ‘Maajabu’ na wengineo.
Uwezo wake wa kujenga timu kwa muda mfupi uliwashtua wengi na akaonekana kwamba atakuwa tishio. Kwa sababu ambazo serikali yenyewe ilizijua, ikaamua aondoke nchini haraka sana pamoja na aliyekuwa kocha wa Simba, Nabby Camara kutoka Guinea. Inaelezwa kwamba wawili hao walihisiwa kwamba huenda ni majasusi wa CIA, hivyo wakawa wameondolewa kwa sababu za kiusalama. Baada ya kurejea kwao Zaire alifundisha klabu kadhaa pamoja na timu ya taifa ya nchi hiyo.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Dk. Jabir Mohammed katundu na Katibu Mkuu George ‘Castro’ Mpondela, uliamua kumwita tena mwishoni mwa mwaka 1993 ili aje asaidiane na Mrundi Nzoysabah Tauzany aliyeiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala, Uganda, mapema mwaka huo.
Yanga ilikuwa imekamilika sana wakati huo, ikiwa na wachezaji nyota kama akina Sanifu Lazaro, Zamoyoni Mogella, Willy Mtendawema, James Tungaraza, Said Mwamba Kizota, Edibily Lunyamila, Mohammed Hussein na wengineo, ingawa si nyota hao wote waliokuwemo kwenye kikosi cha mwaka 1994, bado ilionekana kuwa tishio hata pale ilipokwenda kutetea ubingwa wake mjini Khartoum, Sudan mwaka 1994.
Lakini kwa bahati mbaya ilitolewa kwenye nusu fainali na kuutema ubingwa huo, ambao mwaka huo ulichukuliwa na El-Merreikh ya Sudan. Tangu hapo, kama ilivyokuwa mwaka 1976, wingu nene la mgogoro likatanda tena Jangwani, tena Tambwe yule yule akiwemo klabuni, ambapo lawama zilikwenda kwa wachezaji na baadhi ya wafadhili wa klabu hiyo, hususan Abbas Gulamali, ambaye ilidaiwa aliihujumu timu isitetee vyema ubingwa wake kutokana na uongozi wa klabu hiyo kuwapiga vita wafadhili.
Vurugu kubwa zikaibuka baada ya Yanga kufungwa na Simba mabao 4-1 Julai 2, 1994 kwenye mechi ya marudiano ya ligi daraja la kwanza Tanzania Bara, ambao ilionekana dhahiri wachezaji walicheza chini ya kiwango. Baada ya matokeo hayo baadhi ya wanachama wakalichoma moto duka la Gulamali lililokuwa kwenye Barabara ya Morogoro na kuwapiga marufuku wafadhili hao kukanyaga Jangwani.
Uongozi ‘ukatafuta mchawi’ na baada ya kuridhika ukaamua kuwafukuza wachezaji kadhaa nyota, wakiwemo Said Mwamba Kizota na Thomas Kipese waliokwenda Simba, Edibily Lunyamila na Nico Bambaga wakatimkia Malindi ya Zanzibar, na wengine kama Philemon ‘Fumo’ Felician wakatemwa pia.
Tambwe, ambaye alikuwa upande wa uongozi, alituliza akili na kuamua kuwasuka vijana wa timu B ya Yanga, Black Stars, na kuwapandisha kwa ajili ya msimu wa 1995/96. miongoni mwa wachezaji hao ni Sylvatus Ibrahim ‘Polisi’, Anwar Awadh Gessan, Mzee Abdallah Ngauja, Maalim Salehe, Mkongo Shaaban Nonda ‘Papii’ ambaye alikuja kuwa nyota wa kimataifa katika klabu za Ulaya kama Monaco na Rennes za Ufaransa, FC Zurich ya Uswisi alikoibuka kuwa mfungaji bora wa kwanza Mwafrika kwenye ligi ya nchi hiyo, Blackburn Rovers ya Uingereza na nyinginezo.
Kikosi hicho, ambacho mwaka 1995 kiliitwa ‘yosso’ kutokana na kujaa sura nyingi chipukizi, kiliweza kuigomea Simba katika mchezo wa kwanza wa ligi ya Tanzania Bara kwa kutoka suluhu. Simba ya mwaka huo ilikuwa ikijulikana kama ‘Shikamoo’ kwa kusajili wazee.

Kikosi cha Yanga (Yosso) cha mwaka 1995. Kutoka kushoto waliosimama ni meneja wa timu Nurdin, kipa Mahmoud Nyalusi, Kenneth Mkapa, Reuben Mgaza, Sylvatus Ibtahim 'Polisi', Dominic Mbawala, Ally Jabir Katundu, Sadiq Kalokola, kocha mkuu Tambwe Leya, kocha msaidizi Nzoysabah Tauzany. Waliochuchumaa ni Maalim Salehe 'Romario' James Tungaraza 'Boli Zozo', Ally Yussuf 'Tigana', Anwar Awadh Gessan, Mzee Abdallah Ngauja, Mohammed Hussein Daima 'Mmachinga' na Bakari Malima 'Jembe Ulaya.
Hali haikuwa nzuri katika klabu ya Yanga mwaka 1996, hivyo Nzoyisabah Tauzany akaamua kutimkia Maji Maji ya Songea na baadaye Tambwe Leya akatimkia Visiwani Zanzibar kuifundisha timu ya Small Simba, huku wakiwa wanaidai Yanga malimbikizo ya mishahara yao.
Tambwe alikaa na Small Simba kwa misimu kadhaa kabla ya kuanza kuinoa Mafunzo ya Zanzibar pia, ambayo aliipandisha hadi ikafanikiwa kushiriki Ligi Kuu ya Muungano mwaka 2000, kabla ya kuondoka na kuanza kuifundisha Miembeni ya huko pia, ambayo mpaka anaondoka mwaka 2001 alikuwa akiidai malimbikizo ya mishahara yake.
Uongozi wa shule ya Makongo, ambayo inasifika kutokana na kukuza vipaji vya wanamichezo nchini, ulimwita kocha huyo mwaka huo 2001 ili asaidiane na Mnigeria Prince Ernest Gbaar-Mokake, kuwanoa vijana wenye umri chini ya miaka 17 na 20 waliokuwa wakiunda timu za taifa za umri huo. Hadi kocha huyo anafariki alikuwa akiendelea kukuza vipaji vya vijana hao.

Imeandaliwa na mtandao wa www.maendeleovijijini.blogspot.com

Tafadhali, ukinakili makala haya kwa matumizi yoyote yale ni lazima ueleze chanzo kuwa ni mtandao wa MAENDELEO VIJIJINI

Comments