Featured Post

KUIBUKA NA KUTOWEKA KWA WASHIRIKA TANZANIA STARS ‘WATUNJATANJATA’

Iliibuka na ‘Penzi la Ulaghai’, ikatoweka na ‘Penzi la Kusuasua’
Komandoo Hamza Kalala 'Mzee wa Madongo'

Na Daniel Mbega

“YAMENIKUTA miyeee,
Yamenikuta kijana mwenzenu nipeni pole miye,
Usiku sikulala hoi jama nikifikiria vituko.
Nimekanyaga moto,
Kwa kujitosa kwa mchumba aliyetingisha mji eee,
Nikidhani nimepata oooh jama kumbe nimepatikana x2

Ama kweli kizuri hakikosi kasoro mamaa eeeh,
Kwa muda mrefu nilioishi naye,
Nilimpenda sana, lakini mwenzangu pendo lake,
Lilikuwa la ulaghai, la ulaghai mama x2

Swadakta kabisa. Hapana shaka yoyote kwamba mashairi haya yanawakumbusha mbali wapenzi wa muziki wa dansi enzi zile wakati bendi la muziki wa dansi zilipokuwa kwenye chati zikichuana na disco kutoa burudani.
Ni enzi ambazo muziki wa kizazi kipya au ‘Bongo Flava’ ulikuwa haujaanza rasmi. Muziki wa dansi ulikuwa kileleni na mashabiki walikuwa na ushindani kama ule wa kwenye kandanda. Haikuwa ajabu kukuta vikundi vya mashabiki vikilumbana, ukiingia kwenye kumbi za starehe utakuta shabiki akicheza na chupa mkononi akiwa kifua wazi, shati amelifutika kwenye mfuko wa nyuma wa suruali. Hapo ole wako kivuli chako kingie kwenye eneo analochezea. Ni ngumi tu!
Basi mashairi hayo ya wimbo ‘Penzi la Ulaghai’ ni ya kukumbukwa zaidi kwa wale mashabiki wa bendi ya Washirika Tanzania Stars, maarufu ‘Watunjatanjata’, kwa vile ndicho kibao cha kwanza kabisa kufyatuliwa baada ya bendi hiyo kubadili jina kutoka lile la zamani la Tanzania Stars, ambayo makao yake makuu yalikuwa Maggot, mahali ambapo hivi sasa pana ghorofa kubwa jirani na makao makuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) jijini Dar es Salaam.

Ukiwa ni utunzi wa Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’, ambaye aliimba akishirikiana na Edgar Shekidele maarufu Eddy Sheggy au ‘Fast Mover’ (wote kwa sasa ni marehemu), kibao hiki kilileta sura mpya katika bendi za muziki wa dansi Tanzania kiasi cha kuziweka roho juu bendi kongwe, hususan Vijana Jazz Orchestra, ambako ndiko chimbuko la wanamuziki waliokuwa wanaunda bendi hiyo wakati huo.
Wengi walidai kwamba, Sauti ya Zege alitunga kibao hicho kwa ajili ya uiponda bendi ya Vijana Jazz baada ya wao kuihama, lakini kulingana na mahojiano binafsi baina yangu na yeye mwaka 1994, alisema kibao hicho alitunga mahsusi kwa ajili ya rafiki yake Julius Nyaisanga ‘Uncle J’ (sasa ni marehemu pia) kutokana na masahibu yaliyompata.

ILIKOANZIA…
Bendi ya Washirika Tanzania Stars ilianzishwa rasmi Agosti 1986 ikiwa inarithi jina la bendi ya Tanzania Stars ambayo ilikuwa chini ya Vyama vya Msingi vya Ushirika ikiwa inafanya maonyesho yake kwenye Hoteli ya Maggot pale Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam. Bendi hiyo ilibadili jina mara tu ilipoanza kumilikiwa na Muungano wa Vyama vya Ushirika Tanzania (Cooperatives Union of Tanzania - CUT).
Tanzania Stars iliyokuwa imeongezewa nguvu kwa kuwachukua wanamuziki kadhaa kutoka Vijana Jazz kama Adam Bakari, Eddy Sheggy, ‘Komandoo’ Hamza Kalala na fundi mitambo Salum Pongwe, ilishindwa kuvilipia vyombo vilivyokuwa vimeletwa na Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata) na hivyo kuamua kuomba msaada kutoka CUT.
Vifaa hivyo viliagizwa na Chamudata ambapo vilikuwa miongoni mwa seti nne. Seti nyingine zilichukuliwa na Mwenge Jazz ‘Paselepa’, Polisi Jazz ‘Vanga Vanga’ na Kurugenzi Jazz.
Huo ulikuwa ni wakati wa ‘uhai’ wa Chamudata chini ya uenyekiti wa Kassim Said Mapili, ambapo chama kilikuwa na nguvu kweli kweli tofauti na sasa ambapo kimedorora.
CUT ilitoa fedha hizo kwa makubaliano kwamba zitakuwa zikilipwa kidogo kidogo, lakini bendi hiyo haikuweza kutimiza ahadi hiyo kutokana na mapato yake kuwa hafifu. Ndipo Hamza Kalala akamwendea Mwenyekiti wa CUT, Phillip Ndaki na Katibu wake, David Holela, na kuwapa wazo la kuanzisha bendi, ambalo lilikubaliwa.
Wanamuziki waliokuwa wakiunda Washirika Tanzania Stars ni Adam Bakari, Hamza Kalala, Eddy Sheggy na fundi mitambo Salum Pongwe (wote kutoka Vijana Jazz), Christian Sheggy, Madaraka Morris, Noordin Athumani, Hassan Athumani, Kejeli Mfaume, Abdul Salvador ‘Father Kidevu’ na Juma Shaaban.
Abdul Salvador 'Father Kidevu'
Kama nilivyoeleza hapo awali, kibao cha kwanza walichoibuka nacho ni ‘Penzi la Ulaghai’ kilichoimbwa na Eddy Sheggy katika sauti ya kwanza na Adam Bakari katika sauti ya tatu. Gitaa la solo lilikuwa likicharazwa na Hamza Kalala, solo namba mbili alipiga Robert Mabrish, Noordin Athumani alipiga rhythm, gitaa la bass lilipigwa na Juma Shaaban, Hassan Athumani (tumba), Kejeli Mfaume (drums) na kinanda kilikuwa kinapapaswa na Abdul Salvador.
Onyesho la kwanza la bendi hiyo lilifanyika Novemba 1986 kwenye ukumbi wa Dodoma Hotel kwa ajili ya kuwaburudisha Wabunge na liliingiza jumla ya Shs. 17,000, yakiwa ni mapato makubwa zaidi kuingizwa na bendi yoyote ya dansi nchini kwa wakati huo.
Wakati huo Eddy Sheggy naye aliibuka na kibao chake cha ‘Kisa’, ambacho nacho kilikuwa matata sana.
Tazama mashairi ya wimbo wa ‘Nimekusamehe’:

“Nimekusamehe lakini sitokusahau,
Visa ulivyonitendea Kalala ee eeh, Visa ulivyonitendea Kalala ee eeh

Ulinikana ee wakati mi na shida,
Ukasahau yote tuliyofanya nawe,
Wakati unaelewa hakuna Komando wa shida,
Wakati unaelewa hakuna Bingwa wa shida,
Leo nakukumbusha shida huja na kupita,
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo kakaa
Mimi nakusamehe lakini sitokusahau,

Lalalala lalalala laaaa, lalalala lalalala mimi nimekusamehee,
Lalalala lalalala laaaa, lalalala lalalala mimi nimekusamehee

Rafiki wa kweli ni yule asiyekutupa ee
Kwenye dhiki na faraja mko wote mko wote,
Kwenye dhiki na faraja oooh oooh,
Uliniacha nateseka peke yangu peke yangu,
Pasipo msaada wowote kaka oo oooh,
Pasipo msaada wowote kaka oo oooh,
Lakini Mola muweza wa yote (wa yote)
Kaninusuru na matatizo yamepita o kaka,
Kweli nimekusamehe lakini sitokusahau,
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo kaka,
Kweli nimekusamehe lakini sitokusahau,
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo kaka,

Lalalala lalalala laaaa, lalalala lalalala mimi nimekusamehee,
Lalalala lalalala laaaa, lalalala lalalala mimi nimekusamehee

Naam. Hiyo ilikuwa ni reggae ndani ya dansi, mwanakwetu. Kibao hicho kisemacho ‘Nimekusamehe Lakini Sitokusahau’, kilichopigwa katika miondoko ya reggae, ulikuwa ni utunzi wake Komandoo Hamza Kalala, ambaye inaelezwa kwamba alitunga makusudi kueleza msimamo wake kuwa alikuwa amemsamehe ‘rafiki yake’ Hemedi Maneti Ulaya, kiongozi wa Vijana Jazz enzi hizo.
Eddy Sheggy
Inaelezwa kwamba, Komando Kalala aliondoka Vijana Jazz baada ya Maneti kumpata Bwa’mdogo Shabani Yohana ‘Wanted’ kutoka bendi ya Tancut Almasi Orchestra ya Iringa.
Hiyo ilikuja baada ya Kalala kupata ajali ya gari na kuruhusiwa kupumzika kwa muda wa miezi mitatu, ambapo Maneti alilazimika kumtafuta mpiga solo mwingine. Wanted alikuwa mtundu wa gitaa, halafu ikatokea akawa anamudu kupiga nyimbo zote ambazo Kalala alikuwa anazipiga.
Mara baada ya kupata nafuu na kurejea, inasemekana Maneti alimkataza Kalala asipande jukwaani na muda mwingi akautumia kama ‘mtazamaji’ tu. Komandoo akaamua kuondoka na kujiunga na Tanzania Stars hadi kuanzisha Washirika.
Mara nyingi kisa hiki Komando Kalala huwa hapendi kukizungumzia… “Yaliyopita yamepita…” ndivyo husema daima.
Washirika Tanzania Stars iliendelea kujipatia umaarufu mkubwa hasa baada ya kuibuka na vibao ningine maridadi kama ‘Julie’ ukiwa utunzi wake Madaraka Morris, vibao vya ‘Watoto Wamekuja Juu’ na ‘Mjumbe Nimekuja’ ukiwa ni utunzi wa Sauti ya Zege.
Wakati huo ilikuwa pia imewapata wanamuziki wengine mahiri kama Mhina Panduka 'Toto Tundu', Emma Mkelo 'Lady Champion', na wengineo.

AWAMU YA PILI NA ‘NJATA ONE’
Ikiwa chini ya CUT, bendi hiyo ilikuwa ikishiriki kwenye mambo mengi, yakiwemo kuhamasisha shughuli za ushirika, kwenye sherehe mbalimbali kama za Wakulima, sherehe za Chama cha Mapinduzi enzi hizo za mfumo wa serikali ya chama kimoja, na shughuli mbalimbali za serikali.
Kutokana na bendi hiyo kuwa kipenzi cha wengi na kukusanya mashabiki lukuki kwenye maonyesho yao, viongozi wa CUT wakaifanya kitegauchumi kwa kukusanya mapato mengi. Hata hivyo, badala ya kumpa ng’ombe majani na maji ndipo umkamue, wao walikuwa ‘wanaikamua’ bendi bila kuihudumia. Walikusanya mapato yote na kusahau kuwapa wanamuziki haki zao, ambao ndio wazalishaji.
Hali hiyo ikawalazimu baadhi ya wanamuziki kuondoka ambapo Eddy Sheggy na mdogo wake Christian walikwenda Bima Lee Orchestra, Hamza Kalala alikuwa ametoka mapema mwaka 1988 na kunzisha bendi yake ya HK & Bantu Group na Abdul Salvador akaanzisha bendi yake ya The Hisia Sounds. Mgawanyiko huo ulitokea mwaka 1991.
Awamu hii ya pili ya wanamuziki waliosalia ikaifanya bendi ibadilishe hata mtindo wake, ambapo badala ya Watunjatanjata, ambao maana yake ni ‘Wakulima Tuondoe Njaa Tanzania’, sasa ikaibuka na mtindo wa ‘Njata One’.
Pamoja na kubakia na wanamuziki wengi, bendi hiyo ikaongezewa nguvu na wanamuziki kadhaa wakiwemo Mohammed Shaweji kutoka Vijana Jazz na Toffi Mvambe kutoka Super Matimila.
Vibao kadhaa vikatungwa ambapo Adam Bakari akaibuka na vibao viwili – ‘Penzi la Kusuasua’ na ‘Utamaduni’, ambavyo kwa hakika vilionekana kama ndiyo mwisho wa bendi hiyo.

AWAMU YA TATU
Mambo yakenda yakiongezeka! Lakini si kwa mema. Kizaazaa kwenye bendi hiyo kikatokea mwaka 1993 wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambao mara nyingi huwa ni likizo kwa wasanii wote kutokana na watu wengi kufunga, hususan waumini wa Kiislamu, hivyo burudani zote hupungua.
Wanamuziki wa bendi hiyo walipoanza kudai ‘mafao’ yao ili waende likizo, viongozi wa Ushirika wakaweka ngumu na kutaka waendelee kutumbuiza!
Wanamuziki walijitahidi kuuelewesha uongozi kwamba kipindi hicho mapato huwa haba kutokana na wapenzi wengi wa dansi kuwa katika funga ya Ramadhan. Lakini viongozi hao hawakusikia la Muadhini wala Mnadi Swala! Wakwaambia wanamuziki, kwamba mlango uko wazi, anayetaka kuondoka aondoke, anayetaka kubaki, apige kazi kama kawaida!
Naam. Waliobaki wakabaki, walioondoka wakaondoka!
Katika mahojiano yangu na Adam Bakari mwaka 1994, mwanamuziki huyo alisema kwamba aliamua kumwendea rafiki yake aitwaye Mwakibinga na kumshawishi waanzishe bendi, naye bila hiyana akaridhia na kutafuta vyombo Sinza kwa Mzee Mbaga, ambavyo walivinunua kwa Shs. 2 milioni tu.
Kama masikhara vile, wakaanzisha bendi ya MCA International mwaka 1994, ambayo iliundwa na yeye Sauti ya Zege, Said Makelele (tarumbeta), Abdallah Kimeza (sax), Noordin Athumani (rhythm), George Kessy Omojo (bass), na Kassim Rashid Kizunga (solo), ambaye alikuwa amechukua nafasi ya Kalala kule Washirika katika awamu ya pili. Bendi ya MCA International ikaweka kambi yake Bagamoyo.
Washirika Tanzania Stars ikabaki ikisuasua tu pamoja na jukumu la kuiendeleza kukabidhiwa Zahir Ally Zorro na Hassan Show. Zorro akaibuka na kibao cha ‘Mikufu ya Dhahabu’, lakini juhudi zake hazikuzaa matunda na hatimaye bendi hiyo ikatoweka kwenye anga la muziki wa dansi.
Baada ya serikali kuvunja Vyama vya Ushirika na kuamuru kila mkoa ujitegemee, CUT ikaamua kuja na mtindo wa kuiunda au kuikusanya bendi hiyo kila mwaka inapokaribia sikukuu ya Wakulima (Nane Nane), ambao walikuwa wakiwashawishi baadhi ya wanamuziki waliopata kuimbia bendi hiyo na kwenda kwenye sherehe hizo.
Hata hivyo, juhudi hizo zilikoma mwaka mwaka 1996 na mpaka sasa hakuna anayeikumba. Imekufa kama zilivyokufa Urafiki Jazz, UDA Jazz, Bima Lee Orchestra, na nyinginezo zilizokuwa zikimilikiwa na mashirika ya umma.
Looh! Kweli lilikuwa ni penzi la ulaghai!


Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Ukinakili tafadhali taja chanzo hiki.

Comments