Featured Post

KABEYA CHIBANGU BADU ALIWAHI KUWA MUME WA NURU MHINA 'BABY WHITE'


Kabeya Chibangu Badu, maarufu zaidi tu kama Kabeya Badu (alizaliwa Januari 22, 1945 Likasi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) alikuwa mwanamuziki wa Congo aliyezamia nchini Tanzania ambako ndiko alikopata umaarufu zaidi kuliko nchi yake ya asili.
Na akiwa Tanzania, ambako pia aliwahi kumuoa mwanamuziki wa Nuru Mhina 'Baby White', ndiko alikojenga maisha yake na familia kwa ujumla.

Maisha yake ya awali
Elimu ya msingi aliipata katika shule ya Ecole Officialle Laique de Kolwezi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (wakati huo ikiitwa Congo Leopoldville) na kuhitimu mwaka 1959.
Kabeya alianza tangu akiwa mdogo na alipopata umri wa kwenda kanisani, akajiunga katika kwaya akiwa anaimba nyimbo za Injili.
Ni huko kanisani ndiko alikojifunza jinsi ya kutengeneza ‘melody’ na baadaye mwaka 1963, akiwa anajiamini kwamba anaweza kufanya muziki, alikwenda kujiunga na bendi ya muziki wa dansi ya Ricco Jazz, iliyokuwa katika Wilaya ya Kolwezi.
Akiwa Kolwezi, mbali ya kufanya muziki, Kabeya alijiunga na chuo cha ufundi ambako alichukua ufundi seremala na uashi.
“Tangu nikiwa mdogo, nilipenda sana nyimbo na uimbaji wa Tabu Ley Rochereau na Joseph Kabaselle ‘Le Grand Kalle’, nikatamani siku moja nifikie hadhi yao,” aliwahi kukaririwa akisema enzi ya uhai wake katika mojawapo ya mahojiano yake na wanahabari.
Familiya yake ilijitahidi kumpa moyo ili aweze kufanya vizuri katika muziki, hivyo ilimshauri Kabeya kujifunza lugha ya Kifaransa ambayo inazungumzwa nchini mwao.
Kabeya alikubaliana na ushauri huo na aliingia katika chuo kilichokuwa kikimilikiwa na dhehebu la Protestant huko Kananga. Kiu ya Kabeya ilipozwa wakati alipopokea cheti baada ya kufuzu somo hilo la Kifaransa.
Harakati za Kabeya Badu za kutafuta maisha zilimfikisha kufanya kazi katika gazeti moja la Reality Congolese la mjini Kananga, akiwa kwenye kitengo cha usambazaji mwaka 1967.
“Baada ya miaka miwili kupita, mmiliki wa gazeti hilo alikamatwa baada ya gazeti hilo kuandika habari zilizomuudhi rais wa wakati huo Mobutu Sese Seko, hatma yake gazeti likafungiwa, tukakosa kazi,” alipata kueleza.
Lakini huo haukuwa mwisho wa maisha, kwani mwaka huo huo Kabeya alianza rasmi safari yake ya muziki ambapo alijiunga na bendi ya Lupe Jazz kabla ya kuhama na kujiunga na bendi nyingine ya Amide Success.
Hakuishia hapo, kwani aliondoka tena na kujiunga na bendi ya Santa Fee kabla ya kuelekea katika bendi ya Lupina Nationale, ambako alikutana na Kasongo Mpinda ‘Clayton’ huko Kananga.
Utulivu katika bendi kwake haukuwepo kabisa. Aliondoka tena kwenda kujiunga katika bendi ya Lupe Revolution, iliyokuwa ya vijana kama yeye.
Jina na sifa za uimbaji wake zikazagaa ndipo alipochukuliwa na Omer Baba Gaston Ilunga wa Ilunga katika bendi yake ya Baba Nationale mwezi Septemba 1968.
Mwaka 1970, Kabeya alishawishika kwenda kutafuta ajira mjini Kinshasa. Alibahatika kupata ajira katika bendi ambayo baadaye akagundua kwamba ilimpa ahadi za uongo za maslahi, naye akaachana nayo.
Kati ya mwaka 1971 na 1972 Kabeya alipiga muziki katika bendi ya Festival du Zaire katika jiji la Kinshasa.
Kabeya alirudi Likasi mwaka huo huo wa 1972 na kujiunga na bendi ya Safari Nkoi baada ya kuitwa na mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’. Katika bendi hiyo pia aliwakuta wanamuziki wengine magwiji Freddie Ndala Kasheba na Baziano Bwetii. Yeye na King Kiki walikuwa wamesoma darasa moja katika shule ya msingi ya shule ya Ecole Officialle Laique de Kolwezi, ambako walihitimu mwaka 1959.
“Tangu tukiwa vijana tulikuwa tukielewana sana na Kiki, ndiyo sababu nimekuwa naye sambamba tukienda sehemu mbalimbali pamoja au yeye ananiita,” Kabeya alisema enzi ya uhai wake alipohojiana na mwandishi mkongwe wa burudani Rashid Mtagaluka.
Hata wakati walipokuwa Kolwezi wakipiga muziki katika bendi ya Safari Nkoi, walipanga nyumba moja na walichangia bajeti ya chakula kwa pamoja kila mwisho wa mwezi.
Mwaka 1973 uongozi wa Safari Nkoi ulianza kuwafanyia ‘mtimanyongo’ wanamuziki wake akiwemo King Kiki ambaye hata hivyo aligundua mapema hali hiyo, akamshawishi Kabeya kuondoka na kwenda kuanzisha bendi yao.
Lakini kabla hawajaazisha bendi yao, akajitokeza tajiri mmoja aliyejulikana kwa jina la Paradiso, akimtaka Kiki kwenda Lubumbashi kuanzisha bendi yake. Kiki hakumwacha Kabeya, mwaka 1974 wakaenda Lubumbashi kuunda bendi ya tajiri huyo ya Buka Buka Mabele, lakini ukiritimba wa tajiri huyo ukasababisha bendi hiyo kufa baada ya miezi sita tu.
Baada ya kufa kwa bendi hiyo, mwishoni mwa mwaka 1974 Kiki aliamua kwenda Kinshasa lakini kabla hajaondoka, aliwashawishi Kabeya na wanamuziki wenzake warejee Safari Nkoi. Walikubali ushauri huo nao wakarejea na kupokelewa na uongozi wa Safari Nkoi kwa mara nyingine tena. Kwa kipindi hicho akiwa Safari Nkoi, Kabeya akawa na mawasiliano ya karibu na Kiki akimshawishi kurudi Safari Nkoi kwa vile hali ya utulivu katika bendi ilikuwa imeimarika.
King Kiki alirejea Lubumbashi mwaka 1976, akitokea Kinshasa pasipo kumafamamisha mtu yeyote.
Walikuwa wanapiga muziki katika ukumbi mmoja wa Rele Night Club   mjini Lubumbashi, ghafla Kiki akapanda jukwaani na kushika ‘mic’ akaanza kuimba. Wote wakashikwa na butwaa wakimuona kama ‘shetani’ aliyetua kimiujiza jukwaani.
Mwaka 1977 Kiki alifuatwa na Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’ aliyetokea Marquis du Zaire iliyokuwa nchini Tanzania. Kiki alimuuliza Mzee Paul kama wanamuziki waliokuwepo Marquis du Zaire walikuwa wanakidhi viwango. Mzee Paul alijibu kwa wasiwasi na kupendekeza bora kuchukua wanamuziki wengine huko Congo. Kiki alipendekeza wanamuziki wa kuondoka naye kwenda Tanzania akiwemo Kanku Kelly Kashama (mpuliza saxophone), Mutombo Lufungula Sozy ‘Adios’, Ilunga Banza ‘Mchafu’ (gitaa la bass) ambao wote walikuwa Safari Nkoi. Wakiwa safarini kwenda Tanzania walipitia mji wa Kamina ambako walimpata mnenguaji mwanadada Ngalula Tshiandanda  aliyekuwa akinengua katika bendi ya Sakayonsa ya mjini humo.
Kabeya Badu alikuwa akiwasiliana na King Kiki na akamuahidi kwamba atajitahidi naye aende Tanzania.
Ahadi ya Kiki kwa Kabeya ilitimia baada ya kufika Marquis du Zaire. Safu ya uimbaji ikaonekana kupwaya. Alipendekeza kuongezwa kwa wanamuziki zaidi ili kuimarisha bendi hiyo. Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’ kwa mara nyingine tena akatumwa kwenda Congo kuwaleta wanamuziki waliopendekezwa na Kiki ambao ni watunzi na waimbaji Kabeya Badu na Kalala Mbwembwe, Monga Kiyombo aliyekuwa akipiga gitaa la rhythm na saxophone, Ngoyi Mubenga (tarumbeta), na Khatibu Iteyi Iteyi (saxophone).
Mara tu baada ya kutua Marquis, Kabeya alitunga na kuimba nyimbo nyingi, baadhi yake ni ‘Ndoa ya Kwangu na Mama Kazi’, ‘Pondamali’,  ambazo zilirekodiwa na ‘Kibwe Mutombo’, ‘Muntanda Muli’, ‘Lwembe’ na ‘Maneno’, ambazo hazikuwahi kurekodiwa.
Kabeya Badu alidumu na Marquis du Zaire kwa miaka miwili baadaye mwaka 1980, alichoropoka na kwenda akijunga na King Kiki katika bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS) iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara maarufu Hugo Kisima.
Akiwa na OSS, Kabeya alitunga na kuimba nyimbo za ‘Nani Atashika Jembe’ na ‘Pole Ndugu’. Wimbo wa ‘Yuyu’ alioutunga ulipigwa na kurekodiwa katika kipindi cha Klabu Raha Leo Show kilichokuwa kikirushwa na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Kabeya Badu alikuwa akihitajika sana katika bendi hizo mbili pinzani wakati huo za Marquis na OSS. Hivyo, akawa mithiri ya ‘muigizaji’ kwa kuhamahama. Alirejea tena Marquis kwa kipindi kifupi kisha mwaka 1986 akatakiwa kurejea kwa mara nyingine tena katika bendi ya Orchestra Safari Sound, wakati huo bendi ilikuwa chini ya uongozi wa Ndala Kasheba na haichukua muda mrefu akatoka na wimbo uliowapagaisha wapenzi wa OSS wa ‘Ziada’. Wimbo huo aliuimba peke yake kwa hisia kali akimlilia Ziada, na ukamuongezea sifa kubwa miongoni mwa waimbaji wa muziki wa dansi nchini Tanzania.
Nyimbo nyingine zilikuwa za ‘Kuruthumu’, ‘Simba Wala Watu Wamevamia Mji’, ‘Mama Mwita’, ‘Kayanda’ na nyingine nyingi.
Kabeya Badu alimwelezea King Kiki kuwa ndiye aliyekuwa anaujua umuhimu wake: “Kiki ndiye aliyekuwa akijua umuhimu wangu katika muziki toka mwanzo hadi akanipachika jina la ‘Changa cha Mkonyoyo’ ikiwa na maana ya ‘Siri iliyofichika’”. Hiyo ilikuwa baada ya Kabeya kutunga wimbo wa ‘Changa cha Mkonyoyo’ uliokuwa na ujumbe mzito lakini haukuwahi kurekodiwa.
Aliondoka OSS na kwenda kujiunga kwa mara nyingine tena na Marquis du Zaire mwaka 1988, lakini hakadumu akachukuliwa na kwenda kujiunga na bendi ya Tancut Almasi iliyokuwa na makazi yake mjini Iringa.
Mwaka 1990 akaamua kurudi kwao Likasi katika Jimbo la Katanga nchini Congo DR. Lakini mwishoni mwa mwaka 1998 alirejea Tanzania na mwaka 1999 akapewa kazi ya kuanzisha bendi ya Magoma Moto Sound ya jijini Dar es Salaam. Bendi hiyo haikudumu sana, hivyo mwaka 2001 akajiunga na bendi ya La Capitale ‘Wazee Sugu’ iliyokuwa inaongozwa na King Kiki.

Mauti
Kabeya Badu alikuwa mwimbaji mahiri katika bendi ya La Capitale aliyewaacha wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi nchini Tanzania wakiwa bado wanamhitaji.
Aliaga dunia Machi 6, 2013 akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa maradhi ya figo, akiwa amefikisha umri wa miaka 68.
Msiba wa Kabeya uliwatia simanzi na majonzi makubwa waombolezaji waliofika katika Hospitali ya Muhimbili kuuaga mwili wake na katika mazishi yaliyofanyika katika Makaburi ya Kinondoni Machi 7, 2013. Watu walibubujikwa na machozi mara walipoona mwili wake ukishushwa kaburini.
Tangu alipoanza safari yake katika muziki, Kabeya Badu kamwe hakuwa mtu mwenye soni. Alikuwa tayari kuiacha bendi na kwenda nyingine wakati wowote ule, ili mradi maslahi yawe mazuri kwa sababu muziki kwake ndiyo ilikuwa ajira.
Wakati mauti yanamfika, Kabeya Chibangu Badu aliacha mjane na watoto nane, kati yao watano ni wa kike.

Wasifu
Jina: Kabeya Chibangu Badu
Kuzaliwa: Januari 22, 1945
Mahali: Likasi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Bendi alizopitia: Ricco Jazz, Lupe Jazz, Amide Success, Santa Fee, Lupina Nationale, Lupe Revolution, Baba Nationale, Festival du Zaire, Orchestra Safari Nkoi, Buka Buka Mabele, Marquis du Zaire, Orchestra Safari Sound, Tancut Almasi, Magoma Moto Sound,
Nyimbo alizotunga: ‘Ndoa ya Kwangu na Mama Kazi’, ‘Pondamali’, ‘Kibwe Mutombo’, ‘Muntanda Muli’, ‘Lwembe’ na ‘Maneno’ (Marquis); ‘Nani Atashika Jembe’, ‘Pole Ndugu’, ‘Yuyu’, ‘Ziada’, ‘Kuruthumu’, ‘Simba Wala Watu Wamevamia Mji’, ‘Mama Mwita’, ‘Kayanda’, ‘Changa cha Mkonyoyo’ (OSS).


Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Ukinakili tafadhali taja chanzo hiki.

Comments